Na Tumaini Makene
WAKATI kilio cha muda mrefu cha wanaharakati na wasiasa wakitaka madaraka ya rais yapunguzwe hakijamalizika, Muswada wa Sheria ya mabadiliko ya
Katiba umezidisha mamlaka hayo kuanzia maandalizi yake, huyo ukizuia kujadili suala la urais na muungano.
Muswada huo juzi ulitawala kongamano la katiba lililoandalwia na wanataaluma wa chuo kikuu cha Dar es Salaam ambapo wachangia wengi walitoa wito kwa watanzania kuukataa kila njia.
Kifungu cha tano cha muswada huo, katika sehemu ya tatu, pamoja na masuala mengine kinazungumzia mamlaka ya Rais wa Muungano kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar, kuteua tume itakayoratibu mchakato wa utungwaji wa katiba mpya.
Kifungu cha 6 (1), kinazungumzia wajumbe wa tume hiyo ambao nao watateuliwa na rais, kwa kuzingatia uwiano sawa wa uwakilishi kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Pia katika uteuzi huo, rais atazingatia sifa zingine kama uzoefu na kiwango cha taaluma, umri, jinsia kwa makundi mbalimbali, mgawanyiko wa nchi nzima ya Tanzania, maslahi ya taifa na sifa zingine ambazo rais ataona zinafaa.
Kifungu cha 16 (1) katika sehemu hiyo ya tatu, kinasema kuwa baada ya tume kumaliza kukusanya maoni, itakabidhi ripoti yake kwa rais, ambaye atatoa nakala kwa Rais wa Zanzibar, kisha atamwelekeza waziri kuwasilisha muswada katika Bunge la Katiba.
Pia kifungu cha 21 katika sehemu ya tano ya muswada, kinazungumzia mamlaka ya rais kuunda Bunge la Katiba, kutangaza katika Gazeti la Serikali, baada ya 'kuligeuza; bunge la sasa kuwa bunge la katiba. Pia atakuwa na mamlaka ya kuteua majina ya wabunge watakaounda Bunge la Katiba.
Hoja zinazopinga vifungu hivi vinavyotoa mamlaka makubwa kwa rais kuanzisha, kusimamia hata kuamua mchakato wa katiba ni pamoja na kuwa rais mwenyewe kama kiongozi wa moja ya mihimili ya serikali, ni zao la katiba. Hivyo hawezi kutengeneza katiba kisha akawapatia wananchi waifuate.
Suala hilo la kuhamisha mamlaka kutoka kwa wananchi ambao ndiyo 'wenye' katiba na kuyaweka mikononi mwa mtu mmoja, wadau wengi, wakiwemo wataalam wa sheria wanasema kuwa, litasababisha katiba itakayopatikana kukosa uhalali.
Kwa mujibu wa wataalam wa sheria, katiba ya sasa haina mwafaka wa kisheria wala kisiasa kwa sababu taratibu za msingi, hasa katika kuwashirikisha watu katika mchakato mzima na namna ya kupata bunge la katiba, hazikufuatwa, kitu ambacho kinaonekana kutaka kujirudia tena sasa.
Mathalani, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika mada yake katika Kongamano la Maudhui ya Msingi ya Katiba Mpya, mwishoni mwa wiki, Chuo Kikuu Dar es Salaam, alisema kuwa utaratibu huo wa kumpatia rais mamlaka makubwa ni kupora mamlaka ya wananchi.
Imeelezwa kuwa kulifanya bunge la sasa kuwa bunge la katiba si sahihi, ndiyo mfumo uliotumika kwa katiba ya sasa, ambayo inalalamikiwa kwa ukosefu wa uhalali.
"Rais ni zao la katiba, rais hawezi kutengeneza katiba na kuwapa wananchi waifuate, hii itapelekea katiba hiyo kuwa na lack of legitimacy (kutokuwa halali) tatizo ambalo linadhihirika sana katika katiba ya sasa. Wananchi wameporwa mamlaka kwa kumfanya rais kama chombo cha utengenezaji katiba".
"Kazi ya kutengeneza katiba ni ya wananchi, katiba ni ya wananchi, kwa manufaa ya wananchi," anasema Bw. Kiwanga katika mada yake aliyoitoa kwenye kongamano juzi.
Sifa na muundo wa tume 'mungu mtu'
Kifungu cha 6(1) kinazungumzia wajumbe wa tume watakaoteuliwa na rais na namna muundo wake utakavyokuwa kama ilivyoelezwa hapo juu. Hiki kinaibua hoja ya uhuru wa tume hiyo, huku ikihojiwa kuwa kwa nini wajumbe hao wasiteuliwe na wananchi, kupitia kamati ya bunge ikishirikiana na rais.
Hadidu za rejea, ambazo tume itatumia kufanyia kazi ya kukusanya maoni, zimezungumziwa katika kifungu cha 8(1), ambapo imesemwa kuwa rais ndiye atatoa hadidu hizo kwa tume, kisha ataipatia muda wa kufanya kazi hiyo na kukabidhi ripoti.
