LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa Chelsea, Fernando Torres amesema hana wasiwasi kuhusu kushindwa kufunga japo goli moja, tangu ajiunge na klabu hiyo akitokea
Liverpool.
Hadi sasa Torres, ambaye alijiunga na Chelsea kwa usajili uliovunja rekodi nchini Uingereza, baada ya kusajiliwa dakika za mwisho katika usajili wa dirisha dogo la Januari mwaka huu kwa kitita cha pauni milioni 50, bado hajaifungia bao klabu hiyo mpya baada ya kuichezea mechi nne.
Mchezaji huyo wa taifa wa Hispania, pia juzi alijikuta akiondoka kapa katika mchezo ambao timu hiyo iliondoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Manchester United, lakini Torres alisema alikuwa akifahamu itamchukua muda, ili kujiweka sawa katika klabu hiyo ya Stamford Bridge.
Akitetea ukame wake huo, Torres alisema anaamini ataondokana nao baada ya kuufahamu vyema mfumo ambao Chelsea inautumia kiuchezaji.
"Jambo la msingi ni kwanza kufahamu mfumo ambao timu yako inautumia kiuchezaji, jinsi gani unavyotumika katika mfumo huo na kila kitu," Torres aliliambia jarida la Chelsea.
"Jambo hili mara zote huchukua muda, lakini nafikiri unapolifahamu jambo hilo kila kitu huwa kinakwenda kirahisi," aliongeza na kisha akasema kwamba pia jambo la msingi ni kuwa na maamuzi tofauti katika mfumo unaotumia kucheza.
Torres alisisitiza kuwa na furaha kucheza sehemu yoyote katika timu hiyo ya Chelsea, baada ya kutumiwa kama mshambuliaji pekee kama ilivyokuwa kwa Liverpool.
"Unataka kuwa mchezaji mkubwa, ni lazima uwe tayari kucheza katika hali yoyote kama hii na nina uhakika kwa Chelsea, wakati mwingine nitacheza katika nafasi tofauti," aliongeza Torres.
Alisema kwamba yupo tayari kwa jambo hilo kwa sababu anapenda kucheza kila nafasi, ambayo atapewa na kocha na anafahamu ushindani katika timu hiyo ni mkubwa.
No comments:
Post a Comment