04 April 2011

Kigogo NCCR amwagiwa tindikali

Na Rehema Maigala

MKURUGENZI wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi katika Chama cha NCCR-Mageuzi, Bw. Faustin Sungura amemwagiwa majimaji yanayodhaniwa ni
tindikali na watu wasiojulikana na sababisha kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Tukio hilo lilimkuta juzi saa 2 usiku maeneo ya Ilala Sharifu shamba, alipokuwa anatoka katika shughuli zake akirudi nyumbani.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, Bw. Samweli Ruhuza ambaye aliyekuwa hospitalini hapo alisema kuwa, walipigiwa simu na wananchi kuwa mwananchama wao amemwagiwa tindikali maeneo ya Ilala Sharifu Shamba.

"Kweli tulifika eneo la tukio tukakuta wananchi wanampa huduma ya kwanza Bw. Sungura kwa kumuosha macho yake kwa maji na maziwa, ili kuondoa sumu aliyomwagiwa katika macho yake.

Tulivyomuuliza nini kilichompata alisema kuwa lilimpita gari karibu na miguu yake na alijaribu kulikwepa, baadaye alimuona mtu anateremka ndani ya gari lile huku akiwa na chombo ambacho ndani yake kulikuwa na kitu na kumwagia usoni na kusababisha muda ule ule macho yasione na kusikia maumivu makali," alisema Bw. Ruhuza.

Alisema kuwa baada ya tukio hilo gari hilo liliondoka kwa mwendo wa kasi hali iliyosababisha wananchi kutochukua namba za gari hilo.

Baada ya hapo tulimchukua na kumpeleka katika Hospitali ya Amana kwa ajili ya matibabu.

Aliongeza kuwa Amana walimchoma sindano kwa ajili ya kuua sumu na kumhamisha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikolazwa sasa.

No comments:

Post a Comment