*Amwekea Mosha ngumu kurudi Yanga
Na Elizabeth Mayemba
MWENYEKII wa Yanga, Lloyd Nchunga amesema hatambui kurudishwa madarakani kwa Makamu wake aliyejiuzulu hivi karibuni Davis Mosha.Akizungumza
Dar es Salaam jana, Nchunga alisema kama Mosha anataka kurudi madarakani anapaswa kufuata utaratibu kwa kupendekeza upya jina lake katika Mkutano Mkuu wa wanachama, ili achaguliwe upya.
"Hizi ni vurugu, na kurudishwa kwa Makamu huyo madarakani kumevunja kanuni na katiba ya klabu yetu, kama kweli Mosha anaitaka nafasi hiyo asubiri Mkutano Mkuu wa wanachama, ili achaguliwe upya," alisema Nchunga.
Alisema ni kweli wenye jukumu la kumrudisha Makamu huyo lipo kwa wanachama, lakini wanachama waliomrudisha walipaswa kusubiri hadi siku ya Mkutano Mkuu.
Nchunga alisema katika kikao cha Kamati ya Utendaji walichokaa hivi karibuni, waliamua suala la Makamu huyo lipelekwa katika Mkutano Mkuu wa wanachama ambao wataamua suala lake.
Mwenyekiti huyo alisema endapo Mosha, atapeleka jina lake katika mkutano huo, jina lake litaunganishwa na majina ya wanachama wengine ambao watakuwa wanawania nafasi hiyo.
Juzi baadhi ya wanachama wa klabu hiyo, walivamia nyumbani kwa Mosha na kumtaka arejee madarakani ili aweze kuinusuru timu yao katika mechi zao tatu zilizosalia za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Katika hatua nyingine, Mosha alisema leo anatarajia kutoa msimamo wake, baada ya kusikia matamshi ya Mwenyekiti wake na anafanya hivyo kwa lengo la kuinusuru klabu hiyo na migogoro.
"Leo nitaweka msimamo wangu kwa wanachama ninaipenda Yanga, hivyo sipendi kuona tunaelekea kwenye majibizano ambayo yataleta mgogoro mkubwa hasa katika kipindi hiki ambacho timu yetu inakabiliwa na mechi tatu za ligi," alisema Mosha.
No comments:
Post a Comment