Na John Daniel
BAADHI ya wakazi wa Kurasini na Kigamboni Dar es Salaam wamewaweka kiti moto watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa tuhuma za
rushwa na urasimu na kumtaka Waziri wa wizara hiyo, Profesa Anna Tibaijuka kuwafukuza kazi kabla hawajampa ugonjwa wa shinikizo la damu.
Wananchi hao wanaotarajiwa kuhamishwa kupisha uendelezaji wa mji mpya wa Kigamboni na upanuzi wa bandari katika eneo la Kurasini, walifikia hatua hiyo jana wakati Prof. Tibaijuka alipowatembea kujibu maswali yao kuhusu tathmini na ulipaji fidia.
Katika eneo la Kurasini Kata ya Kurasini, wananchi hao walionesha hasira zao na kukataa ombi la msamaha wa Prof. Tibaijuka kuwaomba wamsamehe Mratibu wa Mradi huo, Bw. John Mhando.
"Hatumtaki Mhando, hatumtaki Mhando, anatunyonya, anachakachua hela zetu, mfukuze, hatumtaki," walisema wananchi hao wakati Waziri Tibaijuka akihutubia.
Katika maelezo yao, wananchi hao walidai kuwa kazi ya tathmini ilitawaliwa na rushwa na urasimu mkubwa na kwamba maofisa wa wizara hiyo wanatumia nafasi hiyo kuingiza majumba hewa kujilipa mabilioni ya fedha.
"Mimi ni mjane, sina mume na nilikuwa na mtoto mmoja tu naye alishatangulia mbele ya haki akaniachia wajukuu watatu nawalea kwa kodi ya wapangaji.
"Lakini siku walipokuja kufanya tathmini, waliniandika vyumba vitano tu, sita wakaacha, hata choo changu cha ndani chenye marumaru na bafu ya kuogelea walikataa, wakaandika choo cha shimo cha nje," alisema Bi. Rose Ngongo.
Alisema alipofuatilia wizarani alitakiwa kuandika barua ambayo aliandika mwaka huo huo 2009, lakini hakupata majibu hadi mwezi huu alipoletewa notisi ya kutakiwa kuhama na kuvunja nyumba yake ndani ya siku saba.
"Kazi ya tathminini ilitawaliwa na usiri mkubwa, tunasikia kuna fomu namba 70 tunatakiwa kujaza lakini hatujaiona, kama ungeangalia hiyo fomu ungeona maghorofa hewa yameingizwa humo na hao wajanja ili kujipatia pesa.
"Tathamini ya nyumba inaweza kuwa milioni 100/- lakini akalipwa milioni 25/- na wajanja wakabaki na milioni 75/- maana hatujui kilichoandiwka kwenye hizo fomu. Mhando (John) amekuja hapa kwa sababu ya kuja kwako wewe, hakuna mtu ambaye watu hawamtaki kama Mhando," alisema Bw. Abdlallha Kavinga.
Wananchi hao walimtaka Waziri Tibaijuka kumfukuza kazi Bw. Mhando au kumwondoa na kumzuia kujihusha kabisa na mradi huo kwa madai kuwa anawapunja haki zao.Akijibu malalamiko hayo Prof. Tibaijuka aliwaomba wananchi hao kusahau mambo ya nyuma na kutambua kuwa hakuna haki ya mtu itakayopotea.
"Kwa kweli lazima niwaombe radhi kwa usumbufu, nawaomba mvute subira Wizara ya Ardhi inaongozwa na mimi, hakuna atakayechakachua malipo yenu.
"Tutaangalia list (orodha) yote ya waliolipwa fidia tukikuta maghorofa yamelipwa wakati hayapo TAKUKURU na polisi wataifanyi kazi haraka," alisema Prof. Tibaujuka na kuongeza:
"Kama kweli serikali imelipa ghorofa hewa hapo patawaka moto. Lakini naomba niulize wakati haya yanafanyika viongozi walikuwa wapi," alihoji Waziri Tibaijuka huku wananchi wakijibu kuwa "walikwepo".
Prof. Tibaijuka alipata wakati mgumu zaidi pale wananchi walipoweka wazi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ni kikwazo kikubwa wanapodai haki zao wanaelekezwa kwake lakini hajibu barua zao wala kukubali kuoanana nao.
"Ni rahisi kumwona Rais Kikwete kuliko kumwona Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi," alisema Bw. Omar Mkung'ata.
Prof. Tibaijuka aliwahakikishia wananchi hao kuwa watapata haki zao, huku akiwaeleza wazi kuwa hivi sasa wizara yake imepata Katibu Mkuu mpya na si wa zamani.Katika eneo la Kigamboni, wananchi walimwonya Prof.Tibaiukka kuwa asipowaondoa watendaji wake wala rushwa na warasimu watamaliza.
"Mhe. Waziri tunakufahamu, wewe ni mtendaji lakini angalia majambazi wako wizarani kwako, usipowandoa watakuondoa, watakupa presha na utabaki kulala nyumbani bure," alisema Evarist Mwita.
Mh.Waziri tumemshangaa kuja Kigamboni hakuna jipya aliloleta ni yaleyale ya kuwa mradi upo na haubadiliki maana wameshatwaa.
ReplyDeleteWananchi tupo ktk kifungo tokea 2008,hatujui khatma yetu,miradi imesimama nyumba huwezi malizia wala mpya hujengi tena,mikopo hatupati maana haijulikani mwisho wake ni nini? watu wanataka kujuwa Lini mradi utaanza,lini tathmini itafnyika,na je,hao watu wameandaliwa wakilipwa hapo waende wapi? Leo Waziri hata Raisi alipokuja zindua kivuko 2009 alisema hakuna atakaehamishwa!! ila kuna nyumba zitakazojengwa ndio watu watahamishiwa humo, hizo nyumba zitaanza kujengwa lini na pesa zinatoka wapi? maana tumesikia zaidi ya Trillion 1.6 za kuanzia mradi wote ni trillion 11.6 sasa tuko ktk kujitolea kukaa bila kazi maalumu mpk lini?
Waziri kaja anasema tufute yaliyopita sasa tunajipanga upya na hata huyo Mkurugenzi wa mji mpya kampa jamaa yake,hivi kujipanga huku tokea 2008 na mpk sasa kaja kufanya nini?