Na Rashid Mkwinda, Mbozi
WAFUGAJI wa nguruwe katika mji mdogo wa Mlowo wameanza kutupa mizoga ya wanyama hao waliokufa kwa homa ya nguruwe kando kando ya
mto Mlowo.
Mwandishi wa gazeti hili alishuhudia mizoga hiyo ikiwa imetupwa kando ya mti huo karibu na daraja la kuelekea Misheni huku mbwa na inzi wakijipatia mlo kutokana na mizoga hiyo iliyotuama katika mto huo.
Harufu kali iliyozagaa katika eneo hilo imesababisha baadhi ya watu wanaopita katika mto huo kufunika pua zao na kuwalaumu watendaji wa mji wa Mlowo kwa kutowajibika juu ya afya za wananchi.
Mmoja wa wakazi wa maeneo hayo aliyejitambulisha kwa jina la Kalasha Mwazembe alisema kuwa utaratibu uliofanywa na baadhi ya wafugaji wa kutupa mizoga mtoni ni kitendo cha hatari ambacho kinaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa wakazi wanaoishi kando ya mto huo.
Naye Bi. Grace Namgala mkazi wa mtaa wa Misheni alisema kuwa wao wanategemea maji ya mto huo kwa matumizi ya nyumbani ikiwemo kufulia nguo na kuoshea vyombo ambapo pia kutokana na uhaba wa maji katika mji hu,o baadhi yao hutumia maji ya mto huo kwa ajili ya kunywa.
"Pembezoni mwa mto huo kuna chemichemi ya maji ambayo tunakunywa…maji hayo kwa sasa yanatoa harufu ya mizoga, watoto wameanza kuugua homa za matumbo," alisema Bi. Namgala.
Alisema kuwa nguruwe wameanza kufa hivi karibuni katika maeneo ya mji mdogo wa Mlowo ambapo wamekuwa wakiugua muda mfupi na kufa na kwamba wafugaji hao wameamua kutupa mizoga ya nguruwe mtoni, jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji wa maji ya mto huo.
Naye Bw. Masomo Shitindi mkazi wa maeneo hayo alisema kuwa kuzagaa kwa mizoga ya nguruwe katika mto huo kumesababisha kuibuka kwa tatizo la maji ambapo wananchi waliokuwa wakiyategemea wamelazimika kuyafuata umbali mrefu.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mlowo, Bw. Jackson Mwanda alisema kuwa hana taarifa za kuzagaa kwa mizoga hiyo isipokuwa alipewa maagizo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi kuwataka wakazi wa mji huo kuacha kuchoma nyama ya nguruwe.
"DC aliniandikia barua kuwaeleza wakazi wa Mlowo na vitongoji vyake kuacha kuchinja wala kuchoma ‘Kiti Moto’..kuacha kununua mazao ya chakula ya Kitimoto kutoka wilaya za nje..tuliwatangazia wananchi wote," alisema.
Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Mbozi, Bw. Thabit Lukalisha alisema kuwa, ugonjwa wa homa ya Nguruwe umeingia wilayani humo na kuzagaa katika maeneo ya Tunduma na Mlowo na kwamba Aprili 11, mwaka huu alipata taarifa za vifo vya nguruwe 231.
Bw. Lukalisha alisema kuwa hata hivyo Halmasahauri ya Wilaya imefanya jitihada za kuhakikisha ugonjwa huo hauenei kwa kutoa elimu ili wananchi wasikiuke taratibu za karantini kwa kutopokea mazao ya nguruwe ikiwa ni pamoja na nguruwe waliopo kuwazuia kutozagaa ovyo.
Tatizo maofisa kata wanangoja kuamrishwa toka wilayani halafu wanakaa hawawajibiki mpk ije amri ingine, hivi kweli ktk Tarafa yako huna taarifa za hali mbaya ya kuzagaa mizoga namna hiyo hivi hata huo uchomaji wa hicho kitimoto wanafatiliaje au wamekaa maofisini kusubiri amri?Maana unapofatilia kama amri imetekelezwa na hapo utaona madudu mengine na si ajabu hata leo akifwatwa tena akiulizwa atajibu hajafika huko kamuagiza mtendaji wa kijiji amletee taarifa.Ni uzembe mpk watu wapuputike
ReplyDelete