27 March 2011

'Bomu' lalipuka na kuua fundi Mbagala

Na Charles Lucas

MKAZI wa Mtoni Msikitini jijini Dar es Salaam, Bw. Joseph Blazio (29) ambaye ni fundi chuma amekufa baada ya kulipukiwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu
wakati akikata vyuma chakavu kiwandani juzi majira ya jioni.

Tukio hilo lilitokea kwenye Kiwanda cha kutengeneza nondo cha A.M.Steel & Iron Mills Limited, kilichopo Mbagala Zakhem Dar es Salaam. wakati mafundi wa kiwanda hicho wakiendelea na kazi ya kukata vyuma kabla ya kuingiza kwenye mashine za kuyeyusha vyuma hivyo.

Baadhi ya mashuhuda ambao hawakutaka kutaja majina yao walisema tukio hilo lilitokea majira yakati ya saa 9 : 30 na walistuka baada ya milipuko mkubwa uliofuatiwa na moshi kwenye eneo hilo na kuwasababisha hofu kubwa.

Naye Mmoja wa walinzi waliokuwapo kiwandani hapo ambaye hakutaja jina kwa kuhofia kupoteza kazi, alisema tukio hilo la kusikitisha lilitokea ndani ya jengo dogo kiwandani humo ambalo huhifadhiwa vyuma mara baada ya kupimwa uzito.

Mmoja wa mafundi wa kukata vyuma kwenye kiwanda hicho aliyekuwapo wakati wa tukio hilo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake alisema kabla ya tukio lile, marehemu alikuwa akikata chuma kwa kutumia gesi na kutokea cheche.

Aliongeza kuwa cheche hizo ziliingia kwenye bomba kubwa linalosadikika kuwa bomu, lililolipuka na vipande vya chuma kumtoboa tumbo na kutokea upande wa pili na vingine kumkata mguu kwenye kisigino.

Pia aliongeza kuwa kabla ya tukio hilo siku moja kabla ya tukio hilo ndani ya kiwanda hicho liliokotwa bomba linalosadikika kuwa ni bomu na haikufahamika uongozi wa kiwanda hicho ulikolipeleka.

Gazeti hili lilizungumza pia na ndugu wa marehemu akiwamo mdogo wake  aliyejitambulisha kwa jina Bw. Gaspal William alisema kuwa yeye alipata taarifa za tukio hilo saa 10 jioni akiwa katika shughuli zake na kutokana na kujeruhiwa vibaya alikuwa amekwishakufa.

Naye Mjomba wa marehemu Bw. Lenard Manolo huku akiwa mwenye masikitiko makubwa alisema kwa jinsi alivyouona mwili wa marehemu wakati wa kuusafisha ulikuwa umechanwa eneo la tumbo na kuacha tundu kubwa lilotokea mgongoni pia sehemu ya mguu mmoja kisigino kilikatika kabisa na kuiomba Serikali kufuatilia kwa umakini suala hilo ili haki itendeke.

Juhudi za gazeti hili kuwatafuta viongozi wa kiwanda hicho ili kuelezea tukio hilo zilishindikana baada ya mwandishi kuelezwa kuwa hawakuwapo kiwandani hapo jana. Mwili wa marehemu ulisafirishwa jana kwenda Tanga kwa maziko yanayotarajiwa kufanyika leo. Tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha Polisi Mbagala Kizuiani.

No comments:

Post a Comment