14 April 2011

Makinda apata wakati mgumu bunge

Na Edmund Mihale

VIJEMBE, ubabe wa kurushiana maneno jana viliibuka katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma baada ya Mwanasheria wa Serikali (AG), kumtaka Spika wa
Bunge hilo, Bi. Anne Makinda kumtoa nje Mbunge wa Nyamagana, Bw. Ezekia Wenje (CHADEMA).

Mzozo uliibuka baada, Bw. Wenje kugoma kufuta kauli aliyoitoa katika ukumbi huo ikidaiwa ni ya udhalilishaji wakati bunge hilo lilipokuwa likichagua Mwenyekiti wa Bunge ambaye hutoka kati ya Wenyeviti na Makamu wa Kamati za Bunge. Wagombea wa nafasi walikuwa Bi. Jenista Mhagama (Peramiho-CCM), Bw. George Simbachawene (Kibakwe-CCM) na Bw. Sylvester Mabumba (Dole-CCM).

Bw. Wenje alisimama na kuomba kutoa taarifa kwa Spika na kuhoji makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi ambapo alisema kwamba yalivunja Kanuni ya Bunge namba 11.

Aliyafananisha makubaliano hayo kama kitu kisichofuata utaratibu ‘dark market’ kwa kuwa aliwasilisha majina matatu badala ya sita kama kanuni hiyo inavyoeleza.Bi. Makinda alisema kuwa wenyeviti wa kamati na makamu wao walikuwepo kwenye kikao hicho, bali walikataa kugombea kwa kuwa hawana ubavu wa kumudu nafasi hizo.

"Katika kikao hicho kulikuwa na wawakilishi kutoka upande wa serikali, kiongozi wa upinzani bungeni pamoja na makamu wake na wote baada ya kukosa wagombea sita walikubaliana na majina ya wagombea hao watatu yapitishwe kugombea," alisema Bi. Makinda.

Wakati hayo yakiendelea, Mbunge wa Kigoma Mjini, Bw. Peter Serukamba (CCM) alisimama na kuomba mwongozo wa Spika ambapo alimtaka Bw. Wenje kufuta kauli yake kwa kukiita kikao cha Kamati ya Uongozi kuwa kilikuwa ni ‘dark market.’

Bi. Makinda alikubaliana na hoja hiyo na kumtaka Bw. Wenje kufuta kauli yake lakini Bw. wenje alisema ameeleweka vibaya na kwamba alichomaanisha ni mchakato wa kuwapata wagombea kuwa ulikuwa hakueleweka na sio kwamba kikao alichokiongoza spika.

Wakati akitoa ufafanuzi huo sauti za wabunge wa CCM zilisikika zikimtaka afute kauli yake la sivyo atolewa nje.

“Futa kauli au utolewa nje, mtoe nje huyo! Mtoe nje huyo! hana adabu huyo!  Sauti za baadhi ya wabunge wa CCM zilisikika huku kwa upande wa upinzani wakisema, “Usifute kauli na hatoki mtu nje hapa.”

Mzozo wa kuzomeana na kurushiana vijembe uliendelea na kufanya spika kupata wakati mgumu wa kuwatuliza wabunge.Hata hivyo, kelele za kumataka Bw. Wenje kutoka ziliendelea, na mbunge ambaye hakutambulika alisikika akisema 'fungeni milango tupigane, hao CCM hawana adabu kabisa’.

Spika alionekana kupatwa na hasira na kufoka huku akiwataka wabunge kukaa kimya.

“Naomba wote mkae kimya. Waheshimiwa wabunge mnafanya ujinga, wananchi waliowapigia kura wanawaoneni mnavyofanya,” alisema na kuongeza, “nchi nzima inawaona mnafanya mambo kama vile hamna akili sisi wote ni watu wazima," alisema lakini kauli hiyo haikufua dafu.

Spika alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, kufafanua hatua za kuchukua dhidi ya Bw. Wenje, naye bila kuzungumza maneno mengi alisema aitwe 'Sergent at Arms' akiwa na maana askari alindaye bunge na kubeba Siwa kumtoa nje ya ukumbi wa bunge, Bw. Wenje iwapo ataendelea kukaidi amri ya spika.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA), alipopata nafasi ya kuzungumza alifafanua yaliyojiri kwenye kikao ambacho Spika alikiongoza na kufikia kuwateua wagombea hao watatu.

“Ni kweli tulikubaliana, lakini wagombea hao hawakuchukua fomu kama inavyotakiwa,” alisema na kisha kuzungumzia suala la Wenje, kuwa sio sahihi kikao cha Spika ni ‘dark market’ lakini pia sio sahihi kuyachukulia maneno ya Bw. Wenje bila kuyatafsiri, na sio sahihi pia kuchukua sergent in arms na kumtoa nje.”

