23 March 2011

Wasanii 13 Five Stars wafa ajalini

Na Waandishi Wetu

NYOTA ya kikundi cha muziki wa taarab cha Five Stars iliyongara katika ulimwengu wa muziki imezimika ghafla usiku wa kuamkia leo baada ya gari walilokuwa wakisafiria
kupata ajali eneo la Doma mkoani Morogoro na kuua wanamuziki 13 papo hapo.

Ajali hiyo ilitokea saa mbili usiku wakati hicho kikiwa safarini kwenda Dar es Salaam kikitokea Mbeya na Iringa kilichofanya tamasha la muziki, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugonga lori lenye shehena ya mbao lililokuwa limesimama maeneo ya kijiji cha Doma, mpakani mwa mbuga ya wanyama ya Mikumi, Kilosa mkoani Morogoro.

Kamanda  wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Adolphina Chialo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea saa 2.30 usiku na kuwataja waliokufa katika ajali hiyo wametajwa kuwa ni pamoja na kiongozi wa bendi hiyo, Nasoro Madenge, Issa Kijoti, Husna Mapande na Shaaban Juma (ambaye alikuwa mpiga kinanda).

Wengine ni Hamisa Musa, Omari Hashimu, Omary Hashimu (mpiga gitaa), Tizzo Mgunda, Ramadhan Kinyoa, Omary Tall 'Fundi Mitambo', Haji ‘Mbeba Vyombo’ na Nassor Madenge (Mhasibu).

Walionusurika katika ajali hiyo ni Ally Juma 'Ally J', Mwanahawa Ally, Samila, Issa Kamongo, Mwanahawa, Zenna Mohamed, Shaaban Mfupi ' Fundi Mitambo', Rajabu Kondo na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Haji.

Mwenyekiti wa kikundi hicho, Khamis Slim, alilieleza gazeti dada la Dar Leo wamepokea kwa masikitiko taarifa za ajali hiyo hizo na yeye pia amenusurika kwa kuwa hakuwapo kwenye ziara hiyo kwa sababu alikuwa amefiwa.

“Sina cha kuzungumza zaidi, lakini pengo tuliloachiwa ni kubwa mno na nadhani hakuna atakayeweza kuliziba,” alisema Slim na kuongeza, “Tumepoteza vijana wengi wenye uwezo wa hali ya juu wa kisanii. Hili ni pigo kwa kundi, vikundi, taifa na familia pia kutokana na michango yao katika fani hiyo.”

Five Stars imetamba kwa nyimbo za Wapambe Msitujadili (Nchumu nchumu tena mwawah!) wa Musa Kijoti, La Uchungu Halisauliki' (Zenna), Riziki Mwanzo wa Chuki, Shukrani kwa Mpenzi na nyinginezo.

Inadaiwa kuwa gari lililowabeba wasanii hao lilikuwa katika mwendo kasi na lilipojaribu kulipita lori hilo kulitokea lori jingine mbele yaka lililokuwa likitokea Morogoro kwenda Iringa lenye nambari T 530 BHY na tela nambari T 182 BKB ambalo nalo lilikuwa katika mwendo kasi hivyo dereva wa gari la wasanii hao akalazimika kurudi kushoto na kuligonga kwa nyuma lori lililoharibika.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Morogoro, Ibrahim Mwamakula alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari la wasanii hao.

Kamanda Mwamakula amesema miili ya marehemu hao imeharibika vibaya kwani mbali na kukandamizwa na vyuma vya gari lao, walichomwa na kutobolewa tobolewa miili yao na mbao zilizokuwa katika roli lililogongwa.

Kamanda Mwamakula amesema wasanii hao walikuwa katika ziara ya kikazi katika wilaya ya Kyela mkoani Mbeya na walikuwa wakirejea baada ya kumaliza ziara hiyo.

Amesema vyombo vya muziki vya wasanii hao vilivyokuwa ndani ya gari hilo vimeharibika kabisa.

Kamanda Mwamakula amesema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro wakati majeruhi tisa wa ajali hiyo wanaendelea na matibabu hospitalini hapo. Habari zaidi ukurasa wa 16.

3 comments:

  1. Mwenyenzi-Mungu tunamwomba azilaze roho za marehemu wote mahala pema peponi-AMIN

    ReplyDelete
  2. HUU NI MSIBA WA TAIFA ZIMA MAANA NI PIGO KUBWA SANA,TENA WAMEKUFA KIFO KIZITO SANA YAANI HUWEZI JUWA NYAMA HII NI YA NANI NA HII NI YUPI INASIKITISHA SANA!!TUNAKUOMBA MWENYEEZI MUNGU UZILAZE ROHO ZA MAREHEMU HAWA MAHALA PEMA PEPONI AMIIIN, KWA UPANDE WA SERIKALI TUNAWAOMBA WAANZE MCHAKATO WA KUWEKA BARABARA PANA ZAIDI NA ZITENGANISHWE ZA KWENDA MBALI NA KURUDI MBALI KULIKO SASA TUNAKWEPANA AU KUPISHANA KWA HATUA MOJA NI KULENGANA NA NI HATARI SANA, TUJITAHIDI KILA MWAKA ANGALAU BARABARA MOJA MPK TUWEZE KUWA KAMA NCHI NYINGINE HII NAYO ITAPUNGUZA AJALI KWA KIASI KIKUBWA SANA.NAWAPA POLE NA WAFIWA WOTE WAWE NA SUBIRA HIYO NDIO JAALA YAO.

    ReplyDelete
  3. MwenyenziMungu tunamwomba alaze roho za marehemu mahala pema peponi-AMIN! lakini.....lakini,....likini hao walionusurika wanatakiwa kuwa makini,tena waache kufanya upuuzi na wamrudie muumba wao kumshukuru kuwanusuru kifo. na wewe mwanahawa ushakua mtu mzima kaa kwako tulizana tafuta shughuli nyingine ya maana, co kujiweka udogo nawakati ushazeeka! habari ndo hiyo.

    ReplyDelete