Hili nalo linapingwa, huku wadau wakitaka hadidu za rejea ziwekwe bayana katika sheria ikayotungwa na bunge, kwani tume hiyo inapaswa kuwa ya wananchi si ya rais. Wanatolea mfano wa Tume ya Jaji Kisanga ya White Paper (1998) ambapo ilipewa hadidu za rejea na rais, baadaye 'akafoka' kuwa wamefanya nje ya majukumu aliyowaagiza.
Lakini pia kwa mujibu wa katiba ya sasa, rais hawajibiki kusikiliza ushauri wa mtu yeyote anapokuwa akitimiza majukumu yake, hivyo wadau wanasema kuwa kifungu hicho kinaweza kutumika kuweka kapuni baadhi ya maoni ya tume ya kukusanya maoni, kisha akapitisha yale tu, anayoona yeye yanafaa.
Kifungu cha 20 katika sehemu ya nne ambayo inazungumzia utaratibu wa tume ya kukusanya maoni, pamoja mambo mengine, kinasema kuwa tume hiyo haitashtakiwa katika mahakama yoyote ile, wala mahakama hazina nguvu ya kuhoji mamlaka ya tume, kitu kinachodaiwa 'kuifanya tume mungu mtu'.
Ni katika sehemu hiyo ambapo inaelezwa kuwa mtu yeyote atakayeonekana kupinga, kuingilia au kuzuia utendaji kazi wa mjumbe wa tume au sekretarieti (au vyombo hivyo), atakuwa amefanya kosa la jinai, ambalo adhabu yake ni faini ya sh. milioni 5 au kifungo kisichozidi miezi 12 gerezani.
Profesa Chriss Maina anaona hakuna umuhimu wa kufanya makosa kama hayo ya jinai, huku wengine wakisema imewekwa kwa nia ya kutaka kuwatisha watu, hasa wale watakaoonekana kutoa maoni kinzani na mwenendo wa tume.
Pia kinapingwa kuwa watendaji wa vijiji na kata ambao watatumika katika mchakato huo wa kukusanya maoni, kuwa wengi ni makada wa CCM, pia wamekuwa ni 'majaji' katika masuala mengi huko vijijini, hivyo kuna uwezekano wakatumia mwanya katika kifungu hiki kuwakamata wote watakaoonekana kutoa hoja kinzani.
Pia kifungu hiki kinazungumzia mikutano ya kijiji itakayoitishwa na watendaji wa vijiji, kutoka sehemu moja mpaka nyingine, kukutana, kujadili, kutoa maoni yao kwa tume kisha kuondoka, bila kuwa na mamlaka yoyote ya kuhakikisha walichojadili kinafanyiwa kazi.
Kifungu hiki kinaelezwa kuwa kimekwepa hatua ya muhimu ya kuwepo kwa Jumuiko la Kitaifa la Katiba, ambalo Dkt. Willibrod Slaa anasema kuwa ni mkutano rasmi wenye mamlaka ya kuyadili maoni hayo na rasimu ya katiba, kipengele kwa kipengele.
Bw. Kiwanga anasema kuwa Jumuiko la Kitaifa la Katiba lina uwakilishi mpana wa mikoa au kanda, jumuiya za dini, vyama vya siasa, vijana, wanawake, watoto na wenye mahitaji maalum, kuwa litajadili, kurekebisha na kupitisha pendekezo la katiba mpya.
Ushirikiswaji wa wananchi ni muhimu
"Kupitisha pendekezo la sheria kama mswada ulivyo hivi sasa tutaruhusu utaratibu unaonyang'anya mamlaka ya wananchi. Nia nzuri ya kutunga katiba ionekane kwa wenzetu wenye mamlaka na dhamana ya uongozi kwa kuweka taratibu nzuri.
"Tanzania ni yetu, hatma ya taifa hili iko mikononi mwetu, tuwajibike, tuache woga, tujadili, tufikie mwafaka wa kitaifa. Katiba mpya ni jibu. Jibu la kurudisha maadili ya taifa na kulinda rasilimali za taifa. Tuchukue hatua," anasema Bw. Kiwanga.
Suala la kura ya maoni
Sehemu ya sita ya muswada huo, kifungu cha 28, kinazungumzia upigaji wa kura ya maoni ya siri, kuikubali au kuikataa rasimu ya katiba mpya kwa kusema 'ndiyo' au 'hapana', huku kikizuia vyama vya siasa au asasi zingine za kiraia kupiga kampeni kuhamasisha wananchi.
Kifungu hicho kimefanya kosa hilo kuwa la jinai kwa mtu yeyote, chama cha siasa au asasi yoyote kufanya kampeni kuhamasisha wananchi kupiga kura hiyo, adhabu yake ni kifungo cha miaka miwili gerezani bila faini. Kazi hiyo itafanywa na tume ya uchaguzi pekee na si vinginevyo.
Hapa napo kumezua mjadala mkali, kwani vyama vya siasa na asasi ndizo zenye wafuasi wengi na ni haki yao kuhamasisha na kuwapatia elimu wananchi, hali ambayo, Profesa Issa Shivji anasema 'kura ya maoni bila kempeni ni hatari sana', kwani ni muhimu elimu ya uraia kutolewa wakati huo.
