17 March 2011

Waziri amwaga milioni 60/- kufadhili sherehe za dini

*Yadaiwa lengo ni kujitakasa kwa kanisa urais 2015
*Waumini watofautina, wasema angetoa Gongolamboto
*Baraza Kuu UVCCM kuwasha moto, viongozi wakamiana
 

Na Mwandishi Wetu

VIBWEKA vya wanaCCM wanaotajwa kugombea urais kupitia chama hicho mwaka
2015 vimeanza kwa kasi huku mmoja wa mawaziri akitajwa kumwaga mamilioni ya fedha kufadhili sherehe moja ya kidini.

Chanzo cha kuaminika kimelidokeza gazeti hili kuwa miongoni mwa mikakati inayofanywa na makada hao sasa ni kuangalia namna wanavyoweza kuteka ngome za kidini kwa lengo la kuungwa mkono kwenye uchaguzi huo.

Mbali na hilo wanasiasa hao wanajaribu kujipanga kwa kutumia makundi mengine muhimu ndani ya jamii kwa lengo la kuhakikisha wanafanikisha mkakati huo ambao unaonekana kuwa ushindani mkali kutokana na kipindi cha rais wa sasa Jakaya Kikwete kumalizika kwa mujibu wa katiba.

Chanzo chetu kimedokeza kwamba moja ya maeneo yanayotupiwa macho na wagombea hao katika kuhakikisha wanafanikisha mkakati wao ni kufanya kila linalowezekana ili wakubalike na dini kuu mbili zenye mtandao mkubwa nchini, yaani Waislamu na Wakristo.

Ili kufanikisha hilo wagombea hao wanadaiwa kujaribu kufanya kila linalowezekana kugusa hisia chanya za dini hizo kwa imani kwamba wanaweza kulamba tufuru kwenye kinyang'anganyiri hicho.

Katika kile kinachoonesha kuthibitisha mkakati huo, mmoja wa wagombea wanaotajwa kuwania nafasi hiyo mwaka 2015 anadaiwa kuchangia jumla ya sh. milioni 60 kufanikisha shughuli moja ya kidini inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii.

"Tumeshangaa, ni kawaida Wakatoliki tunapokuwa na sherehe mbalimbali tunatoa kadi kwa waumini wetu na watu wengine kuchangia. Michango hii ni ya kawaida kwa kadri mtu alivyojaliwa, hatulaumu lakini inatia wasiwasi kigogo mmoja anatoa sh. milioni 60 kuchangia sherehe za kuwekwa wakfu Askofu wa Jimbo la Dodoma," kilisema chanzo chetu na kuongeza;

"Michango ya namna hii inapoteza maana yake hata kama mtoaji alikuwa na nia njema. Si makosa watu wakisema huku ni kujaribu kujipendekeza kwa kanisa ili kuungwa mkono kwa madhumuni fulani. Milioni 60 ni fedha nyingi sana kutoa kama mchango tu kwa sherehe za namna hii, kwanini mtu huyu asitoe fedha hizo kwa waathirika wa mabomu Gongolamboto?"

Taarifa kutoka ndani ya kanisa hilo zilisema kuwa kigogo huyo alitoa fedha hizo kwa awamu mbili, kwanza alitoa milioni 45 na baadaye alimalizia sh. milioni 15, jambo ambalo limezua maswali mengi kwa baadhi ya waumini wa kanisa hilo.

"Inawezekanaje mtu mmoja kuchangia fedha zote hizi kwa shughuli hii? Inawezekana hapa pana ajenda ya kisiasa nyuma yake, ni mbinu za 'kuvalisha kanisa miwani' ili aonekane." 

Majira lilipojaribu kuwasiliana na viongozi wa kanisa hilo kupata ufafanuzi wa suala hilo, simu zao hazikupatika hewani na zingine ziliita pasi kupokelewa.

Hata hivyo mmoja wa wajumbe wa kamati ya maandalizi ya sherehe hizo aliyeomba kutotajwa jina gazetini kwa kuwa si msemaji wa kanisa hilo alithibitisha kupokewa kwa fedha hizo na kukataa kuzungumzia zaidi suala hilo.

Mwanakamati mwingine alidai kuwa mchango huo 'wakutisha' kwa sherehe za kawaida kama hizo, unaweza kuligawa kanisa hilo kwa kuonekana linageuzwa kuwa jukwaa la baadhi ya watu kutafuta njia za kukidhi matakwa yao kisiasa.

Wakati huo huo hali si shwari ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM kwa kile kinachodaiwa kuwepo taarifa za zengwe la kuwang'oa baadhi ya viongozi wake kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja huo unaoatarajiwa kufanyika Jumamosi mjini Dodoma.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba baadhi ya wanasiasa wamejipenyeza ndani ya umoja huo kwa kuwatumia baadhi ya wajumbe kuhakikisha wanawang'oa viongozi wanaoonekana vikwazo katika kukidhi malengo yao.

