14 March 2011

Vimbwanga Loliondo

*Waliokimbia hospitali, wakutana na daktari wao kwa babu
*Betrice Shelukindo aeleza alivyoponywa na mchungaji

Na Waandishi Wetu
 
TIBA inayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa KKKT (Babu), Ambilikile Mwasapile katika kijiji cha Samunge, Loliondo, imeendelea
kuonyesha maajabu yake baada ya wagonjwa kadhaa wa hospitali mbili kubwa nchini kukutana na madaktari wao kwenye foleni, kila mmmoja akitafuta uponyaji.

Wakati hayo yakiendelea, Mbunge wa Kilindi mkoani Tanga, Bi. Beatrice Shellukindo ametoa ushuhuda tiba hiyo ya Babu si jambo la mzaha bali inaponya, yeye amenufaika nayo, pamoja na ndugu zake 18 alioongozana nao.
 
Wakizungumza na majira kwa nyakati tofauti siku chache baada ya kurudi walikokwenda kufuatilia tiba hiyo, baadhi ya wanachi walithibitisha wagonjwa hao kupigana vikumbo na madaktari wao kwenye foleni kila mtu akijaribu kutatua tatizo lake.
 
“Sisi tulikwenda baada ya kushauriwa na daktari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambaye anamtibu ndugu yangu. alitwambiwa moja kwa moja ya kwamba tumpeleke mgonjwa wetu kwa Babu,” alisema Timothy Ndalichako, mkazi wa Njoro, mjini Moshi.
 
Alisema siku chache baada ya kupewa ushauri huo ambao ulitiwa chumvi na kuenea kwa taarifa za huduma ya Babu, walitafuta taratibu za kumpeleka ndugu mgonjwa huyo Loliondo na kufanikiwa kuipata baada ya siku mbili kwa kuwa wakati huo msongamano ulikuwa haujawa mkubwa.
 
“Tukiwa kwenye foleni siku ya pili, ndipo tukamuona daktari aliyetushauri akiwa ameandamana na wenzake kwenye gari, nao wakiwa wanaingia eneo la tiba Loliondo,” alisema.
 
Aidha alisema alichogunduwa ni kwamba madaktari wengine kutoka hospitali hiyo maarufu hapa nchini na nje ya nchi pamoja na wale wa hospitali nyingine za mjini Moshi, walishafika na wengine walikuwa wakiendelea kufika eneo hilo kufuatia tiba hiyo mbadala.
 
Kwa upande wake, Bw. Manase Kiara, alidai kukutana na daktari bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, aliyekwenda Loliondo kufuatia tiba hiyo.
 
“Niliondoka na wenzangu baada ya kujipanga kwenda kupata tiba baada ya kuhangaikia kwa muda mrefu Muhimbili. Kufika huko mimi na wenzangu tulikutana na dokta wetu ambaye baada ya kusalimiana naye tu alituambia mpeni Mungu yaliyo yake Mungu na ya Kaisari mpeni Kaisari,” alisema.
 
Wakati huo huo baadhi ya wananchi wa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro wameipongeza serikali kwa tamko lake kuwa haijazuia huduma ya tiba inayotolewa Mchungaji Mwasapile kwa miezi kadhaa sasa.

Shellukindo atoa ushuhuda wa tiba


Mbunge wa Jimbo la Kilindi mkoani Tanga, Bi. Beatrice Shelukindo amesema akiwa na ndugu zake 18 wakiwa na matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwemo yeye mwenyewe kusumbuliwa na magonjwa mbalimbali kwa muda mrefu, wamefika kwa Babu na kupata tiba.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu akiwa Arusha jana baada ya safari iliyomchukua wiki nzima, Bi. Beatrice alisema sio jambo la mzaha, dawa ya Babu inaponya.

Bi. Shelukindo alisema walifika katika Kijiji cha Samunge wilayani Ngorongoro Machi 7, mwaka huu, lakini kutokana na wingi wa wagonjwa walipata tiba Machi 11 yeye na ndugu zake, na baada ya hapo kila mtu akajisikia amepona, wakiwemo waliokuwa wanasumbuliwa na saratani.

"Mimi mwenyewe nilikuwa nasumbuliwa na presha na vidonda vya tumbo kwa muda mrefu, lakini baada ya kunywa kikombe kile cha dawa nilipona, tangu Ijumaa sijagusa kabisa kidonge cha aina yeyote, iwe kwa ajili ya vidonda vya tumbo au presha.

