28 March 2011

Botswana yatinga fainali za Mataifa ya Afrika

N'DJAMENA, Chad

TIMU ya taifa ya Botswana imekuwa timu ya kwanza kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika, zitakazofanyika mwakani huku ikishuhudiwa mabingwa wa zamani wa michuano
hiyo, timu za taifa za Misri na Cameroon zikivutwa shati.

Mchezaji Jerome Ramatlhkwane, ndiye aliyekuwa shujaa wa timu hiyo ya Zebras, baada ya kuifungia bao pekee lililoipatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chad katika mchezo huo uliofanyika mjini N'Djamena.

Bao lililopatikana dakika ya 50 na liliifanya Botswana ifikishe pointi 16, katika mechi za kundi K ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine katika kundi hilo.

Katika mechi nyingine ya kundi hilo, bao pekee lililofungwa na Moses Chavula dakika ya 18 liliisaidia Malawi kuondoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Togo, ambayo haina uwezo wa kufuzu fainali hizo zitakazofanyika nchini Gabon na Equatorial Guinea.

Matokeo mengine ya mechi zilizochezwa juzi, Afrika Kusini iliwashangaza wengi baada ya kuilaza Misri kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika mjini Johannesburg.

Mchezaji Katlego Mphela, ndiye aliyepachika bao hilo dakika za majeruhi za mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Ellis Park, huku wageni wakipata nafasi nyingi lakini wakashindwa kuzitumia.

No comments:

Post a Comment