31 March 2011

Mnyika ashtukia mudawa wa mabadiliko ya katiba

Na Rabia Bakari

MBUNGE wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA), Bw. John Mnyika amedai kushtushwa na maudhui ya muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa
mwaka 2011 uliochapwa katika Gazeti la Serikali toleo No. 1 Vol. 92 la Machi 11, mwaka huu, akidai kuwa hauna nia ya dhati ya kuleta mabadiliko ya katiba.

Bw. Mnyika alisema jana kuwa kilichomshtua zaidi ni mamlaka makubwa aliyonayo rais katika muswada huo, ambapo maudhui yamedhihirisha tahadhari aliyotoa mara kadhaa kwamba serikali haina dhamira ya kweli ya kuhakikisha panakuwepo na mchakato mzuri wa kuwa na katiba mpya.

Alisema kuwa muswada huo umelenga kuhalalisha yote ambayo yalitangazwa kufanywa na rais kuhusu mchakato wa katiba mpya na kupingwa na wadau mbalimbali, ambapo sasa yanataka kupewa uhalali kwa sheria inayotaka kutungwa na bunge kupitia muswada huo.

"Muswada huo unataka kumpa mamlaka rais ya kuunda tume ya kuongoza mchakato mzima wa katiba bila kuhusisha bunge ama wadau wengine wa msingi. Muswada huo pia utaka kumpa rais mamlaka ya kuteua wajumbe wa tume husika bila kushauriana na mtu yoyote isipokuwa Rais wa Zanzibar.

Muswada huo unaelekeza kuwa katika kuteua wajumbe, rais atazingatia uwakilishi wa makundi ya kijamii, lakini makundi husika hayatajwi hata kwa ujumla wake na hivyo kuacha mamlaka yote ya kuamua uwakilishi kubaki kwa rais," aliongeza.

Mambo mengine yaliyomo kwenye muswada huo, Bw. Mnyika aliyataja kuwa ni pamoja na kumpa rais mamlaka ya kutengeneza hadidu rejea za tume jambo ambalo lilipaswa kufanywa na bunge kwa kuwa sehemu ya sheria husika ama kufanywa na Mkutano Mkuu wa Kikatiba.

Aliongeza kuwa kwa kutoa mamlaka ya kuunda hadidu rejea kwa rais mwanya umetolewa kwa mtu mmoja kuweka mipaka ya nini kinastahili kufanywa na tume wakati wa mchakato wa katiba mpya na hivyo kuminya wigo wa mabadiliko.

"Muswada huo unataka tume iwasilishe ripoti yake kwa rais ambaye atampa nakala Rais wa Zanzibar na baadaye kumwelekeza waziri mwenye dhamana kupeleka bungeni yale atayoamua rais. Muswada huu kwa kuwa na kifungu hiki utaendeleza yaliyofanywa na marais waliopita kuhusu ripoti na mapendekezo ya tume zingine na hivyo kukwamisha mabadiliko ya kweli," alisema Bw. Mnyika.

Pamoja na hayo, aliongeza kuwa muswada huo unataka kutoa mamlaka finyu kwa jukwaa linalohusiana na mambo ya katiba tofauti na mkutano mkuu wa kikatiba ambao ungekuwa na mamlaka zaidi katika mchakato husika.

Aidha kwa mujibu wa Bw. Mnyika pia, muswada huo unataka kutoa mamlakama kubwa kwa rais kuteua wawakilishi wa chombo kikuu zaidi katika mchakato wa katiba bila kushauriana na kundi lolote ama wananchi kuhusika katika uteuzi ama kuwa na wawakilishi walioteuliwa na makundi yenyewe, mathalani vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama wa wakulima, vyama vya wanafunzi, vyama wa wafanyakazi na wengineo.

