08 March 2011

Ushindi wampa jeuri Dalglish

LONDON, England

KOCHA wa Liverpool, Kenny Dalglish amesema anaona fahari kubwa kwa timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Manchester United, katika
michuano ya Ligi Kuu ya England uliofanyika juzi kwenye Uwanja  Anfield.

Mchezaji Dirk Kuyt, ndiye aliyefunga mabao yote matatu dhidi ya kikosi hicho cha kocha, Sir Alex Ferguson na kuamua kusamehe pointi katika mbio za kuwania ubingwa na Arsenal, katika michuano hiyo ya Ligi Kuu.

Mchezaji Javier Hernandez, ndiye aliyewapatia wageni bao hilo pekee, lakini halikuonekana kuwashtua Liverpool ambao walionekana kuwa imara muda wote wa mchezo.

Ushindi huo unadaiwa kuonesha mageuzi kwa kikosi hicho cha Anfield, ambacho kinaonekana kuwa imara tangu alipojiunga nacho, Kenny Dalglish aliyechukua mikoba ya Roy Hodgson, Januari na Mscotland huyo anasema ushindi huo ni moja ya hatua muhimu katika kikosi chake.

Akizungumza na Sky Sports baada ya mechi hiyo, kocha huyo alisema kwa ujumla ushindi huo ni mnono kwako na walistahili kupata sifa kwa jinsi walivyocheza na ameipenda kazi hiyo.

"Ni msimu mgumu na bado haujamalizika, lakini hizi ni pointi nyingi kwa mashabiki wetu," alisema kocha huyo.

"Tulikuwa tukisema kuwa tuna majeruhi kwa sababu kila mmoja alikuwa ni majeruhi, lakini walipoanza kurejea uwanjani tumeanza kuwa kimya na kupata nguvu kikosini." aliongeza.

Alisema kwamba wao ni kama kila timu inapokuwa na majeruhi wengi ni lazima iwe dhaifu kama ilkivyokuwa kwa Manchester United, hali ambayo ndiyo iliwasababisha wapate kipigo hicho.

No comments:

Post a Comment