Na Elizabeth Mayemba
MKUTANO wa viongozi wa matawi wa Yanga, uliokuwa ufanyike juzi makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, ulishindwa kufanyika baada ya
kutokea mvutano baina ya wanachama hao ambao wengine walitaka ufanyika lakini wengine walikataa na hivyo ukavunjika.
Awali Katibu wa tawi la Uhuru, Dar es Salaam Edwin Kaisi alisema mkutano huo ajenda yake kubwa ilikuwa ni kumjadili Mwenyekiti wa matawi Mkoa wa Dar es Salaam, Mohammed Msumi juu ya utendaji wake ikiwemo na kukaa madarakani kwa muda mrefu.
Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Yanga, zinadai kuwa mkutano huo ulivunjika baada ya kutokea mabishano baina ya wanachama hao, kwa madai kwamba ulilenga kuleta vurugu ndani ya klabu yao.
"Kabla ya kuanza kwa mkutano kuliiibuka mabishano, ambapo baadhi ya wanachama walidai kwamba hawatakubali kuona mkutano huo unafanyika kwani ulilenga kuhatarisha amani ndani ya klabu hiyo, hasa kipindi hiki ambacho timu yao inakabiliwa na mechi tatu za Ligi Kuu ya Bara mzunguko wa lala salama," alisema kiongozi huyo ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake kwa kuwa si msemaji wa viongozi wa matawi.
Alisema baada ya mabishano hayo, mkutano huo ukavunjika na kila mwanachama akatawanyika.
Kwa upande wake Kaisi ambaye ndiye aliitisha mkutano huo, alisema kwamba walishindwa kufanya mkutano huo baada ya Kamati ya Utendaji ya matawi kuingia mitini.
Alisema kamati hiyo ya matawi, ina wajumbe watano lakini wanne waliingia mitini ambapo alibakia katibu peke yake, hivyo kuifanya kolam kushindwa kutimia ndiyo maana wakaamua kuahirisha mkutano huo.
"Mwenyekiti Msumi pamoja na wajumbe wengine wanne wa Kamati ya Utendaji ya Matawi waliingia mitini, hivyo tukaamua kuahirisha mkutano huo mpaka siku utakapopangwa kufanyika tena," alisema Kaisi.
No comments:
Post a Comment