"Tupo macho, ingawa kuna taarifa kwamba baadhi ya watu wana mpango wa kuvuruga UVCCM kwa kuhakikisha viongozi ambao wamekuwa kikwazo katika kutekeleza malengo yao wanawekwa kando," alidokeza mmoja wa wajumbe wa baraza hilo.

10 comments:

  1. DDUUHH, HII KALI KULIKO INABIDI PCCB WAMMULIKE HARAKA MAANA KWANZA KAZIPATAJE ACHUNGUZWE AU NDIO MGAO ALIOUPATA WA KUFUNGA BUNGE?NA IANGALIWE HISTORIA YAKE ALIWAHI KUTOA MICHANGO KAMA HIYO KABLA? HUYU NI FISADI!!

    ReplyDelete
  2. hii habari inaukweli wowote au ndiyo kuuza gazeti? hakuna hata jina moja la mhusika? hivi kama kweli ushahidi upo kwa nini msiwataje hao wahusika,yaani huyo waziri na hao waliopokea hizo pesa? tumechoka na habari za namna hii.au na nyie waandishi unawaficha mafisadi ambao wapo katika upande wenu? ingekuwa habari hii inamuhusu Rostam mngeandika majina na kuwa hoji watu kibao.

    ReplyDelete
  3. Tunaweza kujadili kwa namna moja ama nyingine
    1. Jamii ya kitanzania inahitaji msaada mkubwa kiuchumi na kijamii.
    2. Jamii ya kitanzania inahitaji msaada mkubwa kielimu.
    3. Jamii ya kitanzania itambue kuwa msaada una gharama yake, leo umepokea kesho utalipa mara mia mbili au zaidi.
    4. Jamii ya kitanzania itambue kuwa hii adha tunayopata sasa ya kupanda kwa gharama ya maisha inatokana hii misaada ya kijinga inayotolewa na viongozi wa serikali ya ccm.
    5. Nawaomba ndg zangu wa tanzania tuukatae utumwa huu.
    6. Kiongozi bora wa watanzania ni yule anayesimamishwa na wananchi wenyewe, sio mtu anajitokeza anaanza kujikombakomba mara akupe hiki mara kile.

    Watanzania tuamke zama za ujima zimepitwa na wakati.

    ReplyDelete
  4. Habari hii ni upuuuuuuuuuuuzi mtupu na uzandiki,mtajeni huyo waziri,mbona huwa hamwogopi kumtaja Lowassa,Rostam na hata Rais Kikwete!!!

    ReplyDelete
  5. Msitake kuwalisha Watanzania ujinga kwa habari zisizo na chanzo chochote cha kuaminika.Hata kama 'udaku'wenu ni kweli basi mmeongeza magadi badala ya chumvi.

    ReplyDelete
  6. huyo atakuwa lowasa tu maana kila kukicha anabinu mbinu za kumuingiza ikulu lakini ajue kuwa watanzania wapo macho kwa sasa wanajua kila fisadi na kama bado anataka kuwania urais basi ccm wajue ndio wanaangukia pua.ikumbukwe kuwa hata kikwete safari hii ameponea chupu chupu angalia asilimia alizopata wakati wa uchaguzi mkuu uliopita

    ReplyDelete
  7. NI KWELI HUO NI UNAFIKI WEKENI JANA WAZI ILI TUELEWE SIO TENA KUANZA KUUMIZA VICHWA KUMTAFUTA HUYO MTU,KAMA MNASHINDWA KAZI ACHENI ILA ACHENI KUANDIKA UNAFIKI

    ReplyDelete
  8. hii ni habari ya uchunguzi; mwandishi wa habari hajaficha chochote wala hastahili kulaumiwa; amewahabariha wananchi nini kilichopo nchini kwa wakat huu, huku akiwataka muendelee kujadili na kuibana serikali katika masuala nyeti kama hili. mmepewa mwanya wa kuhoji mhusika huyo ni nani,ambaye kwa macho yako hajifichi anajulikana; pia kanisa lililofadhiriwa mamilioni hayo na uongozi wake upo, mnaweza kuwabana. mwandishi ametoa yowe ili wananchi mmsaidie ktk kelele yake; si kumuweka yeye kikaangoni.

    ReplyDelete
  9. kama habari hii ni kweli kwa nini mnaogopa kumtaja huyo mtaka URAHISI

    ReplyDelete
  10. Ni ujinga wenu siasa biashara sasa hivi mnashangaa ya ccm,chadema si imepata vingi vingi safari hii ukicchanganya na viti maalum sasa angalieni vioja vya wanasiasa 2015

    ReplyDelete