Alisema muswada huo unataka Rais ashauriane na Rais wa Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pekee ambapo pia unatoa mamlaka makubwa zaidi ya rais kuamua hata kufanya bunge la kawaida kuwa ndilo bunge la katiba, jambo ambalo linaweza kurejesha udhaifu uliofanywa katika mchakato wa katiba inayotumika sasa ambapo umma uliporwa wajibu na mamlaka yake ya kushiriki moja kwa moja katika kupitisha katiba.

"Muswada kwa ujumla haujaeleza muda wa mchakato wa katiba na vipindi vitavyotumiwa na vyombo mbalimbali katika hatua mbalimbali za mchakato wa katiba; ama kutoa mamlaka ya kuwekwa kwa muda huo kwa chombo chenye uwakilishi mpana wa umma kama mkutano wa katiba au bunge na hivyo kutoa mwanya kwa mchakato mzima kucheleweshwa," alisema.

Bw. Mnyika alikumbusha kuwa mnamo Februari 9 mwaka huu, alitoa tamko kuwa alipokea kwa tahadhari uamuzi wa Serikali kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kubadili misimamo ya awali kuhusu mchakato wa katiba mpya na kuamua kukubaliana na mwito wa kutaka mchakato husika uanzie bungeni kupitia kutungwa kwa sheria ya bunge ya kuratibu na kusimamia mchakato husika kama alivyokuwa akitoa mwito kwa nyakati mbalimbali.

7 comments:

  1. Halafu mbona unasomeka marekebisho ya Katiba (review) badala ya Mchakato wa kutengeneza katiba mpya?

    Tunaomba Serikali isipuuze maoni yetu wananchi. Kwanini haitaki kukubaliana nasi?

    Imefata Mawazo ya Jaji Werema ambaye alishatamka kuwa hakuna hitaji la Katiba Mpya.

    ReplyDelete
  2. Tatizo la watawala ni kwamba kila wanapobanwa na hoja fulani huamua kuzifuta kiaina. Issue ya katiba mpya si ya mjadala lakini imegeuzwa na kuwa marekebisho ya katiba? Katiba imerekebishwa mara ngapi? Serikali inajua kuunda katiba mpya ni mwanzo wa mwisho wao wa utawala. Watanzania lazima tuamke tusikubali kuburuzwa, nchi ni yetu sote si watawala pekee.

    ReplyDelete
  3. ni assumption yangu kuwa Rais na waziri mkuu wanasoma au kupitia watu wao maoni haya huyapata.
    NAOMBA NIWASHAURI MHE. KIKWETE NA MHE.PINDA MALIZENI KAZI VIZURI KWA KUWATENDEA HAKI WATANZANIA HUSUSA NI KWENYE SUALA LA KATIBA MPYA. WATANZANIA WANAISUBIRI KWA HAMU. TANZANIA YA LEO SI YA JANA. MAPINDUZI YATALETWA NA VIJANA WENGINE SIO HAO UVCCM (WATOTO WA MANYANG'AU NA MAFISADI)

    ReplyDelete
  4. Ni dikteta tu ndiye anayeweza kufanya kila kitu peke bila kushirikisha wengine. Sipendi kuamini kama Tanzania inaoongozwa kinamna hiyo. Lakini dalili ya mvua ni mawingu. Nashawishika kusema kuwa kwa namna hii ilivyo, huenda tunaongozwa kidikteta bila kujua, maana demokrasia inazidi kuminywa siku hadi siku. Tusikubali hali hii.

    ReplyDelete
  5. mbona mswada ulikuwa ni katiba mpya sasa inakuwaje kuwa ni marekebisho?si katiba hii ilikwisha fanyiwa marekebisho zaidi ya mara mbili, hatuwezi kuendelea na mfumo uliopitwa na wakati

    ReplyDelete
  6. tunataka Katiba Mpya na si Marekebisho.

    ReplyDelete
  7. watanzania jambo la msingi hapa ni katiba mpya na si marekebisho ya katiba hapa tumechoshwa na ufisadi wa baadhi ya watu mpaka kieleweke lasi hivyo tuandamane kutetea haki yetu tunamuomba raisi kikwete aliangalie hili suala la katiba

    ReplyDelete