Na Gladness Mboma
KESI inayowakabili mawaziri wa awamu ya tatu, Bw. Basil Mramba, Bw. Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw, Gray Mgonja, imeahirishwa
hadi Mei 6, mwaka huu kutokana na mwenendo wa kesi kutokamilika.
Wakili wa Utetezi Elisa Msuya alitaka kujua kama mwenendo wa kesi ya wateja wake kama huko tayari ili waupitie kabla hawajaanza kujitetea.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Bw. Ilvin Mgeta alisema kuwa bado mwenendo wa kesi haujaandaliwa ili mahakimu wa pande zote mbili waweze kujiandaa kwa hoja ya 'kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la'.
Hakimu Mgeta alisema kuwa kwa taarifa alizonazo bado mwenendo wa kesi haujaandaliwa na kwamba baada ya siku 14 utakuwa tayari.
Pamoja na kuahirishwa kwa kesi hiyo, Wakili Msuya alimuomba Hakimu Mgeta kutoa kibali cha wateja wake waweze kusafiri mikoani.
Kwa mujibu wa kesi hiyo, Januari 20, mwaka huu, Wakili wa Serikali Mkuu, Boniface Stanslaus, alifunga ushahidi wao dhidi ya kesi hiyo kwa madai kuwa, wameridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wao 13.
Mramba na wenzake wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya na kusababishia serikali hasara ya sh. bilioni 11.7 kupitia msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stwart ya Uingereza.
No comments:
Post a Comment