LONDON, Uingereza
MSHAMBULIAJI Wayne Rooney ambaye aliifungia timu yake ya Manchester United mabao matatu katika ushindi wa magoli 4-2 dhidi ya West Ham, ametamba kuwa
msimu wao wa Ligi Kuu ndiyo umeanza sasa.
Rooney aliisifu timu yake, lakini pia alijielezea kuwa amerejea katika kiwango chake baada ya kuanza vibaya akiwa kama mshambuliaji.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25, ambaye pia anachezea timu ya taifa ya England, msimu uliopita alifunga magoli 35 katika mechi 46 alizochezea klabu na nchi yake kabla ya kuumia katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, dhidi ya Bayern Munich.
Aliporejea uwanjani hakuwa katika kiwango cha juu, hata katika michuano ya Kombe la Dunia, Afrika Kusini.
Hali ya kutokuwa katika kiwango cha kawaida ilichangiwa pia na maisha yake binafsi, ambapo alifunga magoli matatu katika mechi 28.
lakini baada ya kuanza mwaka huu alianza kurejesha uchezaji wake na kurudi juu.
Rooney alisema kitendo cha United kutoka nyuma kusawazisha magoli mawili na kisha kuongeza mawili, kinawatia wasiwasi wapinzani wao wanaowania ubingwa.
"Miaka michache iliyopita, wakati Chelsea ilipotwaa ubingwa wa ligi, walionekana wangeendelea kufanya hivyo," alikiambia kituo cha televisheni cha klabu yake MUTV.
Rooney akizungumzia kitendo chake cha kwenda mbele ya kamera ya televisheni iliyokuwepo uwanjani baada ya kufunga goli la tatu katika mechi dhidi ya West Ham, alisema hakukusudia kumsema yeyote, lakini timu za Arsenal na Chelsea zinaweza zikawa zimepata ujumbe.
Kwa sasa United inaongoza kwa pointi saba.
No comments:
Post a Comment