17 March 2011

Waliochaguliwa kidato cha tano watangazwa

Na Gladness Mboma

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetangaza majina ya wanafaunzi 36,366 waliochaguliwa kuingia kidato cha tano katika shule 204 na vyuo
vinne vya ufundi vya serikali mwaka huu.

Miongoni mwa wanafunzi hao wamo wasichana 11,210 na wavulana 25,156.

Mwaka huu idadi ya wanafunzi wa kike waliopangwa katika masomo ya sayansi na vyuo vya ufundi imeongezeka kwa asilimia 4.7, na kwa wavulana ni 12.7 sawa na asilimia 25.9 ukilinganisha na mwaka jana.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa alisema jana Dar es Salaam, kuwa wanafunzi 916 kati yao wakiwemo wasichana 55 na wavulana 861 wamepangwa katika vyuo vya ufundi vya Mbeya (MIST) ,Dar es Salaam (DIT), Arusha (ATC) na Chuo cha Maji Dar es Salaam.

Mwaka jana wanafunzi waliopangwa kidato cha tano katika shule na vyuo vya ufundi vya serikali walikuwa 33,662, wasichana wakiwa 12,638 na wavulana 21,024 ambapo wanafunzi 897, wasichana wakiwa 16 na wavulana 881 walipangwa katika vyuo vya ufundi.

"Mwaka huu idadi iliyoongezeka kwa kidato cha tano ni 2,704 sawa na asilimia 8.03, idadi ya waliopangwa vyuo vya ufundi imeongezeka kidogo kwa wanafunzi 19 sawa na asilimia 2.12," alisema.

Alisema kuwa ili mwanafunzi aweze kuchaguliwa kuingia kidato cha tano katika shule za serikali anapaswa kuwa na umri usiozidi miaka 25 wakati akifanya mtihani huo wa kidato cha nne na ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu, awe na pointi saba hadi 25 katika mitihani ya kidato cha nne mwaka 2010.

Dkt. Kawambwa alisema kuwa mwanafunzi anapaswa awe na ufaulu wa gredi A au B au C zisizopungua tatu na ufaulu A au B au C au D zisizopungua tano, ambapo wanafunzi wanaochaguliwa kwenye fani ya ufundi wanatakiwa wafaulu masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati.

Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu wanafunzi 37,774 wa Tanzania Bara walikuwa na ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu na kwamba hata hivyo baadhi ya wanafunzi hawakuwa na sifa zote zilizotajwa kustahili kupangwa kidato cha tano. Orodha ya wanafunzi hao imechapishwa ukurasa wa tano, 19 na 20 ndani ya gazeti hili.

No comments:

Post a Comment