"Lakini maajabu yapo kwa mtoto wangu wa kike, akiwa na miaka 37 tulimpeleka hajiwezi na hajaweza kula wala kusema kwa miezi sita, zaidi ya kunywa uji tu kwa vile alikuwa anasumbuliwa na kansa, lakini baada ya kutoka hapo, kwanza tulishangaa baada ya kutaka tumpe chakula.

"Na kutokana na shida ya safari, wakati wa kurudi tulimuandalia ndege ya kurudi Dar es Salaam alikataa na jana Jumamosi (Machi) amerudi kwa basi. Mwingine ni mama mdogo alikuwa anasumbuliwa na presha mbaya, lakini ghafla amepona," alisema Bi. Shelukindo.

Bi. Shelukindo alisema pia alikwenda na ndugu yake mwanaume, yeye alikuwa anaumwa macho kiasi ambacho moja lilipasuka, lakini alipofika kwa Babu na kunywa dawa amepona, na ndugu zake wote aliokwenda nao wanaendelea vizuri.

"Yusuph (mwandishi) nakusihi sana uende kwa yule mchungaji. Sio vitu vya kubuni, dawa yake inaponya. Hakika ndugu zangu wote wamepona. Ni kweli imani pia ni muhimu katika kutumia dawa hiyo, lakini yenyewe bado inaponya, na inaanza kufanya kazi siku moja mpaka saba tangu unywe dawa hiyo," alimaliza kwa kutoa ushuhuda huo Bi. Shelukindo.


Mazingira yaanza kuwekwa sawa

Hofu ya usalama ilikuwa imetanda kwenye Kijiji cha Samunge imeanza kuondoka baada ya serikali wilayani Ngorongoro
imesema kuanza uboresha wa miundombinu, usafi wa mazingira na kuweka utaratibu mzuri wa wagonjwa kupata tiba.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Elias Wawa Lali alisema jana kuwa
siku chache tu zijazo wananchi watapata tiba hiyo kwa muda mfupi na katika mazingira safi na salama kwa kuwa tayari wameanza jitihada za kukamilisha mpango huo kwa kushirikiana na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati.

Kwa mujibu wa DC huyo kanisa hilo limesema kuwa watahakikisha wananchi hawapati tena taabu walizokuwa wakizipata siku kadhaa zilizopita za kukaa siku zaidi ya tano bila tiba huku wakitishiwa na hatari ya kimazingira kwa afya zao.

 “Kila mmoja anazungumza habari ya Loliondo hata yule ambaye hana taarifa sahihi za huko, lakini uhakika ni kwamba tayari mipango yetu inakwenda vizuri tunachozubiri na
wataalamu hao wa ujenzi kutuletea tathimini nzima ya kinachohitajika huko,” alisisitiza DC.
 
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Askofu Thomas Laiser alisema kanisa hilo katika kuhakikisha azma yao inatimia linatarajia kutumia zaidi ya sh milioni 75
katika kuboresha mazingira ya tiba hiyo.

Fedha hizo ni kwa ajili ya kujenga majengo maalumu yenye uwezo wa kuhudumia watu zaidi ya 600 kwa wakati moja, huku kukiwa na huduma bora za matundu ya vyoo na maji safi na salama ya kutosha.

Aliongeza wachoraji na wasanifu wa majengo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi hiyo, Bw. Ezrael Kariyongi hivi sasa wapo kijijini Samunge wakifanya tathimini ya mradi huo.

Alisema kuwa hata hivyo bajeti hiyo itategemea taarifa ya mchanganuo wa ujenzi huo ambapo utekelezaji wake utafanyika ndani ya wiki mbili zijazo ambapo mchungaji huyo ataendelea na tiba hiyo.

