Na Gladness Mboma
WALIMU wapya waliopangiwa vituo vya kazi katika wilaya ya Temeke wamedai kuingiwa na wasiwasi wa kuchakachuliwa kwa fedha zao za nauli na mizigo baada ya
kudai kwa muda mrefu bila mafanikio.
Wakizungumza na Majira jana Dar es Salaam mmoja wa walimu hao ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa niaba ya walimu wenzake alisema kuwa jumla ya walimu 130 wapya 2010 /2011 mpaka leo hawajalipwa fedha hizo za mizigo pamoja na nauli.
"Tunaofia fedha zetu kuchakachuliwa kwa sababu haituingii akilini walimu wenzetu kutoka mikoa mingine wawe wamelipwa fedha hizo, lakini sisi tuliopo hapa Dar es Salaam, ambapo ndiko kwenye chimbuko la wizara husika tuwe hatujalipwa," alisema.
Alisema kuwa kila wanapokwenda kwa Ofisa Elimu wa Manispaa ya Temeke amekuwa akiwazungusha na kuwaambia waandike barua kisha watazikagua,barua ambazo wanadai wameandika muda mrefu lakini hakuna utekelezaji.
Mwalimu huyo aliongeza kuwa mwanzo walikuwa wakidai fedha za kujikimu ambazo walifuatilia kwa muda mrefu na hatimaye walililipwa, ambapo walimu wa shahada ya kwanza alilipwa sh. 900,000 na wale wa diploma sh. 630,000.
Alisema kuwa wanashindwa kuelewa ni kwa nini Ofisa wa Elimu wa Manispaa Temeke anawazungusha na fedha hizo ambapo wanaamini kwamba zipo na kusisitiza kwamba waraka wa 2010/2011 unasema kuwa ni lazima walimu walipwe nauli na gharama zao za kusafirishia mizigo walikotoka.
Alisema kuwa walimu wenzao wa wilaya ya Ilala wanatarajiwa kulipwa wiki ijayo, ambapo kwa upande wa Kinondoni hawajasikia malalamiko yao ila wanaamini kwamba wamekwishalipwa.
Alisema kuwa kutokana na kuzungushwa kwa muda mrefu, kesho watakwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke ambaye ndiye muajiri wao ili kuonana naye na kama hakutakuwa na muafaka wowote watalazimika kugoma.
No comments:
Post a Comment