Na Mwandishi Wetu
BENKI ya Exim imesema itaendelea kuweka nguvu ya kusaidia mambo mbalimbali ya
kijamii, ikiwemo michezo kama mojawapo ya majukumu yake
mbali na yale ya kibenki.
Meneja Mkuu wa benki hiyo, Dinesh Arora aliyasema hayo juzi jioni katika fainali
za mchezo wa kriketi ya ETG, yaliyofanyika katika viwanja vya Leaders Dar es
Salaam ambapo benki hiyo ilikuwa miongoni mwa wadhamini.
Pamoja na udhamini wake kwa michuano hiyo, Arora alizitaka sekta nyingine
binafsi kuingia katika udhamini wa michezo hususani kriketi, ili kupanua wigo wa
ushindani wa michezo nchini na hatimaye kupata wawakilishi wengi zaidi katika
michuano ya kimataifa.
“Tuna programu maalumu za kusaidia mambo mbalimbali ya kijamii, ikiwemo michezo
kama moja ya majukumu yetu lakini pamoja nasi tunawaomba wadau wengine katika
sekta binafsi kusaidia michezo, ili kuongeza wigo wa ushindani na kupata
wawakilishi wengi zaidi katika michuano ya kimataifa,” Alisema Arora.
Alisema pamoja na udhamini wa mashindano, vyama vya michezo husika vinahitaji
kusaidiwa kupata vifaa vya kisasa vya michezo yao na kwamba serikali pekee
haiwezi kuyafanya yote hayo, hivyo kuna haja ya kipekee kwa wadau wengine
kuongeza nguvu katika hilo.
“Serikali imekuwa ikijitahidi kwa kadri ya uwezo wake kuhakikisha michezo yote
inakuwa katika kiwango cha kuridhisha nchini, lakini bado ipo haja kwa wadau
husika kuongeza nguvu ili vyama husika viweze kuwakilisha vizuri katika ngazi za
kitaifa na kimataifa,” alisema Arora.
Katika michuano hiyo timu ya Caravan waliibuka washindi kwa ‘37-run’ na
kupatiwa kombe ikifuatiwa na Azam ambapo wachezaji Sreejith, Rahul na
Sathish waliisaidia kwa kiasi kikubwa timu ya Caravan kuibuka na ushindi katika
michezo hiyo.
Timu nyingine zilizoshiriki katika michuano hiyo ni ETG Pioneers,
Insignia, Pako Steers CC, Seikh XI, Patel Brotherhood, Vin Mart, IMTU, Madras
Monsters, Indian Fighters, Friends XI, Indian Tigers and Dolphin XI.
No comments:
Post a Comment