13 April 2011

Mbaroni kwa kuua mke mwenzake

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia mwanamke mmoja mkazi wa kijiji cha Mwakibuga wilayani Bariadi anayetuhumiwa kumuua mke mwenzake kutokana na wivu wa
kimapenzi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Diwani Athumani alimtaja mwanamke
huyo kuwa ni Bi. Pili Magese (23) ambaye anatuhumiwa kumuua mke mwenzake kwa
kumkatakata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kufa.

Kamanda Athumani alimtaja mwanamke aliyeuawa kuwa ni Bi. Pili Makoye (20) mkazi
wa kijiji cha Mwakibuga wilayani Bariadi ambaye alikuwa ni mke mdogo na kwamba
tukio hilo lilitokea Aprili 9, mwaka huu saa 2.00 usiku.

Alisema siku hiyo ya tukio Bi. Magese alimvamia mke mwenzake alipokuwa jikoni
akiandaa chakula cha usiku ambapo ghafla alimshambulia kwa kumkatakata panga
sehemu za kichwani, shingoni na sehemu mbalimbali za mwili wake hali
iliyosababisha atokwe na damu nyingi na kufariki dunia.

Inadaiwa kuwa chanzo cha mauaji kinatokana na wivu wa kimapenzi kati ya wanawake
hao na kwamba baada ya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo mtuhumiwa atafikishwa
mahakamani kujibu shitaka la mauaji.

Katika tukio jingine mfanyakazi wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu wilayani
Kahama unaomilikiwa na Africa Barrick Gold Mine  (ABGM), Bw. Mlumbi Aron (27)
amekufa baada ya kupondwa na mwamba wakati akiendelea na kazi ya uchimbaji wa
madini ardhini.

Alisema mfanyakazi huyo alipatwa na majeraha sehemu za kichwani na kuvunjika
mguu wa kulia ambapo kutokana na maumivu hayo alifariki dunia japo watumishi
wengine aliokuwa akifanya nao kazi hawakupatwa na majeraha yoyote.

Tukio hilo lilitokea Aprili 9, mwaka huu saa 9.30 usiku na inadaiwa kuwa chanzo
cha kubomoka kwa mwamba huo kinatokana na mtikisiko uliosababishwa na tetemeko
la ardhi lililopita wakati huo.

No comments:

Post a Comment