Na Reuben Kagaruki
WABUNGE wa Kamati ya Bunge, Katiba, Sheria na Utawala wamekataa watumishi wa halmashauri nchini kusimamia fedha na miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF), na badala yake kuelekeza utaratibu uliokuwa ukitumika wakati wa awamu ya kwanza ndio utumike sasa.
Wabunge hao walikataa watumishi wa halmashauri kusimamia fedha za mfuko huo, Dar es Salaam jana walipotembelea ofisi za TASAF na kuzungumza na uongozi wa juu.
"Umuhimu wa mfuko huu unafahamika sana, mfuko uliipa serikali ya awamu ya tatu na ya nne heshima kubwa," alisema mbunge wa Manyoni Magharibi, Bw. Paul Lwanji na kushauri usimamiwe vyema ili uwe endelevu
Alishauri TASAF iwe na watendaji wake kwenye halmashauri. "TASAF iwe na watu wake, wale wa halmashauri ni wajanja sana, maana unakuta kitu kinaanza vizuri, lakini wengine wanafikiria mianya ya kuanza kuchakachua," alisema Bw. Lwanji.
Kwa upande wake mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Azza Hamad, alisema kuna tatizo la miradi kukwama hali inayotokana na wataalamu wa halmashauri kutoisimamia ipasavyo.
"Watumishi wa halmashauri wanaona shughuli za kusimamia miradi ya TASAF sio sehemu yao ya kazi," alisema Bi. Hamad.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, mbunge huyo alishauri wawepo wakaguzi wa TASAF wanaoenda kuhakiki kama miradi inayotekelezwa ndani ya jamii imekamilika na sio kutumia wataalam wa halmashauri.
Mbunge mwingine aliyepinga watumishi wa halmashauri kupewa jukumu la kusimamia na kukagua miradi ya TASAF ni Bw. Gosbert Blandesi, ambaye alishauri TASAF iajiri watumishi wake.
"TASAF iajiri watumishi wake wa kwenda kufanya ukaguzi wa miradi badala ya kutumia wale wa halmashauri," alisisitiza wakati akitoa mchango wake.
Baada ya majadiliano ya muda mrefu huku wabunge hao wakionekana kuwatilia shaka watumishi wa halmashauri, ndipo aliposimama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Bw. Stephen Wassira na kusema TASAF inapenda kuwa na watumishi wake kwenye halmashauri kama ilivyokuwa wakati wa awamu ya kwanza.
Kauli hiyo iliungwa mkono na wabunge wote wa kamati hiyo. Awali Kaimu Mkurugenzi wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga , alisema awamu ya kwanza ilikuwa na mafanikio makubwa kwa sababu mfuko huo ulikuwa na wahasibu wake kwenye halmashauri.
Kwa sasa TASAF imeingia mkataba na wakurugenzi wa halmashauri ambao wameupatia mfuko huo watumishi wawili kwa ajili ya kuratibu shughuli za mfuko.
No comments:
Post a Comment