Na Rehema Mohamed
SHAHIDI wa kwanza katika kesi ya wizi na kutakatisha fedha haramu zenye thamani ya sh bilioni 3.8 inayomkabili aliyekuwa Mhasibu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Justice Katiti na wenzake watatu, Bi. Paulina Ngowi (37) ameieleza mahakama kuwa aliandaa hati ya malipo ya sh. bilioni 1.4 ya makato ya kodi ya wafanyakazi wa TRA nchi nzima.
Bi. Ngowi ambaye ni mhasibu wa TRA alisema hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Kazi Kisutu mbele ya hakimu Bi. Waliarwande Lema wakati akitoa ushahidi wake mahakamani hapo.
Bi. Ngowi alidai kuwa Agosti 29, 2008 alipokea nyaraka na maelekezo kutoka kwa mhasibu wa mishahara, Bw. John Sangu ambapo alimpa nyaraka zilizoonesha jina la kila mfanyakazi na makato yake kwa ajili ya kuandaa malipo hayo.
Alidai kuwa alifanyia kazi maelezo hayo na kisha kuyapeleka kwa msimamizi wake ambaye ni mhasibu mfawidhi wa TRA, Bi. Dina Edward ili aipitie, kuichapa katika karatasi na kisha kutia saini yake.
Aliongeza kuwa baada ya hapo nakala hiyo ilirejeshwa kwake na yeye kuisaini na kisha kuipeleka ofisi ya mkurugenzi wa fedha kwa ajili ya masuala ya malipo. Hati hiyo ya malipo ni namba PV 0027217 ya Agosti 29, 2008.
Alidai kuwa baada ya taratibu zote mtunza hazina alitengeneza hundi ya malipo hayo ya sh. 1,426,450,684.05.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo yenye mashtaka zaidi ya 11 yakiwamo ya kula njama ni wafanyakazi wa benki wa NBC, Bw. Samwel Renju, Bw. Haggay Mwatonoka na Hope Lulandala.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kati ya Mei na Novemba 2008 jijini Dar es Salaam washtakiwa hao walikula njama na kuiba fedha za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Inadaiwa baada ya kufanya wizi huo, washtakiwa walizihamishia kwenye akaunti za kampuni mbalimbali za watu binafsi huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la jinai.
Ilidaiwa kwamba wakiwa waajiriwa katika ofisi za umma Juni 6 2008, waliiba sh milioni 960.1, Septemba 18, 2008 waliiba sh bilioni 1.4 na Novemba 20 mwaka huo waliiba tena sh bilioni 1.4 mali ya TRA.
No comments:
Post a Comment