Na Jumbe Ismailly, Singida
SERIKALI imesimamisha mara moja shughuli za Mfuko wa Maafa wa Idara ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwa muda usiofahamika kutokana na upungufu
kadhaa uliyojitokeza, ikiwemo kutokuwa na katiba ya mfuko huo.
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bw. Kassimu Majaliwa alitoa agizo hilo juzi wakati akizungumza kwenye majumuisho ya ziara yake Mkoani Singida.
Bw. Majaliwa alisema amelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kubaini kwamba mfuko huo unaendeshwa kienyeji na bila kuwa na ridhaa ya wananchama wake ambao ni walimu wa halmashauri hiyo.
Akifafanua Bw. Majaliwa alisema pamoja na Chama cha Mfuko huo kutokuwa na katiba, hata hivyo taarifa za mapato na matumizi ya mfuko huo zimekuwa hazitolewi kwa wakati.
Alisema kuwa mfuko huo umegeuzwa kuwa ni Chama cha Kuweka na Kukopa, kitendo ambacho hakifanani na malengo ya kuanzishwa kwa mfuko huo.
"Mfuko huu ambao madhumuni yake ni mazuri sana,malengo yake yamegeuzwa na viongozi wake wachache kwa kitendo chao cha kuikopesha Ofisi ya Ofisa Elimu wa Halmashauri hiyo zaidi ya shilingi milioni sita, na walimu wanne wao nao wamekopeshwa zaidi ya shilingi laki tisa "alisema Bw. Majaliwa.
Alisema viongozi wachache wa mfuko huo wamepandisha ada ya mfuko huo kinyemela kutoka sh. 500 hadi sh. 3,000 bila kushirikisha wanachama wa mfuko.
Hata hivyo Bw. Majaliwa akionesha wazi kutokufurahishwa kabisa na uendeshaji wa mfuko huo hakusita kuhoji mlezi wa mfuko huo na ni kwa nini matumizi yake yamebadilishwa na kuanza kukopesha badala ya kusaidia walimu wanaopata bahati mbaya ya kufiwa.
“Hivi ni nani mlezi wa mfuko huu na ni kwa nini matumizi ya mfuko huu yamebadilishwa na kuanza kukopesha badala ya kusaidia walimu wanaopata bahati mbaya ya kufiwa? alihoji Bw. Majaliwa .
Kutokana na swali hilo la aliposimama afisa wa TSD katika ofisi ya afisa elimu katika Halmashauri hiyo, aliyetambulika kwa jina moja la Mwalimu Nkindwa ambaye kwa mujibu wa maelezo yake kwanza alikiri kuwa yeye ndiye mlezi wa mfuko huo.
“Mimi ndiye mlezi wa mfuko huu mheshimiwa naibu waziri,hatujabadilisha malengo ya mfuko isipokuwa ilitokea dharura iliyotulazimu tuazimishe fedha hizo," alisema.
Baada ya jibu hilo Bw. Majaliwa alihoji tena sababu za ada ya shilingi 600,000 za mfuko huo za kipindi cha Januari mwaka huu na shilingi milioni tano za Februari, hadi sasa hazijapelekwa benki.
“Ningependa kufahamu sababu za kutopelekwa fedha benki zilizokusanywa mwezi Januari shilingi 600,000/= na shilingi milioni tano za mwezi Februari?
Hata hivyo alilazimika kusimama tena na kutoa majibu kwamba mchakato wa kuzipeleka benki fedha hizo unaendelea vizuri na wakati wowote zitapelekwa benki.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi Illuminata Mwenda alipoulizwa kama anaufahamu mfuko huo,alidai kwa kiasi fulani anausikia lakini atamwagiza mkaguzi wa ndani kuukagua na kutoa taarifa haraka iwezekanavyo.
No comments:
Post a Comment