Imeandaliwa na Yusuph Mussa, Korogwe; na Heckton Chuwa,
Moshi; na Said Njuki, Arusha

15 comments:

  1. Mwenye masikio na asikie haya ambayo yanatendeka kwa BABU Ambilikile.......Kizito!!

    ReplyDelete
  2. Bwana Asifiwe sana kwa kumthibitisha mtumishi wake. Na wale wapinzani waliokuwa wanatukana washindwe sana na walegee

    ReplyDelete
  3. Babu kula vichwa chapchap, hawakawii kugeuka hawa. Hivi kama dawa inafanya kazi ushuhuda wa nini? Hawa na babu lao moja mtakuja tuambia. Na kanisa lake linajitia kimbelembele kujenga miundo mbinu litakuja aibika likome! Nyie tulieni tu hata DECI walikuwa wachungaji, watu wakionywa wanajidai kichwa ngumu walipolizwa ooo serikali mbaya haitulindi! Unajua hata DECI kuna walionufaika kweli lakini wengi walilizwa! Babu wanyweshe maji mpaka wakomae! Ongeza na bei ili uwaingize mtaroni jumla jumla! Wenzetu wanajenga hospitali za kisasa sisi tunang'ang'ania uganga! Kweli Tanzania kichwa cha mwendawazimu!

    ReplyDelete
  4. mchangiaji mwenye maoni hapo juu anapaswa afungiwe uwezo wa kufikili na mungu ili cku nyingine acwe na mawazo ya kipumbavu namna hii.na mungu amsamehe. na babu atambue kama hizo ni changamoto ktk kazi.

    ReplyDelete
  5. Saa Inakuja sijui tutalia naniTz?

    ReplyDelete
  6. Hii ni sawa kabisa na enzi za NUHU, ni pale Safina itakapo fungwa ndipo tutajua mbivu na mbichi, kama anayesimama madhabahuni na kuhubiri neno la mungu anaenda kwa babu na kuamini kuwa anatapoma kisukari na presure inayomsumbua kwa miaka mingi? iweje wewe unaye hubiriwa uwe mbishi kukubali hilo? amka , angalia muombe mungu akuonyeshee kitu, mkubali babu wa kinyakyusa anaweza kukupunguzia mizigo yako na hata kuitua kabisa nenda kwa babu ukaponywe acha kufananisha uponyaji huu na siasa itakugharimu sana kwa matamshi yako.na wala usiseme nchi yetu ni sawa na kichwa cha mwendawazimu, kumbuka bila wewe kuwa mwendawazimu hii nchi isingekuwa na wendawazimu wewe umechangia kuipotosha nchi hii na watu wake. ubarikiwe na bwana na muombe mungu akufungue akili na macho pia masikio yako yasikie sauti za malaika. mtu anapona ukimwi, kisukari na vipimo vinaonyesha yupo safi ww unakataa????????? fanya mabadiriko ya haraka kijana, milango inafungwa sasa.Amina

    ReplyDelete
  7. Kijana Mungu akusamehe! Muombe Mungu akufungulie milango, umefungwa minyororo. Jiulize, kwani kabla ya hospitali babu zako walitibiwa na nini kama sio mitishamba? achalia mbali kuwa babu kapata maono ya hiyo dawa.

    ReplyDelete
  8. Watu wa mungu inatupasa tumshukuru mungu sana kwa kutuletea tiba hii mbadala kwani bila nguvu zake yeye sisi hatuwezei (jua sio babu bali ni mungu anafanya)Amina ubarikiwe

    ReplyDelete
  9. Mungu mkubwa!kwa ambaye hajafika lazima aropoke, tiba kwa wote habagui katoliki,kkkt,islam,mlokole,wala asie na dini,ni nabii kama kina Musa we unabisha,kaa na presha na sukari yako,kama nauli nenda omba kwa wasamaria!safari njema.Amina.

    ReplyDelete
  10. yetu macho, ni kawaida yetu watanzania kupapatikia vitu tusivyokuwa na uhakika navyo, na ni wepesi wa kusahau pia, YETU MACHO

    ReplyDelete
  11. HAKUNA HAJA YA MALUMBANO MAANDIKO HUDAI IKIWA KAZI HII IMETOKA KWA BINADAMU ITAVUNJWA LAKINI KAMA IMETOKA KWA MUNGU HAIWEZI KUVUNJWA

    ReplyDelete
  12. KAZI YA MUNGU ITADUMU MILELE DAIMA; LAKINI TUTAMBUE HATUWEZI KUYAJUA MAPENZI YA MUNGU KWA KUONGEA BALI TUZIDI KUOMBA. INOCENT SHAYO

    ReplyDelete
  13. ambaye amwamini babu, aendelee hivyo hivyo. ila sisi 2nakunywa dawa na tunaendelea kupona

    ReplyDelete