Na Mwandishi Wetu
MAMBO ndani ya Chama cha Maendeleo Muheza (MDTF) yamezidi kuharibika baada ya sekretarieti inayoongozwa na Bw. Tido Mhando kupinduliwa rasmi na genge
linalojiita wanachama wakareketwa.
Kupinduliwa kwa sekretarieti hiyo kumekuja takriban mwezi mmoja baada ya wanachama hao chini ya uongozi wa Bw. Halid Kibwana, kutoa kitisho cha kufanya mapinduzi hayo.
Waraka wa maandishi uliosambazwa kwa baadhi ya wakazi wa Muheza waishio jijini Dar es Salaam umesema kuwa uamuzi huo unalenga kukinusuru chama ambacho kinaelekea kufa tangu kuingia sekretarieti hiyo mnamo mwaka juzi.
“Tumeamua kuing’oa sekretarieti ya MDTF kutokana na kushindwa kazi. Tangu iingie madarakani mwaka juzi, chama hakina ofisi, hakina hata shilingi kwenye akaunti, shughuli za utawala zimesimama na mipango yote ya maendeleo ikiwemo kuanzisha SACCOS Muheza imekufa.
“Alipoondoka Balozi Adadi Rajabu, aliacha chama kikiwa hai, alijenga shule ya kidato cha sita, visima vya maji na sekondari, lakini sekretarieti hii ya sasa ni mzigo. Kwa hiyo, tumeamua kwa maslahi ya Muheza, kuindoa madarakani. Wakazi wote wa Muheza mnaaombwa kuunga mkono mapinduzi hayo matufuku.”
MDTF inaundwa na sekretarieti inayoongozwa na Mwenyekiti Bw. Tido, Makamu Mwenyekiti, Bi. Marry Chipangahelo, Katibu Bw. Albert Semng’indu ambaye ni Mkurugenzi CHC, Mweka Hazina Nehemia Mchechu, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba (NHC) na Bw. Ramadhan Semtawa, Katibu Mwenezi huku Mkurugenzi Mtendaji akiwa ni Clement Mang’enya.
Alipoulizwa jijini Dar es Salaam jana kwa njia ya simu, msemaji wa MDTF, Bw. Semtawa, alikiri kupata waraka huo na kuongeza kwamba, bado anawasiliana na wenzake kuona namna ya kufanya.
Bw. Semtawa ambaye pia ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi, alisema inawezekana wanachama wakawa na hoja za msingi lakini tatizo likawa njia wanayotumia kutaka kuung’oa uongozi kupingana na katiba.
“Nikiwa kiongozi mkweli, nakiri sekretarieti yetu ina upungufu mkubwa. Ni kweli hakuna mradi hata mmoja ambao tumefanya tangu tukabidhiwe madaraka na wenzetu lakini, hata kama ni hivyo zipo njia za kikatiba kuondoa uongozi madarakani,” alisema Bw Semtawa.
Hata hivyo, aliweka bayana kwamba, tayari karibu wajumbe wote wa sekretarieti walionyesha dhamira ya kutotaka kuendelea na nafasi zao tangu wanachama hao walipotangaza mpango huo wa mapinduzi hapo Februari.
“Wiki moja iliyopita mwenyekiti aliitisha kikao cha kamati tendaji, lakini wajumbe karibu wote (isipokuwa yeye Tido tu), hatukwenda na tulisema tunachojua tayari tumepinduliwa tangu Februari, hivyo tumeachia taratibu nyingine za kupata sekretarieti mpya,” alisema Bw. Semtawa.
MDTF ni chama ambacho kimeanzishwa kwa dhamira ya kusaidia juhudi za serikali kuleta maendeleo kwa wananchi wa Muheza, chama hicho kilipata mafanikio makubwa wakati sekretarieti ikiongozwa na Balozi Adadi.
Bwana Semtawa cha msingi ww jiuzlu wapishe vijana wafanye kazi yake
ReplyDeleteHiyo ndiyo maana ya serikali ya Majimbo ambayo Chadema inaipigia kelele. Waache wenye eneo wasimamie maendeleo yao na siyo kila kitu kifanywe toka central government. Pia wanainchi wanapokuwa wamechagua viongozi wao wa jimbo, pia wanauwezo wa kuuondoa. Siyo Mkuu wa mkoa ni mteuliwa wa Raisi ambaye hana maslahi ya mkoa husika.
ReplyDeleteNguvu ya Demokrasia hiyo.