*Issa Kijoti aacha simanzi
Na Waandishi Wetu, Dar na Morogoro
KIFO cha msaanii wa kundi la Five Star, Issa Kijoti kilichotokea katika ajali ya gari iliyosababisha pia vifo vya wasanii 13 wa kundi hilo, kimewagusa wengi na
hasa familia yake ambayo alikuwa akitegemewa na familia hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana nyumbani kwake Mtaa wa Kwa Kabuma, Mtoni Kwa Azizi Ally, mama mzazi wa marehemu Kijoti, Amina Mohamed alisema hajui hatima ya maisha yake.
"Ninao watoto wengine, lakini Issa ndiye alikuwa mama yangu na baba yangu, ndiye alikuwa akijua nimekula, nimevaa nini na hata wakati wanaondoka wiki iliyopita, aliniachia hela na kunisisitiza kuwa, zitanitosha hadi atakaporejea kesho (leo)," alisema mama huyo huku akibubujikwa na machozi.
Kwa mujibu wa mama huyo, marehemu ameacha mtoto mmoja Nasra Issa (3), ambaye mama huyo ndiye anayemlea, baada ya mama mzazi wa mtoto huyo kufariki mwaka juzi.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa, huku akibembelezwa na akina mama wenzake, mama huyo alisema hajui hatima ya maisha yake, baada ya kutokea kwa kifo cha mwanaye.
Katika maeneo ya jirani ya nyumbani kwa mama huyo kuanzia Mitaa ya Sabasaba, ndani ya baa ya Equator Grill na Mitaa kadhaa ya Temeke, watu na hasa vijana walionekana kukaa kwa vikundi vikundi wakizungumzia msiba huo.
Naye Mwandishi Wetu kutoka Morogoro, anaripoti kuwa ajali hiyo ilitokea katika barabara ya IringaĆ¢€“Morogoro kwenye eneo la Doma, ndani ya Hifadhi ya Mikumi juzi usiku.
Akizungumzia kuhusu ajali hiyo mjini hapa jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Adolphina Chialo alisema ajali hiyo ilitokea saa 2.30 usiku katika eneo hilo.
Alisema gari lenye namba za usajili T 351 BGE toyota Coaster likiwa na wasanii wa kundi la Five Star likitokea Iringa liligonga gari lenye namba T-848 APE, Scania likiwa na trela lenye namba T-559 BDL lililokuwa limepaki kando ya barabara likiwa na shehena ya Mbao.
Kamanda Chialo alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari la wasanii hao, ambaye alijaribu kulipita roli hilo lililosimama na baadaye kushindwa, mara baada ya kuona mbele kuna gari lingine likija kwa kasi na hivyo kuhofu kugongana uso kwa uso.
Chialo aliwataja waliokufa katika ajali hiyo na kutambulika kwa majina ya kisanii kuwa ni Nassor Madenge, Issa Kijoti, Husna Mapande, Shaban Jumanne 'Sheba Juma', Omar Hashim, Tizo Mgunde, Omar Tall, Muingereza Hassan, Hamis Omar, Maimuna, Haji Mzuwanda na mnenguaji mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana wa kikundi cha Kitu Tigo.
Aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Mwanahawa Ally (55) mkazi wa Magomeni, Suzan Benadict (32), Zena Mohamed (27) mkazi wa Mwembe Chai, Samira Rajab (22), Ally Juma (25) Rajab Kondo (25), Mwanahawa Khamis (38) mkazi wa Kimara, Issa Hamis 'Kamongo' mkazi wa Kinondoni na Shaban Khamis.
Alisema kuwa kati ya majeruhi hao 10 ni wanaume na wanawake ni watatu, aidha alidai kuwa hali ya majeruhi mpaka jana asubuhi walikuwa wanaendelea vizuri.
No comments:
Post a Comment