24 March 2011

Simanzi, majonzi vyatawala mazishi Five Stars

Na Addolph Bruno

SIMANZI, vilio na majonzi ziliendelea tena jana kwa mashabiki wa taarabu katika jiji la Dar es Salaam wakati wa maziko ya wasanii wa Kundi la taarabu la
Five Stars waliopata ajali na 13 kufariki Dunia ambao baadhi yao walizikwa juzi usiku na wengine jana mchana.

Baadhi ya wasanii hao ambao walifariki katika ajali iliyotokea katika eneo la Duma ndani ya Hifadhi ya Mikumi, wakitokea Songea walizikwa kwa nyakati tofuati kutokana na miili yao kuharibika vibaya ambao wengine walizikwa Dar es Salaam na wengine katika Mkoa wa Pwani.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kiongozi wa bendi hiyo anayefahamika kwa jina la Ally Juma 'Ally J' alisema miili ya wasanii wawili iliyohalibika vibaya katika ajali hiyo, Issa Kijoti na Omary Hashim walizikwa usiku wa kuamkia jana ambapo Kijoti alizikwa nyumbani kwao Mtoni kwa Azizi Ally, Dar es Salaam na Omary alizikwa nyumbani kwao Kibaha mkoani Pwani.

Kiongozi huyo ambaye ni baadhi ya sehemu ya wasanii walionusurika katika ajali hiyo alisema mazishi ya wasanii hao yaliendelea kufanyika jana ambapo miili ya wasanii wengine watatu, ilizikwa kwa nyakati tofauti Jijini Dar es Salaa na Pwani.

Alisema wasanii waliozikwa katika mkoa wa Pwani ni aliyekuwa mpiga kinanda wa kundi hilo, Tizo Mgunda na mwimbaji Hamisa Omary ambao walizikwa jana asubuhi vijiji viwili tofauti mkoani Pwani ambako ni nyumbani kwa wasanii hao.

Ally J alisema Mgunda alizikwa katika kijiji cha Mkamba huku Hamisa yeye alizikwa katika Msongola vilivyomo katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

"Baada ya kutoka Pwani, kulikuwa na mazishi ya msanii mwingine Juma seba, naye amezikwa leo (jana) katika makaburi ya Madoto Mburahati hapa Dar es Salaam ambapo viongozi mbalimbali wa bendi tulijumuika katika mazishi hayo na sasa bado tunaangalia taratibu za wengine baada ya familia kupanga," alisema kiongozi huyo.

Msanii mwingine wa kundi hilo, Hammer Q alizungumzia kwa uchungu ajali hiyo iliyotokea baada ya yeye kuachwa njiani akisafiri kwa basi kwa kusema vifo vya wasanii hao ni pengo kubwa katika bendi hiyo na kwamba itachukua muda kusahaulika.

Mjomba wa marehemu Kijoti, Lugendo Somo alisema familia yao ipo katika kipindi kigumu baada ya kuondokewa na msanii huyo ambaye alikuwa tegemeo katika familia yao na kwamba watafanya hitima kesho asubuhi na kufuatiwa na sadaka nyumbanii kwao Mtoni kwa Azizi.

Alisema kutokana kifo hicho kilichosababishwa na ajali ya ghafla, familia yao imekaa na kuamua kufanya mapema hitima kumaliza shughuli za msiba huo baada ya hitima ya wasanii wote iliyoandaliwa na Baraza la wasanii iliyopangwa kusomwa leo.

Naye Dada wa marehemu Tizo Mgunda, aliyejitambulisha kwa jina la Halima Mgunda alisema familia yao imepokea kwa masikitiko kifo cha msanii huyo kutokana na kwamba alikuwa tegemeo katika familia yao na kuongeza kuwa amewaacha watoto wawili mmoja wa kike na mmoja wa kiume.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa bendi ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta' Asha Baraka, alisema katika tasnia ya muziki wa taarabu wamepata pengo kubwa ambapo kuliziba itachukua muda mrefu.

Alisema wamepoteza watu maarufu katika muziki huo hivyo ni vigumu kupata watu wanaofanana na wale waliopata ajali kwa ajili ya kuziba nafasi zao.

Alisema kuwa kupeteza maisha kwa wasanii hao kutafanya muziki huo kutokuwa na ladha kutokana na ushindani uliokuwepo kati ya Five Stars na Jahazi.

´´Tumepoteza watu muhimu katika muziki wa taarabu na pengo lao halitazibika mapema na ushindani katika muziki huo utakuwa mdogo sana kutokana na kupeteza wasanii wengi kwa wakati mmoja, tunaomba tutoe ushirikiano wa kutosha kwa ajili ya kuwapa moyo na kuwafariji ndugu wa marehemu,´´ alisema Asha.

1 comment:

  1. Aliowaua Zombe walikuwa wanyama au kwasababu hawakutunisha mifuko ya mafisadi? Roho ni roho tu hata za wale wa mv. bukoba walikufa na wamesahaulika lakini wa Zombe twasikia anadai mabilioni. Na hili je? Jadili

    ReplyDelete