Na Damiano Mkumbo, Singida
WAKAZI wa Kijiji cha Wibia Kata ya Puma Katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida wanajenga zahanati na nyumba moja ya watumishi wa afya kwa gharama ya
sh. milioni 83.8.
Taarifa hiyo ilitolewa na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Bw. Damas Jingu kwa Naibu Waziri wa Nchi (Elimu), Bw. Kassimu Majaliwa alipotembelea kijiji hicho mwishoni mwa wiki.
Bw. Jingu alieleza kuwa mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka jana utawanufaisha wakazi 3,842 na kuondoa kero ya kutembea kilometa saba kufuata huduma za afya Makao Makuu ya Kata Puma.
Ofisa Mtendaji alifafanua kuwa ujenzi wa zahanati unagharimu
sh milioni 39,8 ambapo Halmashauri ya Wilaya imechangia sh milioni 35.5, wananchi sh. milioni 3.8 na wadau wengine sh 550,000/= .
Kuhusu nyumba ya kuishi familia mbili za watumishi zaidi ya sh. milioni 44 zimetumika, wakati wahisani kutoka Ujerumani walichangia sh milioni 37.5 na nguvu za wananchi sh milioni 6.5.
Alizungumza na wakazi hao baada ya kuweka msingi wa zahanati hiyo, Bw. Majaliwa aliwapongeza wakazi wa Kijiji cha Wibia kwa moyo wao wa kuchangia na kushiriki kikamilifu katika mradi huo ili kuboresha huduma za afya, kulingana na mpango wa taifa wa kujenga zahanati katika kila kijiji.
Kiongozi huyo alieleza kuridhishwa kwake na matumizi ya fedha yanayolingana na thamani ya mradi huo.
No comments:
Post a Comment