24 March 2011

Walimu vihiyo watemwa Sengerema

Na Jovin Mihambi, Sengerema

SERIKALI wilayani Sengerema imesitisha ajira za walimu 11 kwa madai ya kupatikana wakitumia vyeti vya kughushi na vingine vikiwa vya watu waliokwishafariki na
wengine wakiwa katika ajira zingine katika makampuni na vyuo mbalibali vya watu binafsi nchini.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni, Katibu wa Huduma za Walimu wilayani Sengerema, Bw. Deus Masota alisema kuwa mafaili ya siri ya walimu hao bado yako katika ofisi ya Ofisa Elimu wa Wilaya ya Sengerema lakini akathibitisha kuwa wamo katika orodha ya kufukuzwa kazi.

Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili, ulibaini kuwepo walimu wengine wilayani humo ambao wanatumia vyeti ambavyo ni vya kughushi na wengine walionunua kutoka baadhi ya vyuo vya elimu vikiwemo Chuo cha Ualimu cha Murutunguru kilichoko wilayani Ukerewe na Ilonga mkoani Morogoro.

Aidha, Bw. Masota alisema kuwa chimbuko kubwa la kuwepo walimu wanaotumia vyeti vya kughushi linatokana na Bodi ya Ajira kwa walimu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambao huwasiliana moja kwa moja na waombaji na kuhakiki vyeti vyao kabla ya kupewa ajira kutoka serikalini.

Alisema kuwa kwa upande wa Ofisi za Elimu, kuanzia ngazi za wilaya hadi mikoa, wao hupeleka maombi ya kupata walimu pamoja na idadi ya walimu wanaohitajika na kwamba ofisi hizo hazihusiki na kashfa hiyo.

Hata hivyo, alisema kuwa kibaya zaidi katika taaluma ya elimu nchini ni pale mtu wa kawaida anaponunua cheti wakati hana taaluma hiyo na kuongeza kuwa ndicho chanzo cha kuporomoka kwa elimu nchini na wanafunzi kushindwa mitihani yao ya mwisho.

No comments:

Post a Comment