Na Zuhura Semkucha, Shinyanga
WATU watatu wamekufa, wawili kwa kuuawa katika kile kinachoaminika kuwa mauaji ya vikongwe yanayotokana na imani za kishirikina na mwingine kwa
ajali mkoani Shinyanga.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Shinyanga, Bw. Justice Kamugisha amesema kuwa tukio la kwanza limetokea katika kijiji cha Dutwa ambapo mwanamke mmoja aliuawa akiwa amelala usiku wa saa 8:30.
Kamugisha alimtaja mwanamke huyo aliyeuawa kuwa ni Elizabeth Mombi (60) ambaye aliuawa akiwa amelala na mtoto wake ambapo watu wasiofahamika walimvamia na kumkata mapanga kwa imani za kishirikina.
Kaimu Kamanda huyo alisema kuwa katika kijiji cha Sengwa wilayani Maswa mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Jajadi Tungu aliuawa kwa kushambuliwa na wananchi na kisha kuchomwa moto na kundi la watu hadi kusababisha kifo chake.
Chanzo cha kuuawa kwa mtu huyo inadaiwa kuwa alichukua mpira wa kunyunyizia maji shambani uliokuwa unamilikiwa na Bw. Bida Mahona ambaye anashikiliwa na polisi kwa mahojiano.
Katika Wilaya ya Meatu gari lenye namba za usajili T 794 ALU aina ya Toyota Land Cruise limepinduka baada ya kuacha njia na kusababisha kifo cha dereva wake Bw. Iddi Ramadhani.
Gari hilo lilikuwa linatoka Ngorongoro, Arusha ambapo walipofika katika kijiji cha Itinje Meatu lilipinduka na kutumbukia kwenye mtaro na kusababisha majeraha kwa watu wanne ambao wamelazwa katika Hospital ya Wilaya ya Meatu.
Waliolazwa ni Jesca Philipo, Peter Isuma, Philipo Elius, Joyce Petro wate wanaendelea hali zao zinaendelea vizuri.
No comments:
Post a Comment