Vitu visivyohojiwa
Kifungu cha 9(2) katika sehemu ya tatu ya muswada kinapiga marufuku kuzungumzia masuala kadhaa wakati tume itakapokuwa ikifanya kazi yake, nayo ni; suala la muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mihimili ya serikali yaani dola, bunge na mahakama.
Mengine yasiyohojika ni; Serikali ya Mapiduzi ya Zanzibar, Umoja, mshikamano na amani ya Tanzania, mfumo wa uchaguzi unaotoa haki kwa wote, ukuzaji na ulinzi wa haki za binadamu, haki sawa mbele ya sheria, utu wa binadamu, serikali kutokuwa na dini na uhuru wa mahakama.
Hapa inashauriwa kuwa wakati wa mchakato wa utungwaji katiba si sahihi kupiga marufuku kuhoji baadhi ya mambo, bali wakati wa utungwaji wa katiba mambo hayo yanaweza kuwekwa, mathalani itapigwa marufuku kuhoji serikali kuwa na dini.
Pia marufuku hiyo izingatie historia ya taifa la Tanzania, kama vile suala la muungano, tunu za taifa, uhuru, umoja na maadili, Azimio la Taifa, Ripoti ya Jaji Kisanga, Misingi ya Haki za Binadamu na Demokrasia.
Katika mada yake, Bw. Kiwanga alimalizia kwa kusema "hatuhitaji kujenga watu au viongozi madhubuti, tunahitaji kujenga mifumo madhubutini itakayodumu na kulinda maslahi ya taifa na kulinda rasilimali za taifa kwa faida ya vizazi vya sasa na miaka mingi ijayo".
tumechoka na hila za ccm
ReplyDeleteZanzibar iwe na wajumbe 2 tu, hakuna mantiki ya wao kushiriki kuandaa katiba ya bara, wakati wanaandaa ya kwao hakuna wa bara aliyeshiriki,haiwezekani kutupangia jinsi gani mambo ambayo si ya muungano tunataka yawe. Wao waingie pale panapohusika tu yaani kwenye maswala ya muungano tu.
ReplyDeleteNa swala hili halitakiwi libebwe kwa rangi ya kijani- CCM. Katiba ni mali ya wananchi,washilikishwe kwa kila hatua,kumuachia mwenyekiti wa ccm bara na wa Zanzibar ni uharamia,ulaghai na hasa ulavi wa kutaka wabakie madarakani hata kama si kwa ridhaa ya wananchi.
Ndugu zangu watanzania inasikitisha kuona muswada huu utapita kwa nguvu zote kwa vile wabunge wa CCM ndio wengi na watapigana patashika nguo kuchanika hadi upite. Nasikitika sana ninaona mbele ya Tanzania kuna giza nene la umwagaji damu za wananchi wasio na hatia kisha ni serikali ya kikwete kuwapa akina werema madaraka ya kuharibu uundwaji wa Katiba mpya ya Tanzania. Muswada huu ni mufilisi kabisa hauna tija. Nawasihi wabunge wa upinzani wote hata wale vibaraka kuukataa kwa nguvu zote. Pamoja na kuwa ni wachache mimi nawapa moyo ukataeni na serikali itakapolazimisha tupo tayari kuingia mitaani kudai katiba mpya kwa gharama yoyote. Haiwezekani tume iundwe na Rais ambaye anatoka chama cha siasa, haiwezekani mambo ya msingi kama masuala ya tume ya uchaguzi ambayo ndiyo msingi mbovu wa uchaguzi usio huru wa kuiba kura yasizungumziwe kwenye katiba mpya. Huu ni uhuni muswada huu urekebishwe kwanza, wananchi twendeni dodoma kwa migu ili hawa wabunge wapumbavu wa CCM wakipitisha tuanze maandamano pale. Hatupo tayari kuchezewa na akina Werema wajinga wachache wa Kikwete. Hapa kinachotakiwa ni mkutano wa katiba ambao kila mwannchi atashiriki, msomi, mwenye busara, mjanja, mbumbumbu hata kichaa ashiriki kwa maslahi ya nchi yake. hatutaki kuandikiwa Katiba na Rais. Nawaasa hawa wabunge mataahira wa CCM wasipitishe Muswada huu wakubali ushauri wa wanaharakati na wabunge wa upinzani ili kuwepo utaratibu mzuri kuuandika katiba mpya ya wananchi na siyo ya Rais Kikwete na Jaji Werema au serikali yao hapa mtaleta maafa ambayo mtayajutia vizazi na vizazi maana hakuna cha polisi au mwanajeshi atakayekubali ujinga huu. Kama watakubaliana tupo tayari kufa. MUNGU ISAIDIE TANZANIA NAONA SASA SERIKALI YA CCM INALETA MAAFA YA LIBYA, MISRI NA TUNISIA. TUTAPELEKA WAPI WATOTO NA HAWA WAGONJWA WENGI NAMNA HII WANAOENDA LOLIONDO?
ReplyDelete