Rehema Mohamed na Angelina Mganga
MFANYABIASHARA Erick Lugeleka amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za wizi pamoja na utakatishaji fedha haramu sh. bilioni 3.8 mali ya
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Frank Moshi na kusomewa mashtaka yake na Wakili wa Serikali, Bw. Ladslaus Komanya.
Akisomewa mashtaka hayo katika kosa la kwanza, Bw. Komanya alidai kuwa Juni 6, 2008 jijini Dar es Salaam mtuhumiwa aliiba sh. 960,148,290.15 mali ya TRA.
Katika kosa la pili ilidaiwa kuwa Septemba 18, 2008 jijini Dar es Salaam mtuhumiwa aliiba sh. 1,426,450,684.05 na katika kosa la tatu anatuhumiwa kuiba sh. 1,415,418,801.37 ambapo fedha hizo zote ni mali ya TRA.
Kosa la nne analokabiliwa nalo mtuhumiwa huyo ni kubadili sh. 960,168,290.15 ili zionekane halali (kutakatisha) alilolifanya kati ya Mei na Juni mwaka 2008.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alihamisha fedha hizo kutoka katika akauanti namba 0120103000711 ya TRA katik Benki ya NBC tawi la Samora kwenda akaunti namba 07410300033 ya Kampuni ya Excel Media, 074103000112 ya kampuni ya Express Booking Enterprises, 074103000276 ya kampuni ya TAC Traders Limited na akaunti 074103000100 ya kampuni ya Daima Phamarceuticals.
Katika kosa la tano mtuhumiwa alitakatisha sh. 1,426,450,684.05 kati ya Septemba na Oktoba mwaka 2008 jijini Dar es Salaam.
Ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alihamisha fedha hizo kutoka akaunti 012103000711 ya TRA benki ya NBC tawi la Samora na kuzihamishia katika akaunti 07410300033 ya kampuni ya Excel Media, 074103000112 ya kampuni ya Express Booking Enterprises, akaunti 074103000276 ya kampuni ya TAC Traders Limited na akaunti 074103000100 ya kampuni ya Daima Phamarceuticals. Akaunti hizo zote ni za benki ya NBC.
Mtuhumiwa huyo alikana makosa hayo yote ambapo mwendesha Mashtaka Bw. Komanya aliiomba mahakama itoe tarehe ya kutajwa kesi hiyo kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu Bw. Moshi aliiambia mahakama kuwa mtuhumiwa huyo atapelekwa rumande kutokana na kosa la nne na tano kutokuwa na dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 4, mwaka huu.
Wakati huo huo Hakimu Mustapha Siyani anayesikiliza kesi ya mshitakiwa Bw. Shida Luanda kutoroka mahabusu ametoa onyo kwa askari magezeza wanaopeleka mahabusu hao mahakamani hapo kwa kutofuata maagizo yanayotolewa mahakamani
Bw. Siyani alitoa agizo la mshtakiwa huyo kutofungwa mnyororo miguuni akiwa mahakamani kwa kuwa ni kinyume na sheria na ni sawa na kumhukumu kuwa tayari ameshatenda kosa.
Msitakiwa huyo alifungwa pingu miguuni wakati akipandishwa kizimbani, na kabla kesi haijaanza kusikilizwa alinyoosha kidole na kumwambia hakimu kuwa pingu za miguuni zinambana.
Askari Magereza walipotakiwa kumfungua pingu hizo walidai kuwa funguo hawazioni na huenda wamezisahau gerezani Keko
Kutokana na hali hiyo hakimu aliamua kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 3, na kuwaonya askari hao kutorudia kitendo hicho.
No comments:
Post a Comment