27 March 2011

Watu 16 wafariki kwa ajali Kibaha

*Wengine 19 wajeruhiwa, walazwa
*Waliokufa waanza kutambuliwa


Na Masau Bwire, Pwani

WATU 16 wamekufa na wengine 19 kujeruhiwa vibaya katika ajali  mbili tofauti zilizotokea juzi usiku katika vijiji tofauti wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.Ajali ya
kwanza ilitokea saa 4 usiku wa juzi katika kijiji cha Mbala na kusababisha vifo vya watu 13 na majeruhi 13.

Katika ajali hiyo kati ya watu 13 waliokufa wanaume ni 11, mwanamke mmoja na mtoto wa kike mmoja. Miili ya waliokufa imehifadhiwa  Hospitali Teule ya Tumbi.

Watu wawili kati ya waliotambuliwa  ni Bw.Ediraid Selestine (40) mkazi wa matombo Morogoro na mwingine ametambuliwa kwa jina moja la Mohamed mkazi wa Bagamoyo.

Ajali ya pili ilitokea saa 6 usiku huo huo katika kijiji cha Ubena  Zomozi na kusababisha vifo vya watu watatu na majeruhi sita. 

Katika ajali hiyo watu wote watatu waliokufa walitambuliwa kuwa ni Bw. Robert Lehena, ambaye ni utingo wa lori linalodaiwa kusababisha ajali, Bw. Miraji  Mwinyi (22), mkazi wa Ngusero, Kiteto na mwingine ametambuliwa kwa jina moja la Joseph, ambaye ni fundi wa magari mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam.

Ofisa Uhusiano Hospitali ya Tumbi, Bw. Gerald Chami aliwataja majeruhi wa ajali ya kwanza kuwa ni Bw. Juma Omary (29) mkazi wa Morogoro, Bw.Godwin Sakalani (55) mkazi wa Kilombero na mtu mwingine ambaye jina lake halikutambuliwa ambao wote wamehamishiwa Hospita ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Wengine ambao wote wamelazwa hospitali ya Tumbi ni Bw. Edwin Mbele (49) mkazi wa Kilombero, Bw. Madaraka Rashid (42) mkazi wa Bunju, Bw, Fredinand Paul (45)mkazi wa Vingunguti Dar es Salaam, Bi. Esther Shija(38), mkazi wa Mbagala na Bw. Nkundunge Mganga (29)mkazi wa Dumila.

Bw. Chami aliwataja majeruhi wengine kuwa ni Bw. Haruna Ngungaruma (24)mkazi wa Kiwalani, Bw. Khalid Hamza(29) mkazi wa Morogoro, Bw.Lawrence Mkunde (30)mkazi wa Mabibo, Bw. Judai Kisiwa (33)mkazi wa Kinondonina Bw. Justine Clemence (34) mkazi wa Mabibo,.

Akieleza tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, Bw.Absalon Mwakyoma alisema ajali ya kwanza ilihusisha gari aina ya Coaster namba T T561 AZP  iliyokuwa ikitoka Morogoro kwenda Dar es Salaam ikiwa na abiria, Mistubish Canter namba T 110 BEZ iliyokuwa imeegeshwa barabarani wakati ikitengenezwa, lori lenye namba T535AAG  likiwa na tela namb T 410 ARB  lililokuwa na shehena ya mbao likisafiri kwenda Dar es Salaamna Fuso namba  T368 ATBV lililokuwa limebeba bidhaa za dukani likisafiri kutoka Dar es Salam kuelekea Morogoro.

MKamanda Mwakyoma alisema wakati Coaster na lori lenye mbao yakisafiri kuelekea Dar es Salaam, lori likiwa limetangulia, lilipunguza mwendo na kusimama nyuma ya Canter iliyokuwa imeegeshwa barabarani kupisha Fuso iliyokuwa ikiendeshwa kwa mwendo wa kasi kutokea Dar es Salaam kuelekea Morogoro.

Alisema wakati lori hilo limesimama Coaster ilikuwa kwenye mwendo mkali ikitaka kupita magari hayo, ghafla mbele yake kukawa na Fuso likiwa kwenye mwendo wa kasi na kulazimisha Coaster kurudi kushoto, ndipo likaingonga kwa nyuma lori lenye mbao na Fuso pia kuigomga Coaster hiyo na kuanguka upande wa kulia mwa barabara, ambapo watu 13 abiria wa Coaster hiyo walikufa papo hapo na wengine 13 kujeruhiwa.

Kamanda Mwakyoma alisema pamoja na Coaster kuwa katika mwendo mkali, chanzo kikubwa cha ajali hiyo ni Canter iliyoogeshwa barabarani  na wahusika kugeuza barabara gereji ya kutengeneza magari, kwani walishusha hadi difu ya nyuma kwa ajili ya matengenezo.

Kuhusu ajali ya pili Kamanda Mwakyoma alisema ilihusisha lori namba T 817 AZU likiwa na tela T651 AMZ lililokuwa limebeba mbao kuelekea Dar es Salaam, lori namba T 890 AUR na fuso namba T317 ATN liloloengeshwa barabarani baada ya kuharibika.

Kamanda Mwakyoma alisema lori lenye mbao namba T 817 AZU na tela T 651 AMZ liligonga kwa nyuma lori namba T 890 AUR lililokuwa likiendeshwa na  Bw. Anthony Mapembe kisha kuligonga Fuso lilikuwa limeharibika na kuacha njia na kuigonga baa ya By Night  ambapo watu watatu walikufa na majeruhi kulazwa hospitali ya Tumbi.

1 comment:

  1. Hizi ajali, lini sisi tutakuja kuachana nazo, Tanzania tuliumbwa kuwa nchi ya Majanga, mara Mabomu, Ajali, Mafuriko, Magonjwa!Jamani.

    ReplyDelete