Na Godfrey Ismaely
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limetangaza operesheni ya kuwaondoa wadaiwa sugu katika nyumba zake kote nchini kuanzia leo, shughuli itakayoendana na
kuwaondoa waliopanga kinyume na sheria za shirika hilo.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Bw. Nehemiah Mchechu katika kikao cha pamoja na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kilichokutana na Menejimenti ya shirika ambacho kilifanyika Makao Makuu jijini Dar es Salaam jana.
"Ili zoezi la kuzijenga nyumba mpya lifanikiwe mapema kuanzia kesho operesheni ya kuwaondoa wadaiwa sugu wa NHC litaanza lengo likiwa ni kuyakusanya madeni yote tunayoyadai kwao kwa kuwa tumedhamiria kulifanya shirika liendelee kuwa na matumani kwa wananchi," alisema Bw. Mchechu.
Alisema kuwa makusanyo hayo yataenda sanjari na kuwachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya watu wanaohukua nyumba za shirika hilo na kuzipangisha kwa watu wengine kwa bei za juu tofauti na makubaliano ya mikataba.
Alisema wadaiwa hao wanadaiwa zaidi ya sh. bilioni 4.8.
"Shirika lipo kwa ajili ya maslahi ya Watanzania hasa kwa kuhakikisha kuwa linajenga nyumba zenye ubora ili ziweze kupangishwa na hata kuuzwa kwa wananchi kwa bei nafuu, lakini kuna baadhi ya wapangaji wamekuwa wakijinufaisha kupitia nyumba za shirika kwa kuwadidimiza wananchi hao hasa kwa kuzipangisha kwa bei kubwa hivyo hatuwezi kuwafumbia macho," alisema Bw. Mchechu.
Alisema baadhi ya shirika limekuwa likipangisha nyumba kwa bei nafuu lakini lakini wao wanazipangisha kwa wananchi kwa zaidi ya dola 50,000 kwa mwezi kitendo ambacho siyo cha haki na akiendani na madhumuni ya shirika.
Bw. Mchechu aliendelea kusema kuwa shughuli hiyo likiendelea kutekelezwa NHC lipo katika hatua za kujenga nyumba 15,000 ambapo 10,000 zitakuwa maalum kwauzia wananchi wenye vipato vya chini na 5,000 kwa ajili ya kuuza na kuzipangisha kwa wananchi wenye vipato vya juu.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Bw. James Lembeli ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kahama alisema kuwa dhumuni la kufanya ziara hiyo katika shirika hilo ni pamoja na kuangalia muundo wa shirika, kuangalia taarifa za utekelezaji pamoja na mikakati ya shirika katika miaka mitano ijayo.
"Ndugu wajumbe nimefurahi sana kupata taarifa zinazonivutia kutoka kwa menejimenti ya shirika ambayo imeshikilia nafasi yake hivi karibuni kwa kuhakikisha kuwa inayakusanya madeni yote yanayodaiwa kutoka kwa wateja sugu.
"Mfano awali nilielezwa shirika lilikuwa likidai zaidi ya sh.bilioni 9, nje lakini mara baada ya kujiwekea mikakati kabambe zimekusanywa hadi kufikia deni la sh.bilioni 4.8," alisema Bw. Lembeli.
Hata hivyo, Bw. Lembeli alitoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa linasaidia shirika hilo kwa hali na mali ili kufanikisha malengo yake ikiwa ni pamoja na kuondoa kodi ya ushuru (VAT) pamoja na kuibadilisha sheria iliyopo kwa sasa.
Jamani hebu acheni zenu hizo kila kila siku mnasema watu kutimuliwa miaka imepita watu wanaishi kama kawaida tunajua sasa hivi watu watatengeneza pesa ile mbaya hizi zote dili za kifisadi hakuna jipya hapa
ReplyDeleteWewe ni mmoja wa mafisadi waliokuwa wakilikwamisha shirika sasa unajua kusema baada yakutupwa nje ya shirika,sisi wapangaji tuna imani na management mpya inavyofanya kazi,acha chuki watanzania tunahitaji maendeleo.
ReplyDelete