18 March 2011

Wabunge wataka ahadi JK kwenye bajeti

Na Tumaini Makene

HALI ngumu ya maisha inayowakabili wananchi wengi hivi sasa, ikichangiwa na uchumi wa nchi kutodhihirika mifukoni mwao, imeonekana kuwazindua wabunge
wengi ambao jana waligeuka mbogo, wakiichachafya serikali juu ya mwongozo wake wa kutayarisha mpango wa bajeti kwa mwaka 2011-2012.

Hali hiyo ilijitokeza jana katika semina ya wabunge juu ya usimamizi wa bajeti ambapo Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustafa Mkulo alikuwa akitoa maelezo juu ya mwongozo wa kutayarisha mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/12 kwa
kuzingatia mfumo wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano (2011/12-2015/16).

Walionekana kuguswa na suala la deni la serikali kuzidi kuongezeka kwa kasi ndani ya mwaka mmoja uliopita, kutoka dola bilioni 9 mpaka bola bilioni 11, ongezeko la asilimia 18, ambapo mmoja wa wabunge hao alisema 'kwa hesabu za watu milioni 40, kwa deni hili hata mtoto aliyezaliwa leo anadaiwa dola za Marekani 245 (zaidi ya sh 340,000), ilhali hakuhusika kukopa.

Wakionekana kukerwa na mipango mingi ya serikali kukosa utekelezaji, baadhi yao walisema watendaji wa serikali ni wabinafsi na wenye roho mbaya, kwa kuwa ni wakwamishaji wakubwa wa mipango na wakati mwingine wanashindwa kubuni vitu kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Ahadi za Rais Jakaya Kikwete, hasa zile za 'papo kwa papo' alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, nazo zilionekana kuwaumiza vichwa baadhi ya wabunge, hasa wale wanaotoka maeneo zilikotolewa ahadi hizo, wakitaka ziingizwe katika
mwongozo huo, ili zifanyiwe kazi katika utengenezaji wa bajeti na kisha zitekelezwe.

Eneo la vipaumbele vya serikali katika mwongozo huo wa mpango wa bajeti ya mwaka kwa kuzingatia mfumo wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano (2011/2012-2015/16), nalo lilionekana 'kuwakwaza' wabunge wengi waliochangia, wakisema kuwa havitekelezeki
wala haviwezi kubadili hali ya uchumi kwani ni vingi mno, vingine havina umuhimu kwa sasa.

Mapema Bw. Mkulo alibainisha vipaumbele 11, ambapo kila kimoja kilikuwa na vipengele takribani vinne. Vipaumbele hivyo ni; elimu, kilimo, mifugo na uvuvi, nishati, uendelezaji wa miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi, maendeleo ya viwanda, afya, maji, ardhi, nyumba na makazi, maendeleo ya rasrimali watu, sayansi
na teknolojia, huduma na fedha.

Mchangiaji wa kwanza, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Bw. Andrew Chenge alisema kuwa nguzo kuu tano zilizoainishwa katika mwongozo huo iwapo zitakubalika kuwekwa kwenye mpango zitakuwa mihimili mzuri ya uchumi, lakini vipaumbele ni vingi, akisema hali hiyo inatokana na 'kila mtu ndani ya serikali kuvutia upande wake'.

"Mwenyekiti kinachoonekana hapa ni kama kuna pressure groups ndani ya serikali. Vipaumbele hivi ni vingi mno. Tuchukue vichache, sina maana vingine havina maana, hapana, tuchukue vipaumbele ndani ya vipaumbele. Tulikomalie suala hili, maana kuna watu serikalini wamejipanga tu kuona mambo yao yanafanikiwa.

"Vipaumbele 12 lakini mwingiliano wake huuoni, tuangalie critical
components katika kila eneo, mimi nafikiri tuanze miundombinu, elimu, maji, kilimo na afya," alisema Bw. Chenge.

Bw. Hamad Rashid Mohamed alisema kuwa serikali haiko makini katika utekelezaji wa mambo yanayoamuliwa. "Mkukuta awamu ya kwanza haukukadiriwa utatumia kiasi gani cha fedha, naona tunaweza kuwa tunarudia makosa yale yale...sasa deni la taifa linaongezeka kufikia asilimia 18, sasa kama linaongezeka basi fedha hizo zionekane zimetumika wapi na namna gani.

