Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imeanza jitihada ya kutafuta soko kwa ajili ya tani 50,000 za tumbaku ambazo zimekosa soko la ndani.Akizungumza juzi jioni, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na
Masoko, Bw. Lazaro Nyalandu ambaye aliongoza msafara wa Tanzania katika kutafuta soko nchini Iran alisema mazungumzo yamefanyika na ana matukmaini tumbaku hiyo itapata soko.
“Nilikuwa nchini Iran katika ziara ya siku mbili kuiwakilisha serikali katika kutafuta soko la tumbaku ili kuboresha kilimo hiki, hii inatokana na Tanzania kuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji wa mazao hali ambayo inaibua changamoto katika soko,” alisema Nyalandu.
Aliongeza, “Tani 90,000 tayari zimeshapata soko hapa hapa nchini lakini tani 50,000 ni tumbaku ambayo bado haijapata soko, hivyo jitihada zinafanyika ili kupata soko nje ya nchi.
Alisema kwa mujibu wa wataalamu, licha ya kuwa tumbaku inayouzwa nchini Iran nyingi inatokea nchini Zimbabwe na China, lakini inayozalishwa Tanzania ina ubora wa aina yake.
“Hivi sasa tunataka kujaribu soko la China na Uturuki, ila kama makampuni ya ndani yataweza kununua tumbaku yetu hilo litakuwa jambo jema, lakini kama watashindwa serikali ni lazima ifanye juhudi za kutafuta soko la nje ya nchi,” alisema Nyalandu.
Huku akizungumzia mpango wa serikali kutafuta soko la mazao mchanganyiko Nyarandu alisema, "Serikali ipo katika mpango wa kutafuta mwekezaji katika usindikaji wa matunda, kwa kuwa usafirishaji wa matunda yenyewe ni kazi mgumu kutokana na kuharibika haraka.
No comments:
Post a Comment