23 March 2011

Mrema atangaza vita na halmashauri

Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imetangaa vita na halmashauri zote nchini ili kukomesha ubadhirifu wa fedha za Serikali unaofanywa na
baadhi ya watendaji wa halmashauri hizo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. Augustino Mrema aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari na kutoa ufafanuzi wa matokeo ya ukaguzi wao katika baadhi ya halmashauri mkoani Kilimanjaro.

Alizitaja halmashauri hizo kuwa ni Moshi Vijijini, Mwanga, Same na Rombo ambazo katika ukaguzi wao walibaini ubadhirifu mkubwa wa fedha za maendeleo ya wananchi.

“Lengo la kamati hii ni kufuatilia nidhamu ya matumizi ya fedha za serikali asilimia 65 ambazo hupelekwa katika halmashauri ili kuharakisha maendeleo lakini zinatumika kinyume na malengo yaliyokusudiwa,” alisema Bw. Mrema.

Alisema serikali imeonesha kufurahishwa kwao na utendaji kazi wa kamati hiyo ambapo juzi, kamati ya LAAC ilikutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bw. George Mkuchika na Manaibu wake Bw. Kassim Majaliwa na Bw. Aggrey Mwanri kwa lengo la kubadilishana mawazo.

Bw. Mrema alisema katika mazungumzo na mawaziri hao, kamati hiyo ilieleza matokeo ya ukaguzi wao mkoani Kilimanjaro ambako walibaini wizi wa fedha, ukosefu wa kumbukumbu za mahesabu na uwajibikaji mdogo wa baadhi ya wakurugenzi na watendaji katika halmashauri walizozifikia.

“Tulipofika Same na Moshi Vijijini, tulibaini uozo mkubwa hivyo kamati iliagiza wakurugenzi wake, wachukuliwe hatua ya kutozwa tozo la asilimia 15 katika mishahara yao.

“Tozo hili litakatwa katika kipindi cha mwezi mmoja, pia tuliiomba wakurugenzi hawa waandikiwe barua za onyo na TAMISEMI, imekubali ombo letu kwani bila kuchukua hatua kali kwa watendaji wa halmashauri, uozo huu utakuwa ukiendelea,” alisema Bw. Mrema.

Aliongeza kuwa, matumizi mabaya ya fedha za Serikali katika halmashauri yameanza muda mrefu bila wahusika kuchukuliwa hatua hivyo kumwamisha huduma muhimu kwa wananchi.

Alisema kutokana na hilo, kamati hiyo imeamua kuongeza kasi katika ukaguzi wa mahesabu ili fedha zinazokwenda halmashauri, ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa wakishirikiana na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Bw. Mrema alisema, moja ya madudu yaliyojitokeza katika ukaguzi wao ni pamoja na milioni 15 kutumika kama posho za watendaji wa halmashauri katika vikao wakati miradi ya maendeleo ikikwama kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

Aliongeza kuwa, hivi karibuni watatoa ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro ambayo Mkurugenzi wake, amesimamishwa kazi baada ya kununua 'injector pump' ya gari aina ya Land Rover kwa sh. milioni 15.

No comments:

Post a Comment