Hata hivyo, kelele za kumtaka Bw. Wenje kufuta kauli yake na kutaka atolewe nje ziliendelea kusikika kutoka kwa wabunge wa CCM, huku CHADEMA wakisisitiza kuwa hatoki mtu ndani ya ukumbi huo.

"Hatoki mtu humu, tutatoa wote! Hakuna wa kutoka! na upande wa CCM wakasikika wakisema 'mtatoka hamna adabu nyie', lazima atoke."
 
Spika Makinda alionekana kufura kwa hasira alisimama tena na kumtaka Bw. Wenje kufuta kauli yake huku akihoji haitamgharimu kiasi chotechote iwapo atafuta kauli hiyo.

Baada ya hapo Bw. Wenje alisimama na kufuta kauli yake lakini alisema alichomaanisha ni ule mchakato.

"Kama dark market ni kosa basi White Maarket," alisema Bw. Wenje.

Baada ya Bw. Wenje kufuta kauli yake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. William Lukuvi alisimama na kutengua kifungu cha 11 cha Kanuni ya Bunge kinachotaka majina ya wagombea wa nafasi ya wenyeviti wa bunge kuwa sita, ambacho Bw. Wenje alisema kimekiukwa.

Kifungu hicho kilipotenguliwa vurugu zilisimama na kikao kuendelea, Bi. Makinda aliwasilisha majina hayo matatu ili wabunge wayapigie kura.Kabla ya kuyapigia kura majina hayo, wabunge walifanya uchaguzi wa wabunge wanatakaowania nafasi za ubunge katika Bunge la African kwa kuwapigia kura za siri.

Nafasi ya Mwakilishi wa Bunge la SADC ilichukuliwa na Bi. Stella Manyanya (CCM) na kwa Taasisi ya APRM ilishinda Bi. Martha Umbulla (CCM).

14 comments:

  1. huyo mama asiwatishie hana lolote amewekwa hapo kwa maslahi ya mafisadi ili awalinde msimuogope huyo

    ReplyDelete
  2. Huyo mama atasonga mbele tena spika songa mbele wasikuchezee hyao wapinzani, wasikubabaishe hao wewe fuata sheria na usipindishe mwendo mdungo hongera Makinda, usitishwe na hao ambao wameingia juzi hawajasoma sheria za bunge, mwendo mdundo tuu.

    ReplyDelete
  3. Makinda kama anajua hali za watanzania wengi, zilivyo ci wakati a kubebana, hivi black market hamnazo nyie??? , au mnalinda kivipi???, lengo lenu ni kupunguza kasi ya kuhojiwa ili muundelee kuiba.

    ReplyDelete
  4. ukweli kama umesikiza live majibishano ktk bunge hapo jana ni utoto mtupu yaana watu wazima tunaowategemea wote walikuwa ni mazuzu hv kwa mtaji huu tunategemea vizazi vipya wawe na mfano gani?Au watatoa uamuzi au sheria zipi za kumlinda mwananchi? Yaani si CCM wala CDM na wote wapinzani waliokuwa na busara ni Mavuvuzela watupu, inasikitisha sana inabidi Taifa kwa pamoja tuwakemee hawa tumewachagua kwa ridhaa yetu wenyewe wamekuwa kama watoto wadogo. Maneno yaliyokuwepo jana atoke nje,hatoki mtu hapa,tokeni woote,funga milango tupigane makondee, mmezoea kutuburuza nk,

    ReplyDelete
  5. Bunge la Watanzania linaanza kufanya mambo kama wahuni wa mitaani,inatisha jamani!!hii kauli ya kupigana inayotolewa kila mara na baadhi ya wanasiasa wana maana gani? kwa nini wabunge wasikubali kutii kanuni za bunge na kama kuna kasoro katika kanuni hizo kwa nini wasijadiliane zirekebishwe kuliko kuonesha ubabe usio na maana bungeni?,wabunge wanatuabisha!

    ReplyDelete
  6. Tatizo baadhi ya walioingia bungeni ni wahuni na si wasomi na hata hao waliosoma wanamezwa na wasomi,hata ukifatilia ktk mijadala wengi wanazungumza pumba na hii inachangiwa na kutokuwa makini ktk kuwachaguwa wabunge wetu na hata hao walioteuliwa pia nao ni pumba nyingi.Ukifatlia huwezi fikiri kuwa hao ndio watunga sheria zetu na wanaopigania maslahi ya nchi na raia zake.Ni wanaiga mambo ya KITOTO, na hawasomi kanuni au hawana maadili mema

    ReplyDelete
  7. Chanzo kikkubwa ni Makinda kukiuka kanuni za bunge. Sijui ndo spika gani tena huyu. Tunamkumbuka sana Sita.

