14 March 2011

CHADEMA yawajia juu Membe, Sofia

Na Tumaini Makene

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewataka mawaziri wawili, Bw. Bernard Membe na Bi. Sophia Simba, kuthibitisha kauli zao kabla
hakijachukua hatua za kisheria, juu ya shutuma dhidi yake kuwa kinafadhiliwa na baadhi ya mataifa ya nje, kufanya maandamano ya kuchochea ghasia na kuvuruga amani ya nchi.

Kimesema kuwa hakijawahi kutamka kuwa kinataka kuiondoa serikali kinyume cha katiba, bali kinafanya maandamano kwa mujibu wa haki ya kikatiba (ibara ya 8), inayoeleza kuwa madaraka ya nchi yako mikononi mwa wananchi, hivyo kinapoona njia za kidemokrasia bungeni na mabaraza ya halmashauri zimeshindikana daima kitarudi kwao.

Chama hicho kimewataka Bw. Membe (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa) na Bi. Simba (Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto), kuweka hadharani wafadhili hao wa nje, balozi au mataifa hayo yanayokifadhili, kwani huo ni ukiukwaji mkubwa wa moja ya kanuni za msingi katika uhusiano wa kimataifa na diplomasia.

Kimeeleza kuwa iwapo kauli hizo hazitathibitishwa kwa kutolewa mifano, wananchi watazichukulia kuwa ni propaganda za serikali dhidi ya vyama vya upinzani, zikifananishwa na namna Chama cha Wananchi (CUF) kilivyozushiwa kuagiza visu kutoka nje ya nchi, kwa ajili ya kuanzisha ghasia nchini, lakini mpaka leo visu hivyo vinaendelea kuuzwa mitaani.

Hivi karibuni, mawaziri hao wamenukuliwa na Shirika a Utangazaji la Taifa (TBC1) na vyombo vingine vya habari, wakisema kuwa kuna chama cha siasa nchini kinafadhiliwa kwa kupewa fedha na nchi za nje ili kianzishe maandamano nchini yenye lengo la kuanzisha ghasia na kuvuruga amani ya nchi.

Wa kwanza kutoa kauli hiyo wakati akitangaza maadhimisho ya siku ya wanawake duaniani alikuwa Bi. Simba ambaye alinukuliwa akisema kuwa chama hicho kinawafadhili kutoka nje ya nchi wanaokifadhili.

Alisema kuwa lengo la wanasiasa wa chama hicho kufanya maandamano katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ni kutafuta umaarufu kwa shinikizo la wafadhili wa chama hicho ambao serikali imeshawatambua kwani ndio wanaosababisha migogoro nchini Misri, Kenya, Libya, Tunisia na nchi nyingine za Afrika na sasa wamepania Tanzania.

Akizungumza jana Dar es Salaam na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John Mnyika, alisema kuwa kauli hizo hazipaswi kutamkwa kisha kuchukuliwa kama mzaha, na iwapo serikali itashindwa kuthibitisha zitaonekana kuwa ni dalili ya serikali kutapatapa.

Bw. Mnyika alisema "zitachukuliwa kuwa ni dalili za kutapatapa na propaganda za mara kwa mara zinazozushwa dhidi ya CHADEMA, hivyo wananchi watazipuuza kama walivyopuuza propaganda za ukabila, udini na uhaini. Mtakumbuka hata CUF waliwahi kuzushiwa kuwa wameingiza kontena la visu nchini kuvuruga amani, lakini visu hivyo vipo vinauzwa".

"Takribani wiki sasa kumekuwa na kauli katika vyombo vya habari zikitamkwa na viongozi wa serikali kuonesha kuwa CHADEMA kinafadhiliwa na balozi mbalimbali kufanya maandamano ya uchochezi na kuvuruga amani, Waziri Sophia Simba alinukuliwa na Gazeti la Majira Februari 26, mwaka huu akisema hivyo.

"Kisha Machi 3 akiwa katika kipindi cha TV Channel Ten, Sophia kwa nafasi yake kama waziri alisema tena kwa kukitaja CHADEMA kuwa kinafadhiliwa na watu kutoka nje, kisha kinawalipa watu fedha kwa ajili ya kufanya maandamano. Machi 7 mwaka huu tena, akiwa katika kipindi TBC;

"Aliwataka wanawake wasijitokeze katika maandamano ya CHADEMA kuwa ni ya vurugu na kuwa CHADEMA kinapewa fedha na wafadhili kwa ajili ya kufanya maandamano ya vurugu. Jana (juzi) Waziri Membe naye akiwa katika kipindi cha TV alisema kuwa kuna chama kinafadhiliwa na balozi za nje kuvuruga amani ya nchi.

"Ingawa Membe hakutaja jina, lakini ukiangalia mtiririko wa logic (mantiki) unaona kuwa kwa kauli hizo serikali wanazungumza kitu kimoja juu ya CHADEMA...kwa kuwa Membe kasema kuwa anazo tuhuma tayari na wanazichunguza basi ni vyema akawaambia Watanzania ni chama gani, nchi gani zinazokifadhili na kwa kiasi gani," alisema Bw. Mnyika.

Aliongeza kuwa chama hicho hakijawahi wala hakina utaratibu wa kufadhiliwa kwa nia ya kuvuruga amani ya nchi, kwani hata maandamano wanayoyafanya ni ya wananchi wakiguswa na agenda za kitaifa zinazobebwa na CHADEMA.

