Na Elizabeth Mayemba
KAMATI ya Mashindano ya Shiriksho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imeikata maini klabu ya African Lyon inayodai kwamba mchezaji Mbwana Samatta aliyeingia
mkataba wa kuichezea Klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)kwamba ni mali yao.
Uongozi wa klabu ya African Lyon, jana ulikakariwa na vyombo vya habari kwamba Samatta ni mali yao na alikwenda kuichezea Simba kwa makubaliano ya msimu mmoja, hivyo fedha watakakazolipwa Simba na TP Mazembe zote ni za kwao.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya TFF, Sad Kawemba alisema wao wanatambua kuwa Samatta ni mchezaji halali wa Simba kwa kuwa wana mkataba halali, unaoonesha mchezaji huyo ni wa Simba.
"Sasa kama Samatta ni mchezaji wa African Lyon ataichezeaje timu ya Simba, sisi tuna mkataba wa Samatta, ambao unaonesha kuwa ni mchezaji halali wa Simba, hayo mambo mengine hatuyajui," alisema Kawemba.
Alisema kama mchezaji huyo alikuwa amekwenda Simba kwa mkopo, kanuni zipo wazi na ingeonesha kwamba mchezaji huyo ni mali ya African Lyon, lakini hakwenda Simba kwa mkopo.
Aliongeza kwamba na kama kweli, Samatta si mchezaji wa Simba basi klabu hiyo ingefutiwa matokeo ya mechi zote alizocheza mchezaji huyo katika Ligi Kuu Bara.
Kawemba ameishauri African Lyon, kutafuta wachezaji wazuri zaidi ya Samatta ili waweze kuwauza na si kuanzisha malumbano ambayo hayana msingi wowote katika maendeleo ya soka.
Kwa upnde wake Katibu Mkuu wa African Lyon, Brown Ernest alisema kulikuwa na makubaliano maalumu kwa mchezaji huyo, lakini Simba walikuwa wanawakwepa kukaa meza moja kumalizana.
'Kila tulipokuwa tunawatafuta wenzetu wa Simba walikuwa wakituchenga kwa kuwa Samatta, ana mkataba na African Lyon unaomalizika Juni mwaka huu, hivyo sisi tunatambua kuwa ni mali yetu, na wala hatukumntoa kwa mkopo Simba," alisema Brown.
Kwa upende wake Simba, wamesema kwamba Samatta ni mali yao na kwamba walifuata taratibu zote za usajili pamoja na kuzungumza nao wakiwepo TFF.
No comments:
Post a Comment