"Sasa hata recurrent expanditure (matumizi ya kawaida) nayo inaingia katika mikopo na misaada. Hii ni hatari...miradi hiyo haionekani, the government is not serious (serikali si makini). Suala la vipaumbele pia ni vingi mno, tunaze na elimu, nishati, kilimo na miundombinu. Tuwe focused zaidi ili mambo yaonekane.

"Lakini pia hakuna discipline (nidhamu) ya maamuzi. Hakuna utekelezaji, nimemsikia Rais Kikwete akisema wazee wastaafu wa Afrika Mashariki walipwe ni kitu kizuri, lakini maamuzi haya yanatoka katikati lakini hayamo katika bajeti," alisema Bw.
Mohamed.

Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu alisema "tataizo la nchi si mipango. Ni utekelezaji wa mipango hiyo. Wenzetu wa Lesotho, Botswana, Rwanda na Burundi wanachukua mipango hii wanaifanyia kazi wanaendelea, sisi tunaoandaa tuko nyuma. Ukiwa na mwiba takoni na mguuni, unaaza kwanza kuutoa wa takoni ili ukae kisha utoe wa mguuni, sisi tunaanza kutoa wa mguuni, tunashindwa kukaa.

"Hakuna maamuzi, watendaji wa serikali wamejaa ubinafsi, watendaji wana roho mbaya katika utekelezaji. Tunapaswa tujikite katika maeneo machache ya ku-champion revenue (kuongeza mapato), kama vile bandari, kilimo, umeme...nilitegemea kuwa kilimo kwanza kingejikita kwanza katika mikoa isiyo na matatizo ya mvua, sasa hakina target.

"Kilimo kwanza kimekuwa ni power tiller, hii ni miradi ya watu...ni aibu kusikia mkuu wa magereza anaomba chakula...tatizo letu hapa mwenyekiti si mvua ni water management (matumzi ya maji0, Misri huko hawana mvua kabisa lakini hatuwafikii kwa sababu wana water
management...sasa watendaji kazi waache roho mbaya na ubinafsi," alisema Bw. Zungu 

Mbunge wa Singida Kusini, Bw. Tundu Lissu alisema kuwa kwa namna deni la taifa linavyozidi kuongezeka, linaiweka nchi katika wakati mgumu, kwa kuendelea kuwa tegemezi na nchi yoyote tegemezi haiwezi kuwa huru.

"Kwa mujibu wa waziri, deni la taifa limeongezeka kutoka dola bilioni 9.3 mwaka 2009 mpaka dola bilioni 11. 8 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 18...ingawa yeye anasema linahimilika, lakini nilikuwa napiga mahesabu hapa, kwa idadi ya watu milioni arobaini, hata mtoto aliyezaliwa leo atakuwa anadaiwa dola 275, hata kama
hakukopa.

1 comment:

  1. Ni vizuri kuona baadhi ya wabunge wamegundua baadhi ya wabunge walivyokuwa na roho mbaya na ubinafsi na kikubwa zaidi ni uzalendo. Sisi watanzania ni wazuri sana katika kuongea na hatukubali kushindwa hata siku moja, mnaambiwa kila siku maendeleo ya taifa lolote duniani bila VITENDO,na UZALENDO hakuna mabadiliko yeyote mapya zaidi ya kuona turundikiwa madeni tu kwa uzembe wa hao Phd. wenu hivi inakuaje hawa viongozi wanashindwa kwenda na wakati, nchi kama rwanda, burundi, licha ya matatizo yote yaliyowakuta wanaanza kutuona wajinga, hebu angalieni baadhi ya mikoa ilivyosahaulika sidhani hata kama zimo kwenye budget ya taifa lakini kwenye kulipa madeni ya serikali nazo zimo je kweli hii ni HAKI? ni aibu kwa taifa zima watu wanaongea kuhusu hali halisi ya uhuru tulionao angalau baadhi ya viongozi wanaona kuwa kunamabadiliko, tuwe wakweli hii miaka 50 ya uhuru wetu nyanja zote za maendeleo ya nchi zimo mikononi mwa watu je ni kweli tutafikia millenium goal na baaadhi ya hawa viongozi wanachangia kiasi kikubwa cha wananchi kupoteza uzalendo na kuleta makataba nchini. MUNGU TUSAIDIE.

    ReplyDelete