Alisema kuwa mara baada ya Bw. Membe kuzitaja nchi hizo, nazo pia zinapaswa kujitokeza kuzungumzia jambo hilo, kwani ni zito, si la kupita 'hivi hivi'.

Bw. Mnyika alisema kuwa chama hicho kitaendelea kuwajibika kwa wananchi kwa kutumia fursa zote zilizopo, kupitia vyombo vya maamuzi kama bunge na mabaraza ya halmashauri lakini iwapo demokrasia itaminywa huko, kitatumia haki ya kikatiba ya kuandamana, katika kushinikiza serikali itimize wajibu wake.

"Ni kawaida ya mawaziri wa CCM kutoa uzushi dhidi ya CHADEMA, walianza na ukabila, wakaja na udini, kisha uhaini wa kutaka kuiangusha serikali, zote zinaonekana hazikushika kasi, sasa wamekuja na ufadhili...hakuna mahali popote tumesema kuwa tutaiondoa serikali kinyume cha katiba, lakini tunatumia kama haki ya kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 8 kushinikiza mambo fulani yafanyike.

Akizungumzia juu ya tatizo la bei ya mafuta, ambapo moja ya sababu imekuwa ikielezwa kuwa ni kupanda kwake katika soko la dunia, Bw. Mnyika alisema kuwa pamoja na ukweli huo, serikali bado ina jukumu la kuhakikisha sababu za ndani zinadhitiwa ili kusaidia hali isiwe mbaya.

"Kweli pamoja na mambo yanayotokea huko Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati, hicho kimekuwa ni kisingizo pekee cha Serikali ya CCM, akisema bado ziko sababu za ndani za kupanda kwa be ya mafuta, kama vile mfumo wa kodi, hivyo akaitaka itoe kauli kwani hali inazidi kuwa tete.

"Lazima serikali iwe na mikakati ya namna gani tunakabiliana na tatizo hili la mafuta, katika nchi zingine kuna mkakati wa kuwa na akiba ya mafuta...hapa mwaka 2008 Waziri Ngeleja aliwahi kuzungumzia juu ya Shirika la Mafuta la Taifa, lakini mpaka leo hakuna kinachoendelea...hii ingeweza kutusaidia dhidi ya chochote kinachotokea duniani.

Alisema kuwa kwa sababu sasa uandaaji wa bajeti ya serikali uko katika hatua za awali, serikali inapaswa kufikiria mfumo wa kodi kwa mafuta, kwani nao unasababisha kupandisha bei na hatimaye ugumu wa maisha kwa wananchi.

Alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa Serikali ya Japan na wananchi wake kwa ujumla, kwa janga la tetemeko la ardhi, akisema Wajapan ni washirika wa maendeleo wa nchi ya Tanzania kwa muda mrefu.

6 comments:

  1. Tuambine nyie kabla ya kampeni hamkuwa na pesa mpaka mkawa mnachangiwa na wananchi na Sabodo akawapa pesa za kampeni. Sasa hizo pesa za maandamano bilioni 20 mmezitoa wapi?

    Mbona zamani mlipopewa pesa na chama cha conservative cha London aka Torry mlikuwa wawazi na mkasema mmetumia hizo pesa kwa kukodi helikopta leo hii mbona hamtaki kusema mapesa yote hayo mumeyatoa wapi? Nani kawapa? Yaani nyie kuweni wazi tu!

    ReplyDelete
  2. hiv ww boya uliyetoa maoni yako hapo juu hautambui kuwa chama kinapokuwa na wabunge wengi na ruzuku yake inaongezeka? kumbuka huko nyuma chadema walikuwa na viti vichache sana kuwa mjanja acha kutetea hiyo mifisadi yako yenye mawazo mgando tunachotaka hapa watutajie hao wafadhili na siyo kuuliza hela wametoa wap? haikuhusu hatawangetoa zao mifukoni tena wakiishiwa hata wananchi tutawachangia.

    ReplyDelete
  3. Nafiri una upeo mdogo sana wa kuelewa masuala ya kitaifa na kimataifa, nasema funga domo lako maana hujui unachoelezea 'you're just a political novice'

    ReplyDelete
  4. Kwa waziri kukurupuka ni aibu tena mno! halafu huo mtindo wetu wa kila waziri kuongea na kusema serikali imesema nina wasiwasi nao. Hata akitoa pumba utamsikia "serikali imesema", waziri mwingine nae akisema hata kupingana na waziri mwenzake utamsikia "serikali imesema". Dada yangu Sophia usiongee mno na kuamkia kwenye front page kwa mara kadaa kwa kauli zako pengine zisizo nzuri! Nawe Membe, kumbuka ulitumwa kwenda kupitia sahihi kwenye Umoja fulani hivi... ukaishia kunuka tu! Pima kwanza!

    ReplyDelete
  5. cadema msihofu hiyo ni dalili ya CCM kufa

    ReplyDelete
  6. sishangai kwa sophia simba kukurupuka na kusema utumbo maana ndio aliouzoea ila nashangaa kidogo kwa mhe. membe maana nilikua namwona kama ni at least afadhali kidogo katika hiyo safu ya madudu ya kikwete...mh hivi tutafika salama 2015?maana kila mtu akiamka na madudu yake haya we

    ReplyDelete