*Mrope achukua nafasi ya Ngassa
Na Addolph Bruno
TIMU ya soka ya taifa 'Taifa Stars', inaondoka nchini kesho alfajiri kwenda Msumbiji huku ikimkosa mshambuliaji wake Mrisho Ngassa, kutokana
na kuwa na maaumivu ya mguu na nafasi yake kuchukuliwa na Julius Mrope.
Stars itamenyana na Msumbiji, Jumamosi katika mchezo maalumu wa kufungua Uwanja mpya wa kisasa wa nchi humo.
Katika mechi hiyo Stars pia itaitumia kujiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya Afrika ya Kati ya kutafuta tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwakani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja wa timu hiyo, Leopard Tasso alisema Ngassa hatakuwemo katika kikosi hicho kutokana na kuumia juzi wakati akiichezea timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23 'Vijana Stars' ilipocheza na Uganda katika mechi ya kutafuta tiketi ya kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana.
Alisema nafasi yake imechukuliwa kiungo wa Mtibwa Sugar Julius Mrope, ambaye tayari ameanza mazoezi na Stars baada ya Ngassa kuumia na kwamba hali ya wachezaji wengine walioitwa zimeendelea kuwa salama.
"Tunaondoka alfajiri ya Aprili 22 (kesho) na wachezaji 20, pamoja na benchi la ufundi la watu 10 na hadi kufikia leo (jana) maandalizi yanaendelea vizuri na tunatarajia hali itaendelea kuwa hivi," alisema Tasso.
Alisema timu hiyo inaondoka ikiwa na lengo moja la kushindana kuibuka na ushindi, ili kujiwekea mazingira mazuri kushinda katika mechi ya marudiano dhidi ya Afrika Kati itakayochezwa kati ya Mei na Juni mwaka huu nchini ugenini, baada ya awali kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Ofisa habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa Stars itamaliza mazoezi leo jioni, kabla ya kuondoka kesho ambapo msafara huo utaongozwa na Makamu wa Kwanza Rais wa TFF, Athumani Nyamlani.
No comments:
Post a Comment