Na Raphael Okello, Bunda
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Bw. Cyprian Oyier amewataka wamiliki wa maduka ya dawa za binadamu wilayani
humo kuzingatia kanuni na sheria ya biashara hiyo kama inavyoelekezwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Akifunga semina ya wiki tano kwa watoa dawa muhimu za binadamu (ADDO) jana, Bw. Oyier alisema kuwa wapo wamiliki wa maduka hayo ambao wamekuwa wakikiuka sheria ya biashara hiyo na kwamba serikali haitasita kuwachukulia hatua ya kisheria ikiwa ni pamoja na kufunga maduka hayo.
“Ninaowaomba wafanyabiashara wa dawa za binadamu wazingatie kanuni na sheria ili kuchangia katika kutoa tatizo la uvunjifu wa sheria katika utoaji wa huduma za dawa,†alisema Bw. Oyier.
Kwa mujibu wa Bw. Oyier wapo wamiliki na watoa dawa katika duka la madawa ambao wamekuwa wakiuza dawa zilizoisha muda, kushiriki katika kutoa mimba kwa wasichana na akina mama na wengine kuendesha shughuli zao katika mazingira yasiyokidhi viwango, jambo alilosema ni kosa la jinai.
Naye mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA), Bw. Ramadhani Msuya alisema kuwa mpango wa maduka ya dawa muhimu (ADDO) ni matokeo ya tathmini katika sekta ya dawa nchini kote ambapo TFDA kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la ‘Management Science for Health (MSH) ilibaini na kupata ufumbuzi wa matatizo katika sekta ya dawa.
Alisema matatizo hayo ni pamoja na kutopatikana huduma za dawa kwa wananchi waishio vijijini pamoja na wauzaji wa maduka ya dawa baridi kutokuwa na elimu ya dawa au tiba bado walijihusisha na hutoaji huduma za kuchoma sindano na kufunga vidonda.
Bw. Msuya alifafanua kuwa lengo la mafunzo hayo kwa watoa dawa wilayani Bunda ni kuwawezesha kupitia sheria, utoaji sahihi wa dawa na kupata elimu ya magonjwa yatokeayo mara kwa mara ndani ya jamii, huduma kwa magonjwa ya watoto kwa uwiano, staidi za mawasiliano kati ya mteja na mtoa dawa na utoaji wa ushauri nasaha kwa wagonjwa.
Aliongezea kuwa baada ya mafunzo hayo kukamilika nchini kote, TFDA itawachukulia hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni ya kutoa huduma hiyo wamiliki na watoa dawa ambao hawatatimiza vigezo vya kuwawezesha kuingia katika mpango wa ADDO.
No comments:
Post a Comment