    ReplyDelete
  8. Ati fungeni milango tupigane! Mhe Uliyetoa hii kauli HUNA SIFA ZA KUWA KIONGOZI. Its quite unfortunate for our country.

    ReplyDelete
  9. bunge sasa limeanza kukomaa.HONGERA WABUNGE WETU KUKATAA KUSIMAMIA UPUMBAVU

    ReplyDelete
  10. Mimi ni yule yule Hafidh -mwanaharakati kutoka visiwa vya Amani- Zanzibar.
    Ndugu zangu kilichotokea jana katika Bunge letu kuhusu uchaguzi wa W/Viti. Naweza kusema kua Spika alienda kinyume na maandiko ya kanuni za kibunge, alichokua anataka kufanya ni kuridhia makubaliano yaliofanyika katika kikao chao cha wenyeviti. Sasa kumbukeni katika ukumbi ule kuna wabunge wengi walikua hawapo ktk hicho kikao na ktk muongozo au tarifa hakuweza kuelelzea mwanzo ! sasa kwa akili ya kawaida lazima atanyanyuka mtu ahoji kua kwa nini kanuni zinapindishwa kwa mujibu wa maandiko ya kikanuni za kibunge / ndicho alichofanya Mh. Raya. Sasa baada ya kujishukia Spika ndipo aliposema mbunge alienyanyuka kawahi ! kwa hiyo source of this issue is Madam Spika.

    ReplyDelete
  11. Hayo yote yanatokana na uadilifu kupotea katika utawala wa sasa na ukiangalia vizuri utaona wabunge wengi hawaangalii hoja za msingi, Maana wengi ni mashabiki tu hawana hadhi ya kuitwa wabunge,!! Na kwa hivyo hufanya mambo ya kuwafurahisha wakubwa zao illi kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuendelea kula kwenye vyama vyao, Wananchi wa Tanzania wamechoka sana kuendelea kuona Mijitu mijinga mipuuzi inayoendelea kupokea mishahara inayo tokana na wavuja jasho wa Tanzania hata kazi wanayo ifanya haionekani, Hili liatawagharimu sana baadae, Kutokana na serekali kutokua makini kwa sasa, Lakini pindi itakapopatikana serikali madhubuti basi wawe tayari kulipa fidia za maumivu walio sababisha kwa wana Nchi.

    ReplyDelete
  12. WAFANYEJE SASA MAMILONI WALIOJIGAWIA WAKATI WA KUANZA BUNGE NDIO INAWATIA WAZIMU,ZITTO KASEMA WAZI KUWA WALIKUWA WOTE NA WALIOPATIKANA KUGOMBEA NI WATATU TU KIPI TENA KINATAKIWA? NI BUNGE LILIJAA WAPUMBAVU WANAOPIGA MAZZUVELA,HAWAKAI WAKAPANGA MIKAKATI YA KUWAONDOA WANANCHI WAO KWENYE UMASIKINI WAMEGEUZA NI USANII WA MIPASHO ILI WATU WAKIWAONA WASEME FULANI BWANA BOMBA SANA.

    ReplyDelete
  13. Waheshimiwa sana tunawaomba muwe na heshima ndani ya hilo Jumba, la sivyo sisi tutaona kuwa tunawakilishwa na MAPEPO badala ya wabunge tuliowachagua!! Kuweni makini la sivyo hii iktakuwa ndio safari yenu ya mwisho!!

    ReplyDelete
  14. Mimi ni yule yule Hafidh mwanaharakati kutoka Zanzibar. Naomba nichangie kitu ambacho kimetokea siku ya Jmosi -16 April katika Bunge letu hii ni kali ya mwaka !!! Ndugu zangu ni kweli wenye akili wamesema " Mwisho wa maji ni tope" leo nilikua nafatilia marekebisho ya sheria za Kimahakama, wakati Mh. Tundu Lisu akiwa amepeleka marekebisho ya sheria hii nakutoa hoja zake pale sheria hii inapojadiliwa kifungu kwa kifungu,KALI YENYEWE NI HII:- Kuna mbunge yawezekana akawa anatoka CCM amemuambia Mh. Tundu Lisu kua hachoki kusimama na kujenga hoja !! dahh hapa hamna kitu kweli kuna mijitu inakula jasho la wanyonge kwa maslahi binafsi, Mh huyu inaonyesha kweli ni mvivu, mzembe na mbinafsi asiejali waliowengi.anachotaka yeye mambo yapelekwe pelekwe tu bila ya mazingatio. yeye anaona kero kujadili maslahi ya umma kwa manufaa ya umma anaona bora yapelekwe pelekwe ili akapumzike akatafute kuku na pilau avimbishe tumbo halaf ajigambe hahah mimi ni mheshimiwa !! kwa mwendo huu hatufiki baba.

    ReplyDelete