24 April 2011

Rais Shein ataka timu za Ikulu kuimarisha utendaji

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Ali Mohamed Shein, amewataka viongozi na wanamichezo wa timu za Ikulu ya Tanzania Bara na
Zanzibar, kuitumia fursa ya michezo kuimarisha utendaji wa kazi zao.
Rais Shein ametoa kauli hiyo jana,  wakati alipozungumza na wanamichezo hao waliofika ofisini kwake kumsalimia, ikiwa ni miongoni mwa kusherehekea Sikukuu ya Pasaka
Alisema jambo la msingi katika kukutana kwao, wanapaswa kuweka mbele maslahi ya kazi zao kwa kusaidiana, kila upande mmoja unapohitaji kusaidiwa.
“Huu ni utamaduni mzuri ambao tumerithi toka kwa wazazi wetu, walianza na utamaduni wa kutembeleana kifamilia na hata ikaamuliwa kutembeleana kimichezo, hivyo mnapaswa kuudumisha na kuimarisha utendaji wenu wa kazi kwa kusaidiana,” alisema.
Hata hivyo, alisema ziara za kimichezo zililenga zaidi kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kudumisha udugu wa kweli uliopo.
“Kufanyika kwa ziara hizi, mbali na kuwepo kwa malengo makuu, lakini pia kutapunguza mawasiliano ya kiitifaki yaliyokuwa yakitumika, kwani hivi sasa itakuwa yanafanyika kwa njia ya kimichezo,” alisema.

Mapema Mwenyekiti wa klabu za Michezo za Ikulu Zanzibar, Abdul Mohammed Mpechi, alimwelezea Rais Shein kuwa, kukutana kwao na wanamichezo kutoka Ofisi ya Ikulu Bara, kutajenga uhusiano mkubwa kwa pande zote mbili.
“Tumeamua kufanya hivi ili kuendeleza uhusiano mlionao nyinyi viongozi, kwani tumekuwa tukishuhudia mkishirikiana kwa kila jambo, na sisi tumefanya hivi kwa kuwa ndio msingi mkuu wa Serikali zetu mbili, na tunakuahidi kuwa,  umoja wetu tutaufanya kwa uadilifu na heshima kubwa,” alisema.

Nae, Mnikulu kutoka Ikulu ya Tanzania Bara, Shaaban Ngurumo,  alisema kuwa, watakubaliana na Rais kuwa, michezo ni udugu, ushirikiano na sio ugomvi, na watahakikisha kila mmoja anakubali kushinda na kushindwa.
Msafara wa wanamichezo hao kutoka Ikulu Tanzania Bara, unafikia wanamichezo 60, unaongozwa na Mnikulu kutoka Tanzania Bara,  Shaaban Ngurumo na kwa mujibu wa ratiba ya wenyeji wao, msafara huo unatarajiwa kuondoka kesho mchana.

No comments:

Post a Comment