15 March 2011

Ushuru wa mazao watozwa shambani

Na Yusuph Mussa, Korogwe

WANANCHI waishio kwenye Mji Mdogo wa Mombo wamelalamika kuwa wakulima wa eneo hilo wanatozwa ushuru wakati wanatoka kuvuna mazao yao
shambani.

Pia mkulima yeyote anayebeba kuni kutoka shamba ni lazima atozwe ushuru wa kuni hizo, huku wakihoji watoza ushuru wanaitumikia Serikali ya Kaisari au ya Rais Jakaya Kikwete.

Wananchi hao walitoa malalamiko hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani maarufu kama Profesa Majimarefu.

Mkulima katika Mradi wa Kilimo cha Mpunga Mombo, Bw. Shaban Athuman alisema wakulima wanaotoka shamba wakiwa wamevuna mazao yao wanapeleka nyumbani, wakifika kwenye kizuizi cha  ushuru na wao wanajumuishwa watoe ushuru huo.

“Hivi huyu anayechukua ushuru wa mkulima anayevuna mazao yake kutoka shambani anafanya kazi hiyo kwa mamlaka ya nani? Hivi hata mazao yanayovunwa shambani yanatozwa ushuru?

“Siku akiamua kwenda kuuza sokoni au mnadani anachukuliwa tena ushuru, hivi kweli hiyo sera ya Kilimo Kwanza na uonevu huu anaofanyiwa mkulima kuna siku itamkomboa?

"Kibaya zaidi huyu anachukua ushuru anasema haiogopi serikali wala polisi anaringia nini huyu,” alisema Bw. Athuman, huku akishangiliwa na wananchi.

Mwananchi mwingine, Bw. Juma Killo alimwambia Bw. Ngonyani kuwa wananchi wa Mombo hawapo Tanzania, na kama wangekuwa Tanzania siku nyingi wangeweza kusaidiwa kwa kuwa tatizo la kulipa ushuru kwa mazao yao shambani ni la muda mrefu.

“Mbunge, huyu bwana anayechukua ushuru wa akina mama waliobeba kuni kichwani, ama wakulima wanaotoa mazao yao shambani sio Mtanzania ni (raia wa nchi jirani), na wala haitumikii Serikali ya Tanzania bali nchi jirani,” alisema Bw. Killo huku naye akishangiliwa na wananchi.

Bw. Majimarefu alisema anavyojua yeye anayetakiwa kulipa ushuru ni mfanyabiashara, lakini si mkulima anayetoa mazao yake shambani, hivyo hatakubali liendelee.

“Hili sikubaliani nalo, yaani mtu atoe mazao yake shambani halafu afike getini achukuliwe ushuru, na siku amekwenda kuanika mpunga achukuliwe ushuru mwingine? Hilo haliwezekani” alisema Bw. Ngonyani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Bw. Lameck Masembejo alisema haujui ushuru wa namna hiyo, labda Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mombo, Bw. Fuad Rashid anaweza kubaini.

Bw. Rashid alikana wakulima kuchukuliwa ushuru huo, na kudai ni wafanyabiashara tu ndio wenye wajibu wa kulipa ushuru kwenye kizuizi.

No comments:

Post a Comment