14 April 2011

Serikali yafanya sensa ya mamba

Na Dunstan Bahai

SERIKALI imesimamisha kwa muda utoaji wa vibali vya uvunaji mamba hadi kazi ya kuwahesabu inayoendelea sasa itakapo kamilika."Huu ni msimu wa
kuwahesabu, tukimaliza wale wote walioomba kuwavuna tutawaarifu na kuwapa vibali hivyo. Kwa sasa tunaendelea na kazi ya kuwahesabu.

"Siyo kwa mamba tu, hata wanyamapori wengine, lakini pia na miti. Tunafanya hivyo baada ya kuona kuna uvunaji holela unaohatarisha kupotea kwa viumbe hao," alisema msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. George Matiko.

Bw. Matiko alisema Wizara inafanya sensa ya mamba ili kupata taarifa endelevu na kwamba wafanyabiashara wa mamba wote wamekwisha arifiwa kwa barua na utaratibu huo ukikamilika pia watawaarifu kwa barua kwa ajili ya kuanza kwa kazi hiyo.

Kauli hiyo ya serikali imekuja baada ya baadhi ya wafanyabiashara kufika katika ofisi za gazeti hili kulalamika kwamba serikali imezuia kutangaza utaratibu wa uvunaji wa mamba hao.

Mmoja wa wafanyabiashara hao ambaye alikataa kutaja jina lake kwa madai anaweza kunyimwa kibali, alisema serikali kushindwa kutoa vibali hivyo, upo uwezekano wa mamba kuua, kujeruhi na kuharibu mali za watu kwa mwaka huu kutokana na kuwa wengi.

Alisema kila mwaka wizara kupitia idara ya wanyama pori hutoa vibali vya kuuawa kwa mamba 1,500 kwa kampuni 30 zinazofanya biashara hiyo.

Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, kutotoa kibali mwaka huu, mbali na mamba kusababisha uharibifu na vifo, serikali pia itapoteza sh. milioni 60 ambazo huzipata kila mwaka kutokana na malipo sh. 40,000/- kwa kila mamba.

Alisema wafanyabiashara hao pia watayumba kimapato kwa kuwa wengi wao kukopa fedha kwa ajili ya kazi hiyo lakini pia ajira za Watanzania takribani 1,200 zitakuwa mashakani.

"Hawa maliasili tukiwauliza hakuna majibu ya maana wanayotupa, kila ukienda unaambiwa subiri kwanza, sasa subiri kwanza hadi lini?" alihoji mfanyabiashara huyo.

Soko la ngozi ya mamba lipo Singapore, Japan, Ufaransa, Ubelgiji na wamekwisha pata soko la nyama China.

No comments:

Post a Comment