Na Rashid Mkwinda, Mbozi
RAIA wa Afrika Kusini aliyefahamika kwa jina la Harrison Philip(28) ambaye ni msimamizi wa ujenzi wa Kampuni ya Ujenzi ya Consolidated Construction Company (CCC) inayojenga
barabara kati ya Tunduma-Ikana amekutwa amekufa chumbani kwake katika hoteli aliyofikia akiwa na dawa zinazosadikiwa kuwa mihadarati.
Bw. Philip alifariki usiku wa kuamkia Aprili 11 na ndani ya chumba chake namba 106 katika Hoteli ya Mbozi Imperial iliyopo Vwawa mjini Mbozi, kulikutwa na vitu vinavyosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroine kete 8 na bangi gramu 3 na mwili wake uligunduliwa na jamaa zake majira ya saa 1:30 asubuhi.
Ilidaiwa kuwa kabla ya kifo chake, Bw. Philip aliishi katika hoteli hiyo kwa takribani miezi mitatu huku kukiwa na pilikapilika nyingi nyakati za usiku ambapo wageni mbalimbali walikuwa wakiingia na kutoka baada ya saa za kazi hadi usiku wa manane.
"Huyu mzungu alikuwa haeleweki jinsi anavyoonekana ni kama mtu aliyelewa nyakati zote na hakuwa anaingia na pombe ndani ya chumba chake, hatujui ni aina gani ya kilevi aliyokuwa akitumia," alisema mmoja wa wahudumu ambaye hakupenda kutajwa jina lake kwa kuwa si msemaji wa Hoteli hiyo.
Kadhalika imedaiwa kuwa wafanyakazi na vibarua wanaofanya kazi katika kampuni hiyo wamekuwa wakitumia dawa za kulevya aina ya bangi ili kuondoa uchovu wa shughuli za suluba zinazofanywa na kampuni hiyo wakati wa ujenzi wa barabara.
"Unajua kazi hii ni ngumu kinoma, bila kupata stimu huwezi kufanya kazi kwa ufanisi, inabidi unapata stimu kidogo ndipo unaingia mzigoni," alisema kijana mmoja ambaye ni kibarua katika kampuni hiyo.
Akizungumzia mahala wanakopata bangi hiyo kijana huyo alisema kuwa inapatikana hapo hapo kazini na kwamba watu wa chini hutumia bangi lakini wale wa juu hutumia Cocaine, Heroine na Mandrax na baadhi yao hujidunga sindano.
Mwandishi wa habari hizi alifika katika hoteli ambayo raia huyo amefia na kukutana na Meneja wa Hoteli hiyo aliyefahamika kwa jina la Fredrick Lupembe lakini hakuweza kuzungumzia tukio hilo kwa madai kuwa taarifa zote za tukio hilo ziko polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Bw. Advocate Nyombi alithibitisha na kusema kuwa hata hivyo jeshi la polisi linaendelea kufanyia uchunguzi mazingira ya kifo chake ikiwa ni pamoja na kuchukua sampuli ya vitu vinavyosadikiwa ni dawa za kulevya.
Mwili wa marehemu ambao ulikuwa umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya mjini Vwawa, ulisafirishwa jana chini ya ulinzi mkali kuelekea mjini Mbeya ambako inadaiwa utafanyiwa utaratibu wa kusafirishwa kwenda Afrika ya Kusini.
No comments:
Post a Comment