29 March 2011

Lipumba: CCM yatumia matatizo ya Watanzania kuwanufaisha wachache

Na Benedict Kaguo, Mtwara

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba amesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatumia matatizo yanayowakabili
wananchi kuwanufaisha watu wachache huku Watanzania walio wengi wakiendelea kupata tabu.

Akihutubia maelfu ya wakazi wa Manispaa ya Mtwara katika Uwanja wa Mashujaa juzi jioni Prof. Lipumba alisema Serikali ya CCM badala ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili wananchi imekuwa ikitumia mwanya huo kuwanufaisha wachache.

Huku mvua kubwa ikinyesha katika uwanja wa mkutano, Prof Lipumba alisema ni jambo la kushangaza serikali inashindwa kutumia rasilimali zilizopo nchini kuzalisha umeme huku akitolea mfano uwepo wa gesi katika maeneo mbalimbali nchini kama vile Mkuranga, Mnazi Bay ,Pangani na Mto Ruvuma pamoja na makaa ya mawe wa Kiwira ili kuzalisha umeme.

“Badala yake ndugu zangu Serikali ya CCM imekuwa ikitumia matatizo ya umeme kuingia mikataba mibovu ya Dowans na kuwanufaisha vigogo wachach serikalini” alisema Prof. Lipumba.

Alisema kukosekana kwa mipango madhubuti ndio iliyosababisha nchi inaendelea kuwa na matatizo makubwa yakiwemo ya kiuchumi na kwamba badala ya kuhangaika kupata suluhisho la matatizo imekuwa ikiyatumia matatizo hayo kuwatajirisha wachache.

Awali Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bw. Julius Mtatiro alisema Serikali ya CCM imekuwa ikiendeshwa kiujanja ujanja kuanzia ngazi ya Taifa hadi ngazi mtaa.

“Nchi inaendeshwa kiwizi wizi kuanzia huko Ikulu hadi kwa watendaji wa mitaa, serikali imekosa mipango ya kukabili matatizo ya wananchi,” alisema Bw .Mtatiro.

Alisema leo wanawake wajawazito wakifika hospitali wanapata tabu huku wakitakiwa kwenda na nyembe na kubaisha kuwa kama serikali imeshindwa kuwanunulia wembe kwenye zahanati na hospitali itawezaje kuwaletea viwanda vikubwa vya korosho wakazi wa Mtwara.

“Ndugu zangu serikali isiyoweza kununua wembe kwa mama mjamzito itawezaje kujenga kiwanda kikubwa kwa wananchi wake wa Mtwara,” alisema Bw. Mtatiro.

3 comments:

  1. Hayati baba wa Taifa Mwl nyerere yeye kuna mambo mengi ya msingi aliyaona na ndiyo maana alikataa kufanya mikataba ya baadhi ya mali asili zetu za watanzania na kusema kwamba Pindi wananchi wangu watakapoelimika watafanya maamuzi yao wenyewe, Katuachia nchi imejaa nema, Madini kila aina, umeme bila mgao, maji tulipata bila shida na alikuwa mkali kuhusu huduma za afya.Sasa hivi idadi kubwa ya madini yetu inachukuliwa Nchi yetu ina maji ya kutosha, Lakini leo hii Hospitali hazina dawa, maji ya tabu, kama asemavyo muheshimiwa LIPUMBA hapa tofauti ya masikini na matajiri inazidi kuwa kubwa na hii ni baadhi ya hao wachache kutajirika kwa rasilimali ya nchi. Mimi naona watanzania wenzangu labda tukubali serikali ya mseto maana hizi purukushani zao zakisiasa hazitoisha leo wala kesho wakati sisi wananchi wa kawaida tunazidi kuteseka kuna watu wanaweza kusaidia na kuleta maendeleo, tukubali kuna baadhi ya viongozi kwenye chama tawala hawatufai lakini tuna vichwa kwenye vyama vingine kwa uchungu wa hali halisi tuliyonayo hawa watu watajituma na tupate maendeleo ya haraka kuliko kukaa watu mnapoteza muda kila kukicha siasa, Vikao visivyoisha ubadhilifu wa pesa zetu tu. Usia wa baba Taifa naona sasa ni wakati wa Muafaka kuwa elimu tuliyoitafuta sasa tuitumie.kazi kwenu wadau.

    ReplyDelete
  2. HAKI YA MUNGU MIMI SIKIELEWI VEMA CHAMA CHA CUF. HIVI CUF ITAIKOSOAJE CCM WAKATI NI MSHIRIKA WAKE?

    ReplyDelete
  3. Janja ya nyani! Wameona wamebanwa na CHADEMA kuhusu UCCM B au ndoa kati ya CUF na CCM. Wameona wanayosema CHADEMA ni kweli, na sasa wanantaka kujisafisha kijuujuu ili waonekane bado ni wapinzani. Wanampinga nani? Au CHADEMA? - kwa sababu kwa hali ilivyo hawawezi kuipinga CCM kwa sababu watakuwa wamejipinga wenyewe. CUF, ndoa yenu na CCM imekula kwenu!

    ReplyDelete