Na Godfrey Ismaely
JITIHADA mpya za kuharakisha maendeleo kwa wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba zimeelezwa kuwa zitafanikiwa pindi wanaharakati wote wa
maendeleo wa visiwa hivyo walioko bara na nje ya nchi watakubaliana kuunganisha nguvu na kuanzisha kampeni za maendeleo.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Business Times Ltd (BTL), ambayo inachapa magazeti ya Majira, Dar Leo, Spoti Starehe na Business Times, Bw. Rashid Mbuguni wakati wa mkutano wa pamoja na wafanyabiashara mbalimbali kutoka visiwani humo ambao wanaishi jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ambao ulifanyikia jana katika ukumbi wa mikutano wa BTL lengo lake lilikuwa ni kuwaelezea wadau hao jitihada mpya za gazeti la Majira za kuhakikisha kuwa linawashirikisha wadau hao ili kurejesha matumaini ya maendeleo katika jamii zao na hata taifa kwa ujumla.
Mkurugenzi huyo aliwaambia wadau hao kuwa wanapaswa kuunda kamati ambayo itaweza kufikisha ujumbe kwa ngazi husika kutokana na ukweli kwamba kwa kushirikiana na vyombo vya habari kama gazeti la Majira ujumbe wa maendeleo utakuwa rahisi kuwafikia walengwa pamoja na wananchi.
Alisema kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Majira katika Mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na hata Visiwani uligundua kuwa kuna sababu mbalimbali zinazochangia kuzorotesha maendeleo hivyo kwa kuwashirikisha wadau hao zitapatiwa ufumbuzi mapema.
Bw. Mbuguni alisema kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kurudisha maendeleo nyuma ni pamoja na jamii kujijengea dhana ya kwamba pasipokuwa na mitaji hawawezi kufanya shughuli yoyote ya maendeleo, ubinafsi, chuki, maradhi, uhalifu, kukosa uelekeo na kukata tamaa kunakosababisha na hujuma mbalimbali.
Hata hivyo alisema kuwa mkakati mpya unaoratibiwa na Majira ambao umeanzia katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Kilimanjaro na hivi karibuni katika Visiwa vya Pemba na Unguja ikiwamo mikoa ya Morogoro na Dodoma kwa kuwashirikisha wadau, wananchi na hata serikali umelenga kurejesha matumaini ya maendeleo kwa jamii.
"Licha ya kuhamsha hamasa pia Majira limejipanga kuunganisha nguvu za wadau kwa kushirikiana na wananchi ili zile kero ambazo zinakwamisha maendeleo yao ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa wakati," alisema Bw. Mbuguni
No comments:
Post a Comment