Na Livinus Feruzi, Bukoba
MAMLAKA ya Majisafi na Majitaka mjini Bukoba (BUWASA) inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uharibifu wa vyanzo na uchakavu wa
miundombinu iliyojengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita ambayo inapelekea upotevu mkubwa wa maji na kusababisha kuwepo kwa mgao wa maji.
Katika kata tano za Manispaa ya Bukoba ambazo ni Nshambya, Kitendaguro, Rwamishenye, Hamugembe na Kibeta maji yanapatikana kwa mgao, kutokana na maji yanayozalishwa kwa siku kushindwa kutosheleza mahitaji ya wananchi.
Kaimu Mkurugenzi wa BUWASA, Bw. Vedasto Mutabasibwa alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya 23 ya wiki ya maji yaliyofanyika katika chanzo cha maji cha Kagemu kilichopo kata ya Kitendaguro mjini hapa.
Alisema kutokana na uharibifu wa vyanzo vya maji, BUWASA kwa sasa inazalisha lita za maji 900,000 tu kwa siku kati ya lita milioni 3 zinazohitajika.
Bw. Mutabasibwa alisema licha ya uharibifu wa vyanzo vya maji, pia mabomba yanayopitisha maji yamechakaa kutokana na kujengwa kwa muda mrefu uliopita kwa takribani miaka 50 iliyopita na kusababisha maji mengi kupotea.
Hivi karibuni Ofisa Uhusiano wa BUWASA, Bi. Juliet Shangali alisema asilimia 49 ya maji yanayozalishwa yanapotea kutokana na mtandao wa mabomba ya maji kuchakaa na wizi.
Naye Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dkt. Anatory Amani aliwataka wananchi wote kuwa walinzi wa vyanzo vya maji kwa kuhakikisha hawafanyi shughuli zozote za binadamu kwenye vyanzo vya maji.
Aliwataka watendaji wa kata na mitaa kutumia sheria katika kusimamia vyanzo hivyo ili wananchi wasivivamie na kuitaka BUWASA kupima maeneo yao ambayo ni vyanzo vya maji ili yafahamike na kuwa rahisi kuyatunza.
No comments:
Post a Comment