18 March 2011

JK: Msilegeze mitihani kufaulisha wengi

John Daniel na Edmund Mihale

RAIS Jakaya Kikwete amesema hakuna sababu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kulegeza utungaji mtihani wa kidato cha nne ili kuongeza idadi ya
wanafunzi wanaofaulu.

Pia ameagiza wizara hiyo kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu, maabara na madarasa zinatumika kama ilivyopangwa bila kubadili matumizi yake.

Akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo na taasisi zake 11 katika ziara yake ya kutembelea wizara hiyo jana, Rais Kikwete alisema kinachotakiwa ni kusimamia ubora wa elimu na si kulegeza kamba katika utungaji mitihani.

"Tusipunguze viwango vya kutunga mitihani ili watoto wetu wafaulu sana, hapana. Lakini lazima tuongeze kiwango cha ufaulu, wizara iandae mkakati. Tuwe makini sana, mtu anapoajiriwa awe ameiva na anajua kufundisha kweli," alisema Rais Kikwete.

Alisema serikali yake imejikita katika kuboresha elimu kuanzia awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu baada ya kubaini kuwa katika ukanda wa Afrika Mashariki Tanzania ilikuwa nyuma kielimu.

"Katika Afrika Mashariki Tanzania ndio nchi kubwa, lakini idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu na sekondari ni ndogo sana, ndio maana tulichukua hatua makusudi kuongeza idadi ya wanafunzi kuendana na idadi ya Watanzania," alisema Rais Kikwete.

Hata hivyo, wingi huo, alisema umeleta changamoto kubwa ya mahitaji ya walimu, madarasa, mahabara, nyumba za walimu na vitabu.

"Msi-reallocate (msibadili matumizi) fedha za vitabu, maabara na nyumba za walimu, si kila mwaka changamoto ni upungufu wa vitabu, nyumba za walimu na maabara, hapana." alisema Rais Kikwete.

Wakati huo huo, Rais Kikwete jana alielezwa kuwa ujenzi wa reli kutoka Isaka hadi Kigali na Keza-Gitega hadi Musongati na Isaka hadi Dar es Salaam unatarajia kugharimu dola bilioni 3.5 hadi dola bilioni 5.1 za Marekani.   

Akizungumuza katika mkutano wa wadau wa reli hiyo uliofunguliwa na Rais Kikwete, Dar es Salaam jana, Waziri wa Uchukuzi, Bw. Omari Nundu alisema kuwa tayari upembuzi yakinifu wa reli hiyo umefanywa kwa gharama zilizotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Alisema kuwa upembuzi yakinifu wa reli ya Isaka - Kigali; Keza Gitega - Musongati na kukarabati ya Dar es Salam - Isaka ulisimamiwa na Kampuni ya Kimataifa ya DB ya Ujerumani 2008.

Alisema upembuzi huo ulionesha kuwa reli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo ya kawaida kwa asilimia 90 na kontena asilimia 80.

Alisema ujenzi huo atakaokuwa chini ya ushirikiano wa Burundi Rwanda na Tanzania ni kutoka Isaka-Keza-Gitega hadi Musongati utagharimu dola za Marekani bilioni 2.63.

Bw. Nundu alisema kuwa mradi huo pia utagharamia ukarabati wa na kuwa ya kisasa yenye uwezo makubwa wakubeba mizigo reli ya Dar es Salaam hadi Isaka gharama ya dola za Marekani 995.96.

Alisema pia fedha nyingine dola za Marekani 912.1 zitatumika kujenga reli mpya ya kisasa na dola za Marekani bilioni 2.47 zitatumika kujenga reli itakayopitia Bandari ya Bagamoyo.      

Akizungumza katika mkutano huo Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa reli hiyo itakapokamilika itakuwa faraja kwa Tanzania kwa kuwa itakuwa na uwezo mkubwa wa kubeba mizigo kuliko ilivyo ya sasa.

3 comments:

  1. Na Bob Nyachia
    Ni kweli umenena JK lakini cha kushangaza sijui nhao mawaziri wako wanafanya kazi gani hawana kazi watimue sie vijana wachapa kazi tupo,tupatie fursa tupige mzigo tuoakoe taifa letu

    ReplyDelete
  2. Ngeleja na Masha ni vijana kama wewe walituambia hayo hayo... sasa ona umeme wa mgao na vitambulisho vya raia ni hadithi

    ReplyDelete
  3. Hamnazo kweli Rais wetu, si ni wewe ulitaka mitihani ya darasa la 4 ifutwe au ishushwe kiwango ili wengi wamalize skuli au sio ww? Sasa unasema nn leo? Mara mbele mara nyuma hata sikuelewi. Nchi imechoka kuliko wakati mwingine wowote.

    ReplyDelete