14 April 2011

Shivji awataka vijana kudai mabadiliko

Na Tumaini Makene

MMOJA wa mabingwa wa sheria, ambaye pia ni Profesa wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu Dar es Salaam, Issa Sivji, amesema wananchi, hasa vijana, ndiyo
wanatakiwa kuwa cheche ya kudai mabadiliko na kuikomboa nchi, hasa katika zama hizi ambapo viongozi wanatumia madaraka yao kujitajirisha.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa mapumziko ya Kongamano la Wiki ya Mwalimu Nyerere lililoanza juzi katika Ukumbi wa Nkrumah, Prof. Shivji alisema kuwa baada ya 'kuuawa' kwa Azimio la Arusha, viongozi nchini sasa wanatumia nafasi zao kujitajirisha, huku wananchi ambao walipigania uhuru wa nchi, wakiachwa kando.

Prof. Shivji aliyasema hayo alipozungumzia uamuzi wa Kigoda cha Mwalimu kuchapisha Kitabu cha Azimio la Arusha na kuendelea kukigawa bure kwa wananchi licha ya azimio hilo kuuawa miaka ya tisini, baada ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukutana Visiwani Zanzibar.

Alisema kuwa wakati wa kuadhimisha miaka 30 ya CCM, chama ambacho kimekuwa madarakani tangu uhuru, wananchi walisikika wakikumbuka azimio hilo wakisema kuwa liliwajali watu wanyonge, kwa kuwa lilizungumzia utu wa binadamu, miiko ya uongozi na maendeleo ya watu kwa ujumla, hivyo linastahili kurudishwa.

"Kimsingi sisi tunachapisha tu hili azimio na kulisambaza kwa watu, lakini ni wananchi wenyewe, tena ninyi (waandishi wa habari) ndiyo mliwauliza na wakasema kuwa Azimio la Arusha liliwajali wanyonge, lilizungumzia misingi ya utu wa binadamu na maendeleo, lakini sasa viongozi wameliacha na wananchi wamewekwa pembeni.

"Mimi kwa kweli wakati mwingine nasita hata kuwaita hawa ni viongozi...maana kiongozi ni yule anayeona majukumu ya kuwatumikia watu. Hawa wanatumia madaraka ya kisiasa, wanatumia vyeo vyao kujitajirisha, wanapenda madaraka...kiongozi wa kweli ni yule asiyependa kuongoza, asiyekimbilia madaraka, maana anauona uongozi ni majukumu. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema hili, kiongozi ni yule asiyeona utamu katika madaraka, anaona majukumu, kiongozi ni yule anayekataa madaraka.

"Wanatumia madaraka kujitajirisha na kuwasahau wananchi. Sasa ni wakati mwafaka kwa wananchi, hasa vijana kuichambua jamii yao, kutafakari, historia ya nchi yao, wapi tulikotoka, tunakwenda wapi, vijana ndiyo wanapaswa kuwa cheche ya kuikomboa nchi yao wenyewe," alisema Prof. Shivji.

5 comments:

  1. AHSANTE PROF. SHIVJI KWA KUTUFUNGUA MACHO VIJANA. VIJANA TUAMKEeeeeeeeeeeeee

    ReplyDelete
  2. Akhsante Prof...wewe ni mwanazuoni wa ukweli! Mungu akupe maisha marefu uione tanzania mpya.

    ReplyDelete
  3. Ahsante Prof. Shivji. Vijana wenzangu tunangoja nini? Tushikamane sote, tuikomboe nchi yetu toka mikononi mwa hawa viongozi wasiotujali. Wakati wa kuikomboa nchi yetu ndo huu.

    ReplyDelete
  4. Shivji shukran sana na hawa wafuasi wa Chadema ungewaeleza historia jinsi gani Mwalimu alivyojali watu hadi kumtimua Mtei kazini kwa kukubaliana na mabeberu,ati leo mzee huyu siku moja kwenye mkutano wa Chadema Moshi akihutubia anawaambia wafuasi wa chama hicho kuwa alifukuzwa kazi na Nyerere kwa sababu alipingana na Nyerere ambaye alitaka mashirika ya umma yauzwe yeye Mtei akakataa,huyu Mtei mnafiki sana, mimi nilikuwa nasoma enzi hizo nikasikia kwenye Radio Tanzania wakati ule kuwa Mtei katimuliwa kazi kwa kukubaliana na IMF na Benki ya Dunia ambao walitoa masharti kwa Nyerere aache kutoa matibabu bure,elimu bure,auze mashirika ya umma.Mwalimu Nyerere alikataa na hawa mabeberu wakamkatia misaada na wakamchukua kibaraka wao Mtei wakampa kazi katika benki ya dunia. ati mzee huyu leo bila aibu wala haya anasema aligombana na mwalimu kwa yeye Mtei kukataa mashirika ya uma yasiuzwe. Watanzania tuwe macho sana na wanasiasa hawa wa leo ni wanafiki sana, Enzi za mwalimu mfanyakazi wa kima cha chini aliongezwa mshahara zaidi ya mwenye kipato cha juu,leo bungeni hapo hao chama tawala na upinzani mshahara ni million saba kwa mwezi na mtu wa kima cha chini ni shilingi laki moja,oneni maajabu haya,mbunge akiingia bungeni tu mkopo milioni 200 na milioni 90 za kununulia magari,halafu nyie wananchi mnapigwa porojo na wanasiasa mnawapigia makofi. WAOGOPENI SANA HAWA WANASIASA WA SASA,SHIVJI KAWAPA SOMO MDAI MABADILIKO MSIDHANI MABADILIKO NI KUITOA CCM TU MADARAKANI HAPANA MDAI MABADILIKO YATAYONUSURU NCHI NA WANASIASA WALIOGEUZA SIASA BIASHARA NA LESENI YAKE NI KUWA NA UWEZO WA KULAGHAI WATU

    ReplyDelete
  5. KWA CHENGE, LOWASA NA ROSTOM-KWA VILE MZEE MAKAMBA ANAFURAHI KWAMBA AMETOKA NA WENGI NDANI YA KAMATI KUU, BASI KWA NJIE HAMNA LA KUFAYA NI KUFANYA MCHEZO MMOJA WA KUFA KWA WENGI NI HARUSI, KWA MAANA HIYO KWA VILE CHENGE UNAWAJUWA WATU WOTE MLIOGAWANA MSHIKO WA RADA NA WEWE WAWEKE HADHARANI NAO WATOLEWE NDANI YA CHAMA, PIA MZEE LOWASA KWA VILE UNAWAJUWA WALE WOTE WALIOKUKATIA MSHIKO WA RICHMOND BASI USIKUBALI KUFA PEKE YAKO, WATAJE WOTE NAO WATOLEWE CCM, NA PIA MHESHIMIWA ROSTOM WEWE NDIYO JEMBE, WALIME WOTE UNAOWAJUWA KUWA ULIWAPA MSHIKO ILI KUPITISHA DEAL ZAKO, USIKUBALI KWENDA MWENYEWE, HUONI MAKAMBA, NI LAZIMA UWE SHUJAA USIFE KIVYAKO KUFA NAO WOTE WALIOPOKEA FEDHA KUTOKA KWAKO

    ReplyDelete