23 March 2011

Wakongwe Simba, Yanga waingiza mil. 13/-

Na Elizabeth Mayemba

MECHI ya wachezaji waliowahi kutamba na timu za Simba na Yanga maalumu kwa ajili ya kuchangi awaathirika wa mabomu yaliyotokea Gongolamboto hivi
karibuni iliyochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, umeingiza sh. milioni 13.2.

Fedha hizo zimetokana na mashabiki 10,796 walioingia uwanjani, ambapo kati ya hizo sh. milioni moja zimepangwa kupelekwa kwa waathirika wa mabomu leo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa mechi hiyo Seleman Mathew alisema timu hizo zilizoshiriki mchezo huo wa hisani kila moja iliambulia sh. milioni 1.1 kwa ajili ya maandalizi.

"Baada ya kufanya mchanganuo wa mapato yote kwa kulipa madeni, kuanzia uwanja, maaskari na vitu vingine vyote fedha iliyobakia ni sh.milioni 1 ambayo inakwenda moja kwa moja kwa waathirika wa mabomu," alisema Mathew.

Alisema fedha hizo wanatarajia kukabidhi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda kuwakabidhi waathirika hao wa mabomu.

Mathew alisema watu wa mikoani wamevutiwa na pambano hilo ambalo mbali ya kuchangia, walitoa burudani nzuri kwa mashabiki, hivyo wamepewa mwaliko mkoani Dodoma kurudiana Aprili 22 au 23 mwaka huu.

Alisema mashabiki hao watapata burudani ya aina yake wakiwemo Wabunge wa Jamhuri ya Muungano Tanzania ambao watakuwa kwenye vikao vya bunge.

No